Waziri akiri kuhusu mbolea feki nchini
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima
Dodoma. Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, imekiri kuwa
inakabiliwa na changamoto ya kuwapo kwa mbolea isiyokuwa na viwango
vinavyokubalika na inayoathiri uzalishaji wa mazao.
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Naibu Waziri
wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, alipokuwa akijibu swali la
Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM).
Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu
tatizo la ubora wa mbolea, linalowakabili wakulima katika kila msimu wa
kilimo.
Naibu Waziri alisema Serikali kwa kutambua hilo,
imeweka udihibiti wa mbolea isiyokuwa na viwango kwa kupitia sheria ya
mbolea ya mwaka 2009, kifungu cha 7 (1).
“Pamoja na hayo, lakini pia Serikali imeunda
Mamlaka ya Usimamizi wa Mbolea ambayo kazi yake ni kuthibitisha ubora wa
mbolea viwandani,” alisema Malima.
Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo katika
ngazi ya halmashauri na wakulima, Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa
wakaguzi wa mbolea na kwamba hadi Mei mwaka jana kulikuwa na wakaguzi 44
kutoka katika halmashauri mbalimbali.
Kwa upande mwingine kiongozi huyo alisema tayari
wizara imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia
wananchi kila ifikapo Agosti mosi.