Bukobawadau

SIMULIZI:MAMA YANGU ADUI YANGU

WASWAHILI wanasena uchungu wa mwana aujuae mzazi, lakini kwa mama yetu ilikuwa kinyume. Sikuamini mama yetu mzazi kuwa chanzo cha matatizo ya familia yetu, pengine hata mimi kushindwa kufikia ndoto zangu za kusoma hadi chuo kikuu na kuishia kidato cha nne huku nikifeli vibaya.

Mwanzo sikuelewa lolote kwa vile nilikuwa na akili za kitoto na kuona kila kitu kiko sawa. Lakini nilikuja kuufahamu ubaya wa mama baada ya kuingia kwenye ndoa ambayo ilighubikwa na utata mkubwa na hapo ndipo nilipoyaona makucha ya mama. Ni mama yangu lakini kama asingekuwa mzazi wangu sijui tungefikishana wapi.

Mambo aliyonitendea mama yangu, kama mzazi aliyenizaa kwa uchungu, hakutakiwa kunifanyia kamwe . Lakini kama sitatanguliza shukurani nitakuwa mwizi wa fadhila. Waswahili wanasema mnyonge mnyongeni haki yake mpeni.

Kwanza kabisa lazima nitangulize shukurani zangu za dhati kwa mama yangu mzazi, kwa kunizaa na kunilea, pia kunipa elimu aliyonikadiria mwenyewe. Hiyo ni hatua kubwa sana katika maisha ya mwanadamu anayopitia akiwa mikononi mwa wazazi wake. Kabla sijafunguka akili nilimuomba Mungu katika maisha yangu aniwezeshe uwezo wa kulipa hata robo ya yote aliyonifanyia mama yangu, japo nilijua ni kazi kubwa. Toka nikiwa binti mdogo nilijua mama yangu ndiyo kila kitu kwa vile alijitoa kwa ajili yetu.

Maisha yote tuliishi na mama yetu, sikubahatika kumuona baba, nilielezwa alifariki mama yangu akiwa na ujauzito wangu wa miezi sita, kwa hiyo sura ya baba yangu niliiona kwenye picha tu. Siku nilipojua siri ya kifo cha baba nilikuwa hoi. Nimeamini nyuma ya mioyo ya watu kuna siri kubwa, ndiyo maana huwezi kujua dhamira ya mtu. Namuomba Mungu asinipe moyo wa mama.

Najua unataka kujua kwa nini mama yetu alituzaa ili ageuke adui yetu namba moja, kwa vile tuko pamoja naomba ungana nami ili siku moja ukubaliane na kauli yangu ili kina mama wenye roho kama ya mama yangu wabadilike.

Naitwa Mwaija mtoto wa mwisho katika familia ya marehemu mzee Salmini. Japokuwa sikubahatika kumuona baba yangu naambiwa nilifanana naye sana. Katika familia ya watoto watano, wa kike wanne na wa kiume mmoja. Baada ya kumaliza elimu yangu ya sekondari kidato cha nne nilipata mchumba wa kunioa.

Ukweli mchumba wangu hakuwa mgeni kwangu, ni mwanaume wangu niliyeanza naye urafiki tangu nilipokuwa kidato cha pili. Mwanzo tulifanya mapenzi ya siri japokuwa kati ya dada zangu, mmoja alimfahamu baada ya siku moja kuniona naye kwa mbali. Aliponiuliza nilijaribu kumficha lakini aliponibana nilimweleza ukweli. Basi ikawa kila siku nikikutana na mpenzi wangu lazima nimpelekee dada zawadi.

Ahadi yetu ilikuwa nikimaliza kidato cha nne tuoane, japokuwa mwanzo nilikuwa na ndoto za kufika chuo kikuu, lakini mazingira ya nyumbani yalinifanya nipoteze mwelekeo wa masomo na kuyabadili mawazo yangu yote kuhamishia kwa mpenzi wangu ambaye muda mwingi baada ya masomo nilikwenda kwake.

Hata matokeo ya kidato cha nne yalipotoka na kuonesha nimefeli vibaya sikushtuka kama wengine waliofikia hatua ya kutaka kujiua. Kwangu ilikuwa sawa kwa vile niliamini kabisa muda ule ulikuwa muafaka kwa mimi kuolewa na Beka.

Baada ya matokeo nilimfuata mwenzangu na kumweleza ule ndiyo ulikuwa muda muafaka wa yeye kuja kujitambulisha rasmi nyumbani.
Siku nilipomtambulisha hakuwa mgeni kwa dada, baada ya kuondoka mpenzi wangu, familia yangu ilitaka kujua anafanya

kazi gani. Niliwaeleza ni dereva wa teksi.
“Teksi yake au ameajiriwa?” mama aliniuliza.
“Ameajiriwa.”
“Sasa akifukuzwa kazi mtakula nini?”
“Mama mbona umekimbilia kufukuzwa kazi kuliko yeye kununua yake?’
“Atawahi! Mwanangu hawa dada zako wamekosa nini hapa nyumbani?”
“Mama wao hawakupenda kukaa nyumbani bali mapenzi ya Mungu.”
“Hata kama kazi ya Mungu, lakini toka warudi nyumbani wana tatizo gani?”
“Hawana matatizo, lakini wao ndiyo hawataki kuolewa tena.”
“Hawataki kuolewa kwa sababu wanaume wasio na uwezo ni mzigo kwa familia tu, kesho akifukuzwa kazi nikulishe mimi?”
“Mama ni kuniombea kwa Mungu nifanikiwe.”
“Kwa kazi kama hiyo nakuomba uachane na wazo hilo,” mama alinikata maini.
“Mama siwezi kuachana na wazo hilo kwa vile nitakayeolewa ni mimi.”
“Kama una uamuzi wako, sawa olewa kwa amri yako.”
“Mama nipo tayari kuishi maisha yoyote ndani ya ndoa, tutaishi hivi mpaka lini tunajazana nyumbani hata heshima hatuna.”
“Kwa hiyo umefanya vibaya kwenye mtihani ili uolewe?”
“Mama uliniambiaje?”
“Nilikuambia nini?”
“Mama si uliniambia huna hela za kunisomesha tena?”
“Ndiyo umefeli kiasi hicho?”


Je Vipi wasomaji mumeipenda hii hadithi? nataka mawazo yenu mukiipenda ıtaendelea hamukuipenda bora niishie hapo mnasemaje?Toeni Mawazo yenu........
Next Post Previous Post
Bukobawadau