Bukobawadau

MASWALI MAGUMU Na Ansbert Ngurumo

MACHI 10, mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, alifanya kikao na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Waziri Nchimbi, aliwatangazia waandishi kuwa aliwasimamisha kazi maofisa sita wa polisi kwa rushwa, biashara ya mihadarati, kufungua kesi za uongo na kufanyahujuma katika operesheni za biashara haramu ya madawa ya kulevya.

Nchimbi pia aliuarifu umma kuwa Msaidizi Mkuu wa Kamishna wa Polisi, Renatus Chalamila, alisimamishwa kwa mwezi mmoja baada ya kushukiwa kupokea rushwa kutoka kwa askari wanafunzi 95 ili kuwaruhusu wajiunge na Chuo cha Polisi cha Moshi (CCP).

Nanukuu maneno ya Nchimbi: “Sina madaraka kwa Chalamila, kwa hivyo nimemsimamisha kazi kwa mwezi mmoja na kuipeleka kesi yake kwa rais, ambaye ndiye mwenye madaraka ya kumteua,” Nchimbi aliiambia Sabahi. “Wanafunzi hao 95 nao pia wamefukuzwa.”

Ni muda mrefu sasa, tunatarajia ushahidi huu wa wazi uliotangazwa na Waziri Nchimbi ulikuwa ni wa kweli, tena tunajua pengine ulifanyika kwa kuzingatia maadili ya polisi na sheria za nchi, na hatuamini kuwa kuutangazia umma wa Watanzania suala hili hakukufanyika kisiasa.

Nchimbi aliuarifu umma wa Watanzania kuwa rais alikuwa nje ya nchi, na kwa sisi wafuatiliaji wa mambo ya nchi tunajua siku hiyo hiyo rais alirejea nchini baada ya ziara ya siku tatu nchini Afrika Kusini.

Siku hiyo hiyo aliporejea Rais Kikwete alikwenda hospitalini kumjulia hali na kumpa pole mzee Yusuf Mzimba, mmoja wa wazee maarufu wa Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (YANGA) ambaye alilazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiuguza majeraha kufuatia kugongwa na bodaboda katika Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.

Tangu rais arejee nchini ni miezi takriban minne sasa, je, Kikwete ameshindwa kumchukulia hatua kigogo huyo wa polisi aliyekwapua pesa za watoto wa maskini?

Rais wetu ana utamaduni wa kukaa meza moja na wahalifu akawasamehe kimya kimya kama alivyofanya wakati wa sakata la EPA, wezi walirudisha pesa, tukaambiwa zimepelekwa kwenye mfuko wa pembejeo lakini hadi sