Bukobawadau

UTITIRI WA KODI WAKWAZA WAVUVI KAGERA

TANZANIA inakabiliwa na hatari ya kutofaidika na soko la pamoja la Afrika Mashariki katika sekta ya uvuvi kama haitarekebisha viwango vya ushuru na tozo kwa wavuvi ziende sawa na za nchi jirani.

Pamoja na kushuka kwa bei ya samaki aina ya sangara kwa karibu nusu ya bei kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo mtikisiko wa uchumi katika nchi za Ulaya, aina nyingi za ushuru anaotozwa mvuvi zinachangia kuvushwa kwa samaki wengi kwenda kuuzwa nchini Uganda kwa njia za kinyemela.

Uchunguzi wetu kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa umebaini kuwa pamoja na kutafuta bei nzuri ya samaki inayotolewa na viwanda vya kuchakata samaki nchini Uganda, sababu nyingine kubwa ni kukimbia mlologo wa kodi nyingi anazopaswa kulipa mvuvi kwa mamlaka mbalimbali nchini.

Pamoja na kutakiwa kulipa kodi ya mapato kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), mvuvi anatakiwa pia kulipa leseni ya mtumbwi ambayo inatozwa kwa dola 50 (Tsh.

80,000/-) za Kimarekani kwa mwaka, usajili wa mtumbwi ambao pia unalipiwa dola 10 (Tsh.16,000) kwa mtumbwi wenye urefu wa mpaka mita 11, na dola 50 (shilingi 80,000/-) kwa mtumbwi wenye urefu wa mita kati ya 11- 15, kulipia leseni ya mvuvi shilingi 15,000 kwa mwaka kwa mvuvi mmoja na kila mtumbwi unatakiwa kuwa na wavuvi watatu.

Sanjari na tozo hizi mvuvi huyo huyo pia anatozwa ushuru wa samaki ambapo analipa asilimia 5 ya bei aliyonunulia kwa halmashauri, ushuru wa maegesho kwa mitumbwi midogo shilingi 500 kila siku, mitumbwi mikubwa shilingi 1000 kwa siku.

Tozo nyingine ni ushuru wa viwanda wa asilimia 5 ya bei ya kununulia, ushuru wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) ambao unatozwa kwa dola 34 (Tsh.54,400) kwa mtumbwi wa mpaka mita 11.

Pamoja na tozo hizo mwaka huu wa fedha umeongeza aina nyingine ya tozo kwa wavuvi, wanatakiwa kulipia ushuru wa usafirishaji wa shilingi 50,000 kwa kila safari ya mtumbwi au gari linapopeleka samaki kiwandani bila kujali uzito wa samaki iliyobeba.

Hali hii, kwa mujibu wa katibu msaidizi wa Chama cha Wavuvi (TAFU) Daudi Kasiri, itasababisha ama wavuvi wengi kufilisika au kuwashawishi kukwepa kodi na kuanza kufanya biashara za magendo kupeleka samaki kule kuliko na soko zuri, wanakoweza kupata faida.

Kasiri anasema wavuvi, kama wafanyabishara wengine, wanawekeza pesa nyingi katika biashara hiyo ambayo hata hivyo ni kama haipewi umuhimu unaostahili na serikali, kwa kuwa pamoja na umuhimu wake katika kutoa ajira na kuingiza pato la nje bado wavuvi ni kama wametelekezwa.

“Injini ya mtumbwi ya horse power 9.9 na 15 ni shilingi milioni 4, kuuchonga mtumbwi wa mita 11 sasa hivi ni shilingi milioni 3 na kila mtumbwi unahitaji nyavu zaidi ya 80 na kila wavu mmoja huuzwa shilingi 60,000.

“ Nyavu hizi unaweza ukatumia hata kwa mwezi tu zikaibiwa au hata kukatika, wakati mwingine tunatumia nyavu hata kwa siku mbili tu,” anasema Kasiri.

Anasema mazingira haya yanakuwa magumu sana katika kufanya biashara kwa Watanzania ukilinganisha na jirani zao ambao wakati mwingine wanatumia udhaifu ulioko nchini kurekebisha biashara yao na ndiyo maana wanavutia wavuvi kwenda kuuza samaki kwao.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa wavuvi wengi katika visiwa ya Nyaburo, Kinagi, Lushanja, Chamkuvi, Goziba na Kerebe vilivyoko mkoani Kagera wamekuwa wakisafiriha samaki nyakati za usiku mpaka katika kisiwa cha Kasensero nchini Uganda ambako huwauza kwa bei ya juu viwandani tofauti na wanavyouza kwa viwanda vya nchini.

“Sasa hivi natoka kiwandani, leo bei ya samaki katika viwanda ni shilingi 2,200 kwa samaki wenye uzito wa kila moja mpaka nne na shilingi 2,800 kwa samaki wa kuanzia kilo 5, wakati jana nimetoka kupata oda ya kiwanda kimoja nchini Uganda ambako wananihakikishia bei ya shilingi 5,000 za Tanzania kwa kilo,” anasema wakala mmoja wa samaki ambaye anakiri kuwa amekuwa anapeleka samaki katika kisiwa cha Kasensero.

Afisa mmoja wa uvuvi kutoka idara ya kudhibiti ubora wa samaki mkoani Kagera amekiri kuwa wimbi la usafirishaji wa samaki kupeleka nchini Uganda ni kubwa kiasi kwamba wastani wa tani 25 – 30 husafirishwa kwenda nchini Uganda kwa wiki.

“Katika kipindi hiki cha mgogoro wa bei ya samaki hapa, samaki wanaovushwa kwenda Uganda ni wengi sana kama nilivyokwambia, lakini tatizo letu kubwa ni uwezo mdogo wa kudhibiti hali hii kwa kuwa vifaa vya doria ni vichache na duni,” anasema.

Katika mkutano wa sekta ya uvuvi uliofanyika Julai 4 mwaka huu Jijini Mwanza, ambao pia ulihusisha kamati ya kudumu ya Bunge ya Mifugo, Kilimo, Maji na Uvuvi, Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Mathayo David aliunda kamati maalumu kwenda kuona hali ya biashara hiyo ilivyo katika nchi jirani za Kenya na Uganda na kuishauri serikali namna nzuri ya kusimamia sekta hiyo.

Kamati hiyo iliyoongozwa na Emmanuel Mondoka, Afisa kutoka kitengo cha kudhibiti ubora wa samaki, akiiwakilisha serikali, iliundwa na wajumbe kutoka serikalini, viwanda vya samaki na wavuvi ilikuwa na kazi ya kuangalia bei za samaki katika mialo na viwanda vya nchi hizo.

Kwa mujibu wa ripoti ya kamati hiyo bei ya samaki aina ya sangara katika kipindi cha Julai katika mialo ya Tanzania ya Sota (Rorya), Marehe na Igabilo (Kagera) ilikuwa kati ya shilingi 2,000 hadi 2,800 kwa kilo wakati bei ya viwandani ilikuwa ni kati ya shilingi 3,000 hadi shilingi 3,500.

Kwa upande wa Kenya bei ya kilo moja ya sangara katika mialo ya Nyagw’ina (Muhuru Bay) na Dunga (Kisumu) ilikuwa kati ya shilingi za Kenya 140 (shilini za Tanzania 2,660) na shilingi za Kenya 160 (za Tanzania 3,040) na viwandani ilikuwa ni kati ya shilingi za Kenya 200 (Tanzania 3,800/-) na shilingi 250 (Tanzania 4750).

Nchini Uganda kamati hiyo ilitembelea mialo ya Masese (Jinja) na Kigungu (Entebbe) ambako bei katika mialo kwa kilo ilikuwa ni shilingi za Uganda 5,000 (Tanzania 3,571) huku bei ya kuuza samaki viwandani kwa kilo ikiwa kati ya shilingi za Uganda 6,000 (Tanzania 4286) hadi shilingi za Uganda 7,000/- (Tanzania 5,000).

Kwa mujibu wa ofisi ya Uvuvi ya Wilaya ya Migori nchini Kenya wavuvi hutozwa leseni za mitumbwi midogo ya shilingi za Kenya 200 (Tanzania 3,800) kwa mwaka, leseni ya usafirishaji shilingi za Kenya 1000 (Tanzania 19,000) na leseni ya kuchakata samaki shilingi 1,000 za Kenya.
Next Post Previous Post
Bukobawadau