Bukobawadau

TUMUENZI NYERERE BILA KUFANYA DHIHAKA


Kumuenzi mtu ni kumpa heshima ya kuendelea kukumbukwa kulingana na thamani ya mchango wake alioutoa kwa jamii aliyokuwa akiitumikia. Jamii yoyote huamua kumuenzi mtu kutokana na mema aliyoitendea. Ni nadra sana mtu kuenziwa kwa mabaya yake. Kwa vile kuenzi ni kutoa heshima hapanabudi utaratibu maalumu ufuatwe ili kujenga picha yenye kutoa maana inayoeleweka ambayo muhimu zaidi ni kuisimika heshima maridhawa kwa mlengwa.

Inabidi pawepo na utaratibu maalumu wa kumuenzi muhusika sanasana akiwa wa ngazi ya Kitaifa ili kuzuia watu wanaoweza kupotosha maana ya jambo hilo kwa kufanya mambo yanayoweza kuchafua jina la mtu maarufu katika jamii kwa kisingizio cha kumuenzi.

Hapa nchini kwetu jina la Julius Kambarage Nyerere ni jina kubwa ambalo, sina shaka, litaendelea kuwa kubwa kuliko majina yote ya Watanzania waliobaki kwa kipindi cha miongo mingi kama siyo karne nyingi zijazo. Nyerere ni kiogozi wetu, mwalimu wetu na Baba yetu, ambaye hata kabla hafariki dunia tulikubaliana, pasipo mtu yeyote kubisha, kumuenzi kama Baba wa Taifa. Hii ni heshima ya pekee tuliyoamua kumtunukia bila kulazimishwa na nguvu yoyote bali msukumo wa mapenzi yetu kwake, mapenzi yaliyomfanya kila Mtanzania amchukulie Nyerere kama mmojawapo wa wanafamilia yake. Kila Mtanzania alimuona Nyerere kama mwanafamilia wake.

Mapenzi ya Watanzania kwa Mwalimu Nyerere yalianza kujionyesha punde tu alipoamua kuacha kazi ya ualimu na kuingia kwenye siasa akiwa na lengo la kutia msukumo wa nchi yetu kupatiwa uhuru, Tanzania bara, wakati huo ikijulikana kama Tanganyika.

Ni wakati huo wananchi walipoanza kumuenzi Nyerere  kwa kuwapa watoto wao, hasa waliozaliwa kuanzia kipindi hicho, majina yaliyokuwa yanadhihirisha mapenzi yao kwa mwalimu. Watoto wengi walipewa majina ya Julius, wengine wakaitwa Kambarage na wengine kuitwa Nyerere. Ukiondoa jina la Julius ambalo ni jina la Kizungu linalotumika huku kwetu kama jina la kidini (la Kikristo), yaliyobaki yaani Kambarage na Nyerere ni ya kikabila, bilashaka ya Kizanaki, lakini hatahivyo wananchi waliyatumia wa makabila mbalimbali bila kujali asili yake na wala maana yake. Watanganyika na baadaye Watanzania walijali zaidi kwamba asili ya majina hayo ni mtu abaye tayari alikuwa mtu wao.

Pia wananchi walimjengea Nyerere uadhimu wa pekee wanaoendelea kuuhifadhi mpaka leo pamoja na ukweli kwamba Nyerere hatukonaye kimwili. Utasikia katika maeneo mbalimbali ya nchi, watu wanapotaka kusisitiza jambo, mfano, kitu fulani hakiwezi kufanyika labda kama angekuja Nyerere! Siku fulani nikamsikia mtu mmoja anapinga kwamba hawezi kupokea barua ya kuitwa Mahakamani akisema kwamba labda kama ingekuwa na sahihi ya Nyerere! Sio kwamba wanaosema hivyo hawajui kuwa alitoka Nyerere akaja Mwinyi  baadaye Mkapa na sasa tunaye Kikwete, ila hii inaonyesha imani iliyojengeka katika mioyo ya wananchi kwamba pamoja na Nyerere kuwa Rais kama hawa waliomfuatia bado ukubwa wa jina lake ni wa pekee.

Isitoshe kuna vitu vingi ambavyo tayari vilishapewa majina ya Nyerere kama kumbukumbu yake. Kuna shule nyingi za sekondari na hata za msingi zinazoitwa Nyerere au Kambarage. Ukitembelea kila mji na kila jiji  hapa nchini ni lazima utakutana na mitaa inayoitwa ama  Nyerere au Kambarage au yote mawili. Huu ni ushahidi tosha kwamba Mwalimu tumemuenzi kiasi cha kuridhisha. Zaidi ya hapo tutajikuta tunamchafulia jina. Nitaeleza kwanini.

