UJIO WA RAIS OBAMA NCHINI TANZANIA
Imeelezwa kuwa ujio wa Rais Barack Obama wa Marekani nchini, ni
fursa nyingine kwa Tanzania kukuza uchumi na kuimarisha uwekezaji.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili Profesa Ibrahim
Lipumba ambaye ni mchumi kitaaluma, amesema kuwa ujio wa Rais Obama
unaweza kuleta neema hasa kama atakuwa ameambatana na wataalamu wa
masuala ya maendeleo.
Hii itakuwa ziara ya pili ya Rais Obama katika Bara la Afrika.
Hii itakuwa ziara ya pili ya Rais Obama katika Bara la Afrika.
Ziara yake ya kwanza aliifanya wakati wa awamu
yake ya kwanza madarakani, wakati ziara ya safari hii ni kipindi chake
cha lala salama.
Rais Obama alianza rasmi awamu yake ya kwanza kama
Rais wa Taifa kubwa, Januari 20, 2009, wakati ng’we yake ya mwisho
ilianza Januari 21, 2013.
Rais Obama anatarajiwa kufanya ziara hiyo mwishoni
mwa Juni mwaka huu, ambapo Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi za mwanzo
za Afrika Mashariki kutembelewa na kiongozi huyo.
Ziara ya Rais Obama inafanyika baada ya ziara ya
Rais Xi Jiping wa China aliyeitembelea Tanzania Machi 28, mwaka huu,
ambapo Tanzania ilikuwa nchi yake ya kwanza kuitembelea kwa Afrika tangu
achaguliwe kuwa rais, Machi 14, 2013.
Akizungumzia ziara hiyo tarajiwa, Mwenyekiti wa
Taifa wa Chama cha Wananchi (Cuf), Profesa Ibrahim Lipumba ambaye ni
mchumi, alisema amani, utulivu na uimara wa mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi kwa kulinganisha na nchi nyingine za jirani, vimechangia kuwapo
kwa ziara hiyo.
Profesa Lipumba alisema pia ugunduzi wa rasilimali
za asili kama vile gesi, mafuta na madini ya urani ni sababu nyingine
iliyomfanya Rais huyo kuja nchini.
Hivyo aliwashauri viongozi wa Serikali kujipanga kwa ajili ya kufungua mlango huo mwingine wa uchumi na uwekezaji.
Alisema pamoja na hali hiyo pia kuna mambo ambayo
yanaweza kuchafua taswira ya nchi kama vile ubovu wa miundombinu ya
barabara, msongamano wa magari barabarani na msongamano wa meli
bandarini wakati zikisubiri kushusha mizigo.
Jumatano ya wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa
Marekani, John Kerry alitangaza mbele ya wajumbe wa Kamati ya
Ushirikiano kati ya Marekani na Afrika, kwamba Rais Obama hivi karibuni
atafanya ziara Afrika.
Ingawa Kerry hakutoa maelezo zaidi ya nchi gani za
Afrika ambazo Rais Obama atazitembelea, lakini baadhi ya vyombo vya
habari vya Nigeria vilieleza kiongozi huyo atafanya ziara Tanzania,
Rwanda na Nigeria.