Viongozi wetu chungeni ndimi, kauli zenu
Tanzania ambayo kwa muda mrefu imejinadi kuwa ni kisiwa cha amani, utulivu na mshikamano, inapitia katika kipindi kigumu mno pengine kuliko kingine chochote katika historia yake tangu ipate uhuru mwaka 1961.
Ni katika kipindi hiki cha mpito ambacho nchi yetu imeshuhudia kuzuka kwa matukio mengi yakiwamo yale yanayoashiria uvunjifu wa amani, vurugu za hapa na pale na harakati nyingine nyingi zilizojitokeza katika maeneo mbalimbali.
Tumeshuhudia kwa mfano, matukio ya Mtwara ambayo yamesababisha uharibifu mkubwa kwa mali na maisha ya watu na hivi sasa Arusha ambako milipuko ya bomu imetumiwa kusababisha umwagikaji wa damu ya watu wasio na hatia.
Machafuko kama hayo pia yamewahi kutokea mkoani Iringa zaidi ya mara moja na pia katika Mkoa wa Morogoro na kote huko damu ilimwagika. Wakati hayo yakitokea, kumezuka mtindo wa kurushiana makombora ya lawama kunakofanywa na wanasiasa au viongozi wetu wakiwamo wa chama tawala, CCM kwa upande mmoja na wale upinzani hasa Chadema, kwa upande mwingine.
Wote wameshambuliana na kutuhumiana kuhusu vyanzo au sababu za matukio hayo ambayo yamezidi kujitokeza na kuchafua sifa ya taifa hili.
Maneno mengi yamesemwa kuhusu matukio hayo, kiasi kwamba kupitia safu hii tumejitahidi kuweka wazi msimamo wetu kwamba hatuiungi mkono mizozo na migogoro ambayo inazidi kujitokeza.
Tunasema nchi yetu inahitaji utulivu, umakini, busara katika kutatua mizozo na migogoro ambayo imejitokeza.
Hata leo bado tunashauri kuwa kamwe hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja katika mizozo hii inayoendelea nchini mwetu na kuhusisha wanasiasa, viongozi, wanaharakati au hata wananchi.
Tunaamini, kauli hizi ambazo zimekuwa zikitolewa na viongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa hazina tija. Tujielekeze kwenye utatuzi wa mizozo au migogoro ambayo inaota mizizi na siyo kuikuza. Ni vyema viongozi wetu wote, wale walioko madarakani au wa vyama vya siasa wawe makini kwa kauli na ndimi zao zinazoweza kuisambaratisha nchi.
Tunasema kauli zinazochochea vyombo kama polisi kujichukulia sheria mkononi kwa kisingizio cha kutuliza ghasia, kuleta amani kwa vyovyote vile hazikubaliki, hata kama zimetolewa na kiongozi mkubwa au mwenye ushawishi kiasi gani.
Viongozi wa vyama vya siasa na Serikali, watumie nafasi zao kuwaeleza wananchi na wanachama wao kuheshimu sheria na kuzitii bila shurti, kama kaulimbiu ya Jeshi la Polisi inavyosema.
Kwa upande mwingine, vyombo vya dola ikiwamo polisi navyo viongozwe na misingi ya sheria, taratibu au kanuni za kuanzishwa kwao, siku zote vitimize wajibu wao kwa umma tena kwa uadilifu usiotiliwa shaka. Siku zote vijiepushe kuwa chanzo au sababu za kuendelea kwa vurugu hizi ambazo zinajitokeza katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.