Bukobawadau

Kuna umuhimu wa kukumbuka watumwa


Katika kitabu cha Dk Livingstone wakati anakwenda Nyasaland (Malawi) akitokea Mikindani, mkoani Mtwara amezungumzia watumwa.
Alisema aliwaona watumwa wakichapwa baada ya kushindwa kazi na wengine walioshindwa kutembea kabisa walifungwa kwenye miti kwa kamba au minyororo ili wasitoroke na kurudi kwao.
Lengo wafe. Pia aliona maiti za watumwa walioshindwa kutembea kutokana na maradhi, njaa na uchovu. Watu hao waliuawa kwa magobore ili wasichukuliwe na mabwana watumwa wengine.
Haya ni sehemu tu ya mateso ya watumwa na athari zake ambazo haijawahi kuelezewa kwa undani, hasa katika pande hizi za Afrika Mashariki. Ingawa Waarabu wanaonekana ni vinara wa biashara hii, lakini mataifa mengi yalihusika na kubeba watumwa kutoka Afrika Mashariki wakiwamo Wareno, Wamisri, Waajemi, Wahindi na Waingereza waliokuja kupinga biashara ya utumwa.
Wakati huo, utumwa ulikuwa ni biashara muhimu sana katika Bara la Afrika. Biashara hiyo imeathiri kujitambua kiuchumi na hata uhusiano wetu kati yetu na wageni waliotutembelea na wale waliotufanya Watumwa.
Nimeandika makala hii kwa ushawishi wa msomaji mmoja wa makala iliyopita kuhusu John Springfield, Mzanzibari wa Kwanza kupinga biashara ya utumwa na hatimaye kuhamia Uingereza. Msomaji huyu anaona umuhimu wa kuwa na siku ya kuadhimisha utumwa Afrika Mashariki, hasa Tanganyika, Malawi, Congo na Burundi ambako watu wameathirika zaidi. Maadhimisho hayo yangekuwa na umuhimu mkubwa.
Kwanza ni kwa ajili ya kuweka kumbukumbu kwa usahihi zaidi kuhusu idadi kamili ya watumwa, na makabila yaliyoathirika zaidi. Pia kujua wahusika wa ndani na wa nje na kuelezea athari yake kwa maendeleo.
Mpango huo utasaidia kujua pia mtawanyiko wa watu wetu baada ya biashara ya utumwa kufanyika katika Pwani ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika na kwengineko. Siku hii ya kukumbuka utumwa inaweza kutusaidia kujua walifikaje huko na mengine zaidi.
tavicom.tavici@yahoo.com, 0766959349
Next Post Previous Post
Bukobawadau