Wenye divisheni ziro 30,000 wapeta
Dar es Salaam. Wanafunzi 30,063 waliopata daraja sifuri katika
matokeo yaliyopita, wameula baada ya kupandishwa hadi daraja la nne
kutokana na ukokotoaji upya wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
yaliyofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) na kutangazwa jana.
Marekebisho hayo yalifanyika baada ya kufutwa kwa matokeo ya awali yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu.
Kufutwa kwa matokeo hayo, ilikuwa ni utekelezaji
wa sehemu ya mapendekezo ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, baada ya wanafunzi 240,909 kupata daraja sifuri kwenye matokeo
yaliyotangazwa mara ya kwanza.
Akitangaza matokeo hayo jana, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema sasa watakaokuwa na
sifuri ni 210,846 sawa na asilimia 56.92 wakati wavulana wakiwa ni
104,259 na wasichana 106,587.
Hiyo ina maana kuwa sasa ufaulu umepanda na kuwa asilimia 43.08 badala ya ule wa kwanza ambao ulikuwa asilimia 34.5.
Dk Kawambwa alisema kutokana na ukokotoaji mpya wa
matokeo ya sasa, idadi ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo kwa daraja
la kwanza mpaka la nne imeongezeka na kufikia wanafunzi 159,747 kutoka
126,847.
Wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 3,242
wavulana wakiwa ni 2,179 na wasichana 1,063 ikiwa ni asilimia 0.88 ya
matokeo yote, daraja la pili ni 10,355 sawa na asilimia 2.8 wavulana
wakiwa 7,267 na wasichana 3,088.
Waliopata daraja la tatu ni 21,752 sawa na
asilimia 5.87 wavulana wakiwa 14,979 na wasichana 6,773, daraja la nne
ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 .
Tofauti na matokeo yaliyofutwa, ambayo watahiniwa
waliopata daraja la kwanza walikuwa ni 1,641, wavulana wakiwa 1,073 na
wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na
wasichana 1997.
Waliopata daraja la tatu walikuwa 15,426, wavulana
10,813 na wasichana 4,613, waliopata daraja la nne 103,327, wavulana
64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903,
wavulana 120,664 na wasichana 120,239.
Dk Kawambwa alieleza watahiniwa waliosajiliwa
kufanya mtihani huo walikuwa ni 480,029 na waliofanya ni 458,139 sawa na
asilimia 95.44.
Alisema kuwa watahiniwa wa shule waliosajiliwa
kufanya mtihani huo walikuwa ni 411,225 na waliofanya ni 397,138 sawa na
asilimia 96.57 huku wa kujitegemea wakiwa ni 68,804 na waliofanya ni
61,001.