Wizara Maliasili kuajiri askari wanyamapori 400
Dodoma. Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kuajiri askari 400 wa Wanyamapori nchini katika kipindi cha Julai mwaka huu.
Ahadi hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa
Maliasili na Utalii Balozi Khamisi Kagasheki ambaye aliahidi pia
kupeleka bungeni Sheria ya kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori katika Bunge
la Novemba mwaka huu.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza
la Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema) ambaye alihoji mpango wa
Serikali kuchelewesha kutungwa kwa mamlaka hiyo kuwa ni ukiukwaji na
dharau kwa Bunge ambalo lilipendekeza hivyo.
“Ndiyo maana tunalalamikia sheria hiyo kwani kila
wakati tembo wanauawa na hasa wale ambao wako nje ya hifadhi, kuna
kigugumizi gani cha kutoleta sheria hiyo mapema bungeni,” alihoji Zitto.
John Lwanji (Manyoni Magharibi-CCM) alihoji mpango
wa kuanzisha Mamlaka itakayosimamia hifadhi za mapori ya akiba ya
wanyamapori badala ya idara ya wanyamapori.
Naibu Waziri wa Malisili na Utalii Lazaro Nyalandu
alisema kuwa ahadi ya Serikali ya kuanzisha Mamlaka ya Wanyamapori iko
palepale ambapo hadi sasa rasimu za kwanza za sheria hiyo
zimekwishakamilika.
Nyalandu alisema kuwa katika mkutano wa nane wa
Bunge, Serikali iliahidi kuwa ifikapo Desemba 2012, mchakato wa
uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori utakuwa umekamilika.
“Hata hivyo, baada ya kamati ya uanzishwaji wa
Mamlaka kupata maoni ya wadau, iligundua uwepo wa mambo muhimu
yaliyohitaji kujadiliwa kwa kina,” alisema Nyalandu.
Alizitaja sababu zilizochelewesha utaratibu huo ni
kupanuka kwa wigo wa wadau kwani walikusanya maoni kutoka kwa watu
wengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kikamilifu