Uhamiaji wazidisha masharti ya kutoa ‘pasipoti’ kwa vijana
Dar es Salaam. Idara ya Uhamiaji imesema kwa sasa inapata katika kipindi kigumu katika kutoa hati za kusafiria na kwamba imeamua kuwanyima kabisa baadhi ya watu na hasa vijana wanaotaka kwenda nje ya nchi.
Imesema hatua hiyo inatokana na vijana wengi kujihusisha na shughuli zisizokuwa halali, zikiwamo biashara ya dawa za kulevya wanapofika katika nchi za kigeni.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Msemaji Mkuu wa Idara hiyo, Tatu Burhani, ambaye alisema matukio ya watu kukamatwa na kutumikia vifungo kwa sababu ya kujihuisisha na shughuli hizo, yameifanya idara kuwa makini zaidi katika utoaji wa hati za kusafiria.
“Kwa sasa tutakuwa makini sana katika utoaji wa pasipoti hasa kwa vijana kwa kuwa tumegundua kuwa vijana wengi wakienda nje ya nchi hawana shughuli za kufanya na badala yake, wanaanza kufanya kazi zilizo kinyume na sheria za nchi husika,”alisema Burhani.
Alisema idara kwa sasa imeanza kuwawekea masharti vijana ikiwa ni pamoja na kuwataka warudi mapema nchini mara wanapomaliza shuguli zao katika nchi za kigeni.
Alisema watu wengi wanapata matatizo kutokana na kuamua kuishi kwenye nchi za watu wakati muda wao ukiwa umemalizika.
Alisema kitendo cha Watanzania kushikiliwa katika nchi za nje kinaliingizia taifa hasara kwa sababu wanapomaliza vifungo vyao wanapaswa kurudishwa nchini kwa gharama za Serikali.
Alisema katika magereza ya nchi mbalimbali yakiwamo mawili ya Pakistani yana jumla ya wafungwa 35 wa Kitanzania wengi wao wakishikiliwa kwa kosa la kuishi kinyume na sheria na biashara ya dawa za kulevya.
Juzi idara hiyo ilitoa taarifa ikiwa imeambatanisha na picha za raia 35 wa Tanzania wanaoshikiliwa katika magereza mawili nchini Pakistan.
Taarifa hiyo iliwataka ndugu, jamaa na marafiki wa raia hao kufika katika ofisi za idara hiyo ili kuapata taratibu za kuwarudisha nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo raia hao wameshikiliwa katika magereza ya Lahore na Rawlpindi nchini Pakistan.
Hata hivyo haikuelezwa wanakabiliwa na tuhuma gani.