Bukobawadau

Bagamoyo lango la biashara ya dawa za kulevya

JUMATATU, JULAI 08, 2013 04:22 NA GUSTAPHU HAULE, KIBAHA
WILAYA ya Bagamoyo mkoani Pwani imetajwa kuwa ni lango kubwa linalotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kupitisha madawa ya kulevya na wahamiaji haramu kutoka Ethiopia, Sudan na maeneo mengine. Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza amemwagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Ahmed Kipozi kuhakikisha anaimarisha ulinzi katika mipaka ya wilaya kuhakikisha vitendo hivyo vinadhibitiwa .

Mahiza alitoa kauli hiyo juzi alipozungumza na viongozi wa dini na wa vyama vya siasa kujadili jinsi ya kukomesha vitendo vya matumizi ya madawa ya kulevya kwa vijana na suala nzima la amani.

Alisema maeneo ya Chalinze na mipaka ya Bagamoyo haina ulinzi wa kutosha jambo linalosababisha baadhi ya watu kutumia mianya hiyo kupitisha madawa ya kulevya.

Hata wahamiaji haramu hupita kwa urahisi hivyo ni lazima ulinzi uongezwe katika wilaya hiyo, alisema.

"Bagamoyo imegundulika kuwa ni wilaya pekee ya Mkoa wa Pwani ambayo imekuwa ikitumika kama lango kuu la kupitia watu haramu na madawa ya kulevya.

“Leo nakuagiza DC nenda kaimarishe ulinzi kupitia jeshi la polisi ili watu wanaokiuka sheria za nchi wakamatwe,'' alisema Mahiza.

Katika mkutano huo, Mahiza aliwapa darasa viongozi wa dini kwa kuwataka waache kupokea watu wasiowajua katika makanisa na misikiti yao.

Alisema na kama wanataka kuwapokea ni vema wakafanya uchunguzi wa kujua mahali walipotoka na hata kazi wanazofanya kwa vile wapo magaidi wanaoingia nchini kupitia makanisa na misikiti.
Next Post Previous Post
Bukobawadau