Bukobawadau

WACHEZAJI WENYE IMANI YA DINI YA KIISLAM WANAVYOBADILI UTAMADUNI WA LIGI KUU YA ENGLAND



Wakati Premier League ilipoanza mwaka 1992, kulikuwepo na mchezaji mmoja tu aliyekuwa na imani ya dini kiislam, kiungo wa Tottenham anayetoka Spain Nayim. Ligi hiyo ya juu kabisa  nchini England sasa ina zaidi ya wachezaji 40 wanaofuata imani ya dini ya kiislam - na wachezaji wanaleta mabadiliko makubwa kwenye mchezo wa soka nchini England. 
Tarehe 5 February, 2012, Newcastle United ilicheza na Aston Villa kwenye uwanja wa St James' Park na baada ya dakika 30 za mchezo huo, Demba Ba alifunga bao kwa upande wa Newcastle. Akakimbia mpaka kwenye kibendera na kuungana na msenegali mwenzie Cisse. Wachezaji hao wawili wenye imani kali ya dini yao walishangilia kwa kusujudu. 
Kukua kwa idadi ya wachezaji wa kiislam inazidi kukua kila siku baada nguvu ya soka kuongezeka kwenye anga ya kimataifa.
Maskauti wa kusaka vipaji wamesambaa dunia nzima kusaka vipaji vipya na premier league imekuwa kivutio zaidi kutokana na umaarufu na ukubwa wa mishahara ya wachezaji.  

Vijana wadogo kutoka maeneo ya Afrika Magharibi, kaskazini na hata au kwenye maeneo wanayoishi watu wenye kipato cha chini kwenye viunga vya mji wa Paris - vijana hawa sasa wamekuwa mastaa wakubwa. 
Wanaweza wakawa matajiri na maarufu kwa kwa sasa wakichezea kwenye vilabu vya kiingereza, lakini wengi wao bado hawajasahau mizizi ya utamaduni wao, kitu ambacho kinawaongoza na kuwaunganisha pamoja majaribu ya kidunia - imani yao ya kiislamu. 
Wakati mchezaji wa ubora wa Demba Ba, ambaye aliondoka Newcastle mwaka uliopita na kujiunga na Chelsea, anaposema kwamba ni mtu anayefuata kwa umakini imani ya dini yake, baadhi wanaweza kutoa hoja kama vilabu vinaweza kusikiliza matakwa yao. 
Wachezaji wa kiislam wanapewa mahitaji yao muhimu yanayoendana na imani ya dini yao - kuanzia chakula, mavazi, na pia huwa wanapewa muda wa kufanya ibada zao - hii ni zaidi kwa wanasoka ambao bado wanakuwa wanaishi kwenye zile academy. 
Mpaka hivi karibuni, wachezaji wote wa Premier League ambao wanashinda zwadi ya mchezaji bora wa mechi wamekuwa wakizawadia chupa ya shampeni.
Lakini kwa wachezaji wa kiislam, vilevi vimekatwaza. Hivyo wakati kiungo wa Manchester City Yaya Toure alipokataa kiustaarabu kupokea zawadi wakati akifanyiwa mahojiano kwenye Television - akisema kwamba ni kinyume na imani ya dini yake, waratibu wa 'man of the match' ikabidi wakae na kufikiria cha kufanya. 

Shampeni iliondolewa kama zawadi na badala yake sasa wachezaji wote wanaoshinda tuzo ya 'man of the match' watakuwa wanapokea kikombe kidogo.

Wakati Liverpool waliposhinda ubingwa wa kombe la ligi katika fainali ya mwaka 2012, wachezaji wa Liverpool wakiongozwa na nahodha wa Steven Gerrard waliondoa nguo za daktari wa timu, ambaye ni muislam, nje ya chumba cha kubadilishia nguo ili vilevi visije vikamwagikia nguo hizo. 

Bado kunakuwepo na changamoto nyingi sana wakati waislamu wakiwa kwenye ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. 

Ni vipi wachezaji ambao hawali wala kunywa kwa masaa zaidi ya 12 wanaweza kucheza kwa kiwango cha juu kwa dakika 90? 
Baadhi ya wachezaji wanasisitiza kutimiza ibada ya kufunga. Wengine wanaweza kufunga wakiwa kwenye mazoezi lakini sio kwenye mechi. Klabu zinajaribu kwa kila hali kufuata matakwa ya imani za wachezaji wao, lakini haiwezi kuwa kipindi rahisi kwa wachezaji au makocha. 
Kiungo wa Arsenal Abou Diaby, 27, anasema: "Arsenal wangependa mie nisifunge, lakini wanaelewa kwamba huu ni wakati muhimu kwangu na wanajaribu kwa kila hali kufanya mambo yaende kiurahisi."
Ba, 28, anakiri kwamba amewahi kuwa na matatizo na makocha wake kuhusu suala la kufunga, lakini anasema amekuwa imara kusimamia imani yake. 
"Mara zote nimekuwa na kocha ambaye amekuwa hana furaha na jambo la kufunga, nimekuwa nawaambia: 'Sikiliza, nitafunga. Ikiwa kiwango changu bado kipo vizuri nitaendelea kucheza; ikiwa jambo hilo ni baya basi usinipange kwenye timu, hivyo tu.'"
Mchezaji wa zamani wa Stoke Mamady Sidibe, 33, anasisitiza: "Kuna wachezaji ambao wanafunga na wanafanya vizuri uwanjani, na kunakuwa hamna tatizo lolote. Kwa upande wangu mie wakati wa Ramadhani siku ya mechi sifungi ili nisiwape visingizio watu wengine."
Bahati nzuri kwa pande zote mbili, Ramadhan mwaka huu inaisha August 7, siku 10 mbele kabla ya msimu mpya wa Premier League kuanza. 

Mikataba ya udhamini nayo imekuwa ikileta utata. Timu ambazo zinatangaza biashara ya kamari na mikopo kwenye jezi zao zimekuwa zikiwaweka wachezaji wa kiislamu kwenye wakati mgumu, kwasababu wanakuwa wanatumika kutangaza biashara ambazo zinaenda kinyume na imani ya dini yao. 
Mwezi uliopita Papis Cisse alisema kwamba anapanga kuongea na Newcastle na wadhamini wao wapya, Wonga, kwa sababu alikuwa na mashaka kwamba imani yake haiwezi kumruhusu kuonekana akiwa amevaa jezi ya kuipromoti kampuni hiyo ya kamari, pia kukawa na tishio kwamba baadhi ya wachezaji wengine waislamu wa Newcatle kama vile Ben Arfa, Moussa Sissoko and Mapou Yanga-Mbiwa, wangefuata mkumbo, lakini kwa bahati nzuri hawa wengine jana walionekana wakifanya mazoezi huku wakiwa na vizibao vyenye nembo ya Wonga, ingawa bado Cisse ambaye hakuwepo mazoezini bado anaonekana kutokuwa tayari kuitangaza Wonga.





Golikipa wa Wigan Ali Al-Habsi ambaye anatajwa kuwa na asili ya Tanzania visiwani, lakini ni raia wa Oman, analizungumzia hili suala: "Sisi wachezaji na hivi vitu vinatoka kutoka klabu, hatuwezi kufanya chochote kuhusu suala la udhamini, tunachopaswa ni kufanya kazi yetu. Pia waislamu wote wanajua kwamba kamari ni dhambi - hili limeandikwa kwenye vitabu vitakatifu na pia mawaidha yanatolewa kila siku hivyo mie nikivaa shati ya Wonga haimanishi kwamba nimesema watumie."


Mashabiki pia wamekuwa wakijifunza vitu vingi kupitia wachezaji wa kiislamu. 

Baadhi ya watoto wanaocheza kwenye viwanja vya bustani ya Newcastle wamekuwa wakionekana wakisujudu kila pale mchezaji mwenzao anapofunga goli.
Wanaweza wasiwe wanaelewa hasa nini kitendo hicho kinamaanisha, lakini ni ishara kwamba matendo ya wachezaji wa kiislamu yameanza kufahamika katika utamduni wa kiingereza. 
BY AIDAN CHARLIE SEIF

Next Post Previous Post
Bukobawadau