MKUU WA MKOA WA KAGERA AWATOA HOFU WANANCHI KUHUSU M23
Kagera. Serikali mkoani hapa imewataka wananchi walioko wilaya
zinazopakana na nchi jirani kutokuwa na hofu ya usalama baada ya tishio
la Kundi la Waasi la M23 la DRC kutishia kuvamia Tanzania.
Akiongea na wandishi wa habari wilayani Ngara,
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Masawe alisema kuwa,
wananchi wanatakiwa kutoa ushirikiano na kuwabaini watu wasio wafahamu
watakaojipenyeza kwa kutoa taarifa ili waweze kushughulikiwa kikamilifu
Masawe alisema, Serikali iko macho kuhakikisha
mipaka yake haivamiwi na kwamba kufuatia taarifa hizo hatua za kiusalama
zimeshachukuliwa kwa kutandaza vikosi mbalimbali vya usalama kwenye
mipaka yake na nchi jirani.
“Atakayejilengesha kuivamia Tanzania atakutana na
kilichomg’oa Nduli Iddi Amini wa Uganda katika vita vya mwaka 1978-79,
nami nilikuwa mpiganaji mahiri,” alisema Masawe.
Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kukagua
shughuli za maendeleo, Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Costantin Kanyasu
aliiomba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuingilia
kati na kuilinda mipaka ya Kijiji cha Kasange wilayani humo na ileya
vijiji vinavyopakana na Wilaya ya Giteranyi Burundi.
Kanyasu alisema, wananchi wa maeneo hayo
wanagombea ardhi kwa jili kilimo kwa kila mmoja kujiona kuwa yupo sahihi
ndani ya nchi yake na hivyo kuzua tafrani katika uhusiano wa pande zote
mbili.
Aliiomba Wizara ya Jumuia ya Afrika ya Mashariki
kufanya mazungumzo ili kupatikane suluhu ya usalama wa wananchi wa nchi
hizo mbili kwa kukaa meza moja pamoja na kudhibiti wahamiaji haramu
wanaotoka nchi wanachama wa shirikisho hilo bila kufuata taratibu za
kuhamia nchi nyingine.
Hata hivyo Kanali Masawe amewataka wananchi na
viongozi wa maeneo hayo kuwashauri wanaotaka kuingia nchini na kuishi
kujiandikisha kwa kufuata taratibu na kuwa raia wa kuandikishwa.