Kwa sasa suala la kumuenzi Nyerere limebaki kuwa suala la Kitaifa. Na linapaswa kuwa la Kitaifa kwelikweli kwa maana ya Taifa kusimamia pamoja na kudhibiti matumizi ya jina la Mwalimu Nyerere, huko ndiko tunakoweza kukutaja kama kumuenzi Nyerere. Tena Taifa lisiishie kufanya mabadiliko tu tunayoyaona yakifanyika katika kile kinachoitwa kumuenzi Nyerere, mabadiliko ambayo ni pamoja na kutaka kubadili karibu majina ya kila kitu na badala yake vitu hivyo kuviita majina ya Nyerere! Kumuenzi Nyerere ni zaidi ya matumizi ya jina lake.

Katika jiji la Dar es Salaam peke yake jina la Nyerere linaelekea kupoteza umuhimu wake kutokana na vitu chungu nzima kupewa jina la Nyerere. Ngoja nitaje baadhi. Iliyokuwa inaitwa barabara ya Pugu (Pugu road) ilibadilishwa jina na kuitwa barabara ya Nyerere (Nyerere road). Uwanja wa maonyesho ya Kimataifa ya biashara uliokuwa ukijulikana kwa wakazi wa Dar es Salaam kama uwanja wa Sabasaba umebadilishwa jina na kupewa jina la Nyerere. Iliyokuwa ikiitwa Nyumba ya sanaa sasa hivi ni kituo cha sanaa cha Mwalimu Nyerere! Uwanja wa Kimataifa wa ndege wa Dar es Salaam nao umebadilishwa jina na kupewa jina la Nyerere. Tena hii ni kwa upande ambao mabadiliko hayo yanatolewa maamuzi na serikali au kupitia kwenye asasi zake.

Bado kuna maamuzi ya kulitumia jina la Baba wa Taifa yanayotolewa na watu na asasi binafsi kama ulivyotolewa uamuzi wa kulipa jina la Nyerere lile jumba la sinema la Mwenge linalomilikiwa na mpenzi wa kutupa wa Mwalimu Nyerere Mzee Sabodo.

Mbali na hapa Dar es Salaam kuonekana jina la Nyerere limezagaa kila pahala, mikoani nako mambo yako vilevile. Mara utasikia maonyesho ya kilimo ya Nyerere kule Morogoro, bustani ya Nyerere kule Dodoma nakadhalika.

Nafikiri umefika wakati serikali ichukuwe uamuzi wa kudhibiti matumizi ya jina la Baba wa Taifa ili kulinda hadhi na thamani yake  ikiwa ni njia mojawapo kuu ya kumuenzi mzee wetu. Kuliachia jina la Nyerere likaendelea kutumika kihorera isichukuliwe kuwa ni njia ya kumuenzi tu vilevile inaweza ikawa njia ya kumfanyia dhihaka. Fikiria mtu anaamua kumuita ndama wake aliyezaliwa jina la Nyerere kwa kisingizio cha kulienzi jina hilo!

Sidhani kama utakuwa mwendelezo wa kulienzi jina la Baba wa Taifa kama kutatokea hata zile sehemu zinazotumika kunajisi maadili ya jamii nazo zikaanza kupewa majina ya Nyerere kwa madai ya kulienzi jina hilo. Hebu fikiria patakapojitokeza vitu kama Nyerere guest house, Kambarage lodging, Nyerere pub au J. K. Nyerere camp wakati tukielewa kwamba camp zilizo nyingi ni magenge ya kuvutia bangi na madawa ya kulevya.

Ningeshauri vitu vilivyopewa majina ya Nyerere vipunguzwe ili kuleta maana muafaka  ya matumizi ya jina hilo.

Matumizi horera ya jina la Nyerere si kitendo cha kulienzi jina hilo hata kidogo, kinyume chake, ni kwamba litaanza kushuka hadhi. Hii ni kwa sababu kitu kikiwa chekwa kikakosa uhadimu thamani yake inashuka na ubora wake unapotea. Kwahiyo kuzidi kuyatumia majina ya Baba wa Taifa kwa vitu mbalimbali bila ulazima wa msingi kunaweza kuonekana kama dhihaka badala ya heshima tunayolenga kumpa huyu mwasisi wa Taifa letu.

Kitu kingine ni kwamba matumizi haya tusipokuwa waangalifu, yanaweza yakaipotosha jamii ikajikuta inamuelewa Nyerere katika maana tofauti na ile inayokusudiwa na hao watumiaji wa jina hilo. Kutokana na nchi yetu kukosa utamaduni wa kuvitunza vitu vyake katika hali ya unadhifu upo uwezekano mkubwa wa vitu vilivyopewa majina ya Nyerere kuvikuta katika hali ya shaghalabaghala. Inaweza ikatokea barabara zote zinaitwa Nyerere zikawa mbovu kutokana na kutofanyiwa ukarabati. Mathalani, mtu anatoka Mwanza anaacha barabara ya Nyerere ina mashimo, anafika Dar anakuta barabara ya Nyerere iko vilevile kama ya Mwanza,  picha inayojengeka kichwani ni nini hasa kwa watoto? Vivohivyo kwa vitu vingine vilivyopewa majina ya Nyerere kila mahali,  picha inayojengeka ni kwamba vitu vinapokuwa vibovu ndipo vinapoitwa Nyerere!

Au yanaweza yakajengeka mazoea kwamba kitu kikiwa na urefu fulani kinaitwa Nyerere, au kikiwa na ukubwa fulani kinaitwa Nyerere! Yakaja kujitokeza yaleyale ya jamaa zetu fulani waliokuwa wameyazoea maghorofa ya hospitali ya Bugando ya jijini Mwanza na kujijengea imani kwamba kila mji waendako na kukuta maghorofa basi ni Mabugando! Sasa hii itakuwa kumuenzi Nyerere au kumdhihaki?

Kwa upande mwingine Kanisa nalo limeanza mchakato wa kumuenzi Nyerere kwa kutaka kumtangaza kwamba ni mwenye heri. Ingawa sielewi hii ina maana gani, sababu mimi naamini kwamba maamuzi ya Mwenyezi Mungu hayana ushawishi kutoka kwa wanadamu sababu Mungu si mla rushwa, bado hii nayo itaendelea kulitangaza jina la Nyerere tena kwa njia ambayo nadhani ni bora zaidi kuliko hata ile inayotumiwa na serikali. Tutaanza kuyaona makanisa yanayoitwa Mwenye heri Nyerere na vitu vingine vinavyomilikiwa na kanisa hilo.

Mambo yanayonivutia kwa upande wa uamuzi wa Kanisa wa kumuenzi Nyerere ni mawili. Jambo la kwanza ni kwamba kanisa linapoamua kumuenzi mtu linaangalia zaidi matendo yake wakati wa uhai wake kuliko umaarufu aliokuwa nao. Kwahiyo katika mchakato wa Kanisa wa kumtangaza Nyerere mwenye heri waamini wote wa Kanisa hilo wanatakiwa kuyazingatia na kumuomba Mwenyezi Mungu awawezeshe kuyatekeleza kwa vitendo yale yote yaliyokuwa yakielekezwa na Mwalimu Nyerere. Waamini hao watamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie ujasiri wa kuvichukia vitu alivyokuwa akivikataza Nyerere. Mfano,  ujasiri wa kuiona rushwa kwamba ni adui wa haki kama alivyo eleza Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake.

Vilevile kuyakataa yote aliyokuwa akiyakataza Mwalimu,kama vile ubaguzi katika misingi ya kabila na rangi. Wizi wa mali ya umma, ufisadi wa kujitajirisha kwa mtindo wa kujirundikia mali, uonevu na ukandamizaji kwa lengo la kuhodhi na kuyang’ang’ania madaraka nakadhalika. Kwa misingi hii Kanisa litatuonyesha njia iliyo sahii ya kumuenzi Baba wa Taifa hata kama  kufanya hivyo hakutupi uhakika wa moja kwa moja kwamba hicho kinaweza kuwa kishawishi cha kumshinikiza Mwenyezi Mungu kutengua maamuzi yake. Ila kwa vile tunaamini na kuabudu kwamba Mungu ni mwema hatuna haja ya kutilia shaka mapendekezo yetu kwake.

Uzuri wa pili ninaouona katika mchakato wa Kanisa wa kumuenzi Nyerere ni huu: Baba wa Taifa , mpaka mauti yalipomfika, alikuwa akilalamikia umasikini unaozitesa  nchi zinazoitwa eti  za dunia ya tatu, nchi yake Tanzania ikiwa miongoni mwa zile zilizo taabani kabisa. Litakuwa jambo la faraja kwake, kama upo uwezekano wa yeye kutokea kule aliko kuyaona yanayotendeka huku nyuma, akiona jina lake linachangia kuinua uchumi wa nchi yake na watu wake kupata ahueni.

Tukiweka imani pembeni, kitendo cha kumtangaza mtu kuwa ni mwenye heri na baadaye mtakatifu kinalenga zaidi katika uchumi wa sehemu husika. Sababu hicho ni kivutio cha utalii wa aina yake. Sina takwimu sahihi kutoka Maliasili na Utalii ili kujua  tunapata watalii wangapi kwa mwaka wanaotembelea nchi yetu kwa ajili ya vivutio mbalimbali, ila sidhani kama wanafika milioni moja. Sasa kwa kivutio kimoja cha Mwenye heri Julius Kambarage Nyerere, sintashangaa tukipata watalii zaidi ya milioni nne kwa mwaka! Kwa hilo nalipongeza Kanisa katoliki kwa upeo wao wa kuona mbali.

