Bukobawadau

MASSAWE;Vijana Jishughulisheni na Ufugaji wa Nyuki ili kujikwamua kimaisha na Uchumi kuliko kutegemea serikali kuwatafutia ajira.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Fabian Massawe.
Muonekano wa Mzinga wa nyuki.
Kundi la vijana  katika wilaya zilizoko mkoani Kagera limetakiwa kujishughulisha na ufugaji wa nyuki kisha kujikwamua kimaisha kwa kuongeza kipato ,kiuchumi kuliko kutegemea serikali kuwatafutia ajira.

Mkuu wa mkoa wa Kagera ,Kanali mstaafu Fabiani Massawe ametoa wito huo katika uzinduzi wa kutundika  Mizinga ya nyuki kanda ya ziwa uliofanyika  katika  wilaya ya Biharamulo hivi majuzi

Kanali Massawe alisema kuwa vijana ndio kundi kubwa lisilokuwa na ajira wala mapato katika mfumo wa maisha kwa wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 na wanahitaji kujiajiri kwa kutumia rasilimali na maliasili zilizoko katika mazingira yao.
Aliwataka vijana hao kujiunga kwenye vikundi vya pamoja na kuanzisha ufugaji wa nyuki na kuweza kupata asali na nta kisha kupata soko  litakalosaidia kujiinua kiuchumi na kuongeza mapato katika familia ikiwa ni pamoja na  kuepukana na kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa kuvunja sheria. 
“Vikundi vikiundwa na kuonesha uhai serikali itatoa ufadhili wa fedha na kuendeleza miradi yenu kuliko kubaki maisha tegemezi na ombaomba kwa kutumia ardhi na misitu hii ya asili jirani na hifadhi za Taifa”.Alisema Massawe.



Awali Meneja na wakala wa huduma za Misitu kanda ya ziwa Bw. Haji Hatibu  alisema lengo la uzinduzi wa utundikaji  wa mizinga wilayani Biharamulo ni  kuhamasisha jamii kufuga nyuki kwa kutumia njia za kisasa na kuzalisha kwa wingi zaohilo   ambapo mizinga 100 yenye thamani ya Shilingi Milioni  7 , imezinduliwa na kutundikwa katika eneo la misitu lililotengwa .

  
Bw.Hatibu alisema takwimu inaonesha Tanzania ina hekta za misitu zipatazo Mil 34 ambazo ni makazi ya makundi ya  nyuki  yapatayo mil 9.2 yenye kuzalisha tani  130 za asali yenye thamani ya dola za kimarekani  Bil.133 na kuinua kipato cha mwananchi.



Kwa mujibu wa Meneja huyo alidai kuwa kutokana na uvunaji  jamii inaweza kutoa tani  9000 yenye thamani ya dola za kimarekani Bil 35 kwa kwa mwaka ambapo kwa sasa uwezo uliopo Tanzania inazalisha Tan 4800 za asali yenye thanani Bilioni 4.9 na nta tani 324 zenye thamani ya Bil 648 sawa na kutumia 3% ya uwezo tulionao wa  rasilimali zilizopo za asali na misitu .
“Kutokana na ufugaji wa nyuki  jamii inaweza kujipatia gundi ya nyuki , sumu ya nyuki inayotumika katika tiba pamoja na maziwa ya nyuki kama chakula na tiba “.Alisema hatibu.

Vilevile alifafanua kuwa  wananchi kwa kufuga nyuki wataweza  kupata huduma ya uchavushaji wa mazao na kuongeza ubora wa mazao na kuanzisha biashara ya kuuza makundi ya nyuki  akiwemo malkia wa nyuki kwa ajili ya kuongeza makundi yaliybora kwa kutumia fursa zilizopo.



Katika hatua nyingine aliwaasa wananchi na wafugaji kujiepusha na uharibifu wa mazingira kwa kuchoma na kukata miti na makazi ya nyukikwa kukosa maua na maji kisha kuzalisha kiwango kidogo cha asali na nta na hata kuhama katika mizinga baada ya kupata usumbufu wa makazi kimazingira.


Habari na picha Na:Shaaban Ndyamukama.
 
Next Post Previous Post
Bukobawadau