Bukobawadau

Maandamano yazuka baada ya Zimmerman kuachiwa huru

Rais wa Marekani  Barack Obama ameomba  kuwe na  hali ya utulivu Jumapili baada ya mahakama moja katika jimbo la Florida kuamua kuwa George Zimmerman aliyekuwa akifanya  doria za kujitolea katika mtaa wake hana hatia.
Uamuzi huu ulifuatia  kesi iliyofuatiliwa kwa karibu na umma wa Marekani ambapo Zimmerman alishtakiwa kwa kumpiga risasi na kumuua kijana M’marekani mweusi asiyekuwa na silaha.

Katika taarifa ya maandishi bw.Obama alisema mauaji ya Trayvon Martin yanahuzunisha  familia yake na Wamarekani.Kesi hiyo pia imetawala vyombo vya habari vya Marekani kwa wiki kadha sasa. Kulizuka  maandamano ya amani katika miji kadhaa ya Marekani kufuatia uamuzi huo, wengi wakisema ‘ikiwa hakuna haki hakutakuwa na amani’

Rais Obama aliomba  kuwe na utulivu  akisema  Marekani ni taifa linalofuata sheria na kwamba  baraza la mahakama limeamua.  

Kesi dhidi ya Zimmerman iliamuliwa Jumamosi usiku. Baraza la majaji likisema limefikia maamuzi ya kauli moja kwamba hana hatia. Uamuzi huo ulitangazwa moja kwa moja kwenye televisheni  za Marekani na mitandao ya mawasiliano ya Internet na kuzua mjadala wa kitaifa kuhusu  ubaguzi wa rangi na kesi za uhalifu nchini Marekani.

Martin mwenye umri wa miaka 17 aliuwawa mwaka jana katika makabiliano na Zimmerman aliyekuwa na bunduki. Zimmerman ni mwana wa M’marekani mzungu na mama mwenye asili ya kihispania.
Next Post Previous Post
Bukobawadau