Tofauti na Kanisa, serikali inasisitiza kumuenzi Nyerere lakini kwa njia ambazo zinaonekana wazi kwamba ni dhihaka, kebei, kejeli na uzandiki. Huwezi kusema kwamba unamuenzi Nyerere kwa kutenda mambo ambayo yalikuwa haramu kwake na mpaka anakufa alikuwa akiyalaani. Huko si kumuenzi ila ni kumdhihaki. Tendo la kupachika jina lake  kwa karibu kila kitu lakini yakipuuzwa yale yote aliyokuwa akiyahimiza yafanyike ni kumkejeli si kumuenzi.

Inawezekana jina la Nyerere likawa bado linahitajika na utawala wa sasa ili liusaidie kujiimarisha madarakani kwahiyo ikawa sababu ya utawala kuonekana unalienzi jina hilo, huu ni uzandiki!

Mpaka katika hotuba zake za mwishomwisho Mwalimu alikuwa anasisitiza jinsi ilivyo vigumu kwa mwanadamu kutumikia mabwana wawili, yaani kutumikia mali na kumtumikia Mungu. Viongozi wa watu ni watumishi wa Mungu.  Maana yake ilikuwa kwamba wenye mali, matajiri,  ambao zamani aliwaita mabwenyenye,  hawakufaa kuwa viongozi wa wananchi. Lakini sasa hali ikoje? Asiyekuwa na mali ndiye hafai kuwa kiongozi! Je, huku ndiko kumuenzi Nyerere?

Mwalimu alikuwa na msimamo kwamba raslimali asili za nchi hii si kwamba ni za kizazi kilichopo kwa sasa peke yake, bali hata vizazi vijavyo karne nyingi mbele. Ndiyo maana alikuwa anasisitiza kwamba zile raslimali asili ambazo tulikuwa hatujaweza kuzishughulikia sisi wenyewe hatuwa na haja ya kufanya haraka sababu alikuwa akiamini kwamba utafika wakati watakaokuwepo kwa wakati huo wakawa wameishaweza kuzishughulikia wangefanya hivyo sababu nao ni haki yao.

Lakini viongozi wetu wanasema hapana, hii ni haki(yao?)yetu, hata kama hatuna uwezo wa kuishughulikia bora tukawatafute wenye uwezo huo wakaishughulikie na kuzoa, potelea mbali chochote watakachoamua kutupatia si haba kuliko kuiacha eti kwa ajili ya vizazi vijavyo! Vizazi vijavyo vitashughulikia mahandaki na milima bandia inayotengenezwa na hao wataalamu wa kuchimba na kuzoa mali asili za wenzao. Je, humu kuna dalili zozote za kumuenzi Nyerere?

Mwalimu amekufa akiwa bado ni muumini hai wa Azimio la Arusha. Na si ajabu wakati anakata roho alikuwa na vitabu viwili mfukoni mwake, kama alivyokuwa akitueleza kila mara, kitabu cha Biblia takatifu na kile cha Azimio la Arusha. Azimio ambalo viongozi wa awamu ya pili walikaa kule Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1990 na kulipangua katika Azimio la kimyakimya lililokuja kujulikana kama Azimio la Zanzibar. Wengi wa walioshiriki katika Azimio la Zanzibar bado tunao hadi leo na wengi wamo katika Serikali ya awamu ya nne wanaendelea kula kuku kwa mrija huku wakiwa mstari wa mbele wakiongoza wimbo wa kumuenzi Nyerere!

Nyerere alikuwa anakataza mtumishi wa umma kutumia fursa hiyo kujinufaisha na mali ya umma au kuiba mali ya umma. Kwa msimamo huo hata nyumba yake ya Msasani aliyoijenga kwa mkopo wa Benki alikuwa ameamua kuisalimisha serikalini  baada ya yeye mwenyewe kukiri kuwa alishindwa kulipa mkopo wa benki. Leo hii viongozi walioamua kujibinafsishia nyumba na maeneo ya serikali wanaimba wimbo wa kumuenzi Nyerere! Hii kama siyo kejeli ni nini?

Tumemuona kiongozi mmoja aliyetumia ndege ya serikali (Jeshi) kufanya ziara binafsi nyumbani kwao, alipoulizwa ilikuwaje naye akauliza, mlitaka niende kwa baiskeli? Naye huyu anadai anafanya hivyo kwa kumuenzi Nyerere!

PRUDENCE KARUGENDO
Next Post Previous Post
Bukobawadau