Bukobawadau

WILAYANI KARAGWE ARDHI YA NYAKASIMBI YARUDISHWA MIKONONI MWA WANAKIJIJI.

 Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bi Darry Rwegasira.
 Tawira  maeneo mbalimbali Wilayani Karagwe.

 Ofisi ya chama cha Mapinduzi Wilayani Karagwe.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bi.Darry Rwegasira ametoa tamko rasmi kuhusu nani mmiliki halali wa ardhi katika mgogoro uliodumu kwa zaidi ya mwaka mmoja kati ya wanakijiji cha Nyakasimbi Wilayani Karagwe pamoja na mwekezaji anayedaiwa kuwa mhamiaji haramu kutoka nje ya Tanzania.
Bi.Rwegasira alitoa tamko kuwa ardhi ile ni mali ya wanakijiji cha Nyakasimbi kata ya Nyakasimbi kupitia mkutano wa hadhara wa wananchi kijijini hapo Mei. 14. 2013 baada ya tume aliyoiunda mapema mwaka jana kuchunguza swala hilo, kukamilisha kazi yake ambapo amesema kuwa, pamoja na mambo mengine yaliyobainiwa na tume yake ugawaji wa ardhi hiyo kwa mwekezaji huyo ulikiuka taratibu za ugawaji ardhi kisheria.
Aidha mkuu huyo wa Wilaya aliuagiza uongozi wa Kijiji hicho kupitia upya taratibu za kisheria kuhusu matumizi bora ya Ardhi na kugawa upya eneo hilo kwa wanakijiji watakaoomba ardhi wakizingatia maelekezo ya sheria ili kuepuka migogoro mingine kama ile ambayo imesababisha hali ya kutoelewana baina ya uongozi wa kijiji pamoja na wanakijiji.
Hata hivyo Bi.Rwegasira ameongeza kuwa watendaji wote waliohusika kugawa holela ardhi hiyo bila kufuata taratibu,watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa hatua hiyo inafuatia hatua kali ambazo zimeshachukuliwa dhidi ya viongozi waliokuwa wakidaiwa kuwabeba wale ambao wanadaiwa kuiteka ardhi hiyo kwa minajiri ya ufugaji kinyume cha sheria.
Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dk Emmanuel Nchimbi alimfukuza kazi Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Matagi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kagera akituhumiwa kuwapiga na kuwabambikizia kesi zisizo na dhamana wananchi wa kijiji cha Nyakasimbi ambao walikuwa wakidai kupokonywa ardhi yao na wafugaji wanaodaiwa kutokuwa raia wa Tanzania.
Akielezea uamuzi huo wa kumfukuza kazi ofisa huyo,Waziri nchimbi alisema, “Mwaka jana kulikuwa na mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Nyakasimbi huko Kagera kati ya wanakijiji na mmiliki mmoja wa shamba, wananchi waliona kuwa mmiliki wa shamba hilo ana eneo kubwa hivyo walikubaliana katika mkutano wa kijiji kuingia kwenye shamba hilo kwa nguvu,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza:
“Waliingia na kuanza kuswaga ng’ombe kuelekea kwa Mkuu wa Wilaya, walikamatwa watu 12 lakini wawili walifanikiwa kutoroka na walisafiri hadi Dodoma kumwona mbunge wao, ambaye aliomba kuonana na mimi.”
Dk Nchimbi alisema licha ya kukubali kuonana nao, ilishindikana baada ya watu hao kukamatwa wakidaiwa kuwa ni majambazi ambao walikuwa wakitafutwa huko Karagwe.
“Nilimpigia simu Kamanda wa Polisi Kagera nikitaka kuonana na hao majambazi katika Hoteli ya Dodoma na waliletwa na niliwasikiliza na kugundua kuna tatizo la wao kubambikiziwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha ambayo huwa haina dhamana,” alisema.
Alisema aliunda timu ambayo aliiongoza akiwa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA), Aggrey Mwanri na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye na kusimamia uchunguzi na Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali iligundua hakuna mashtaka kama hayo na ndiyo maana Matagi anafukuzwa kazi na kushtakiwa kijeshi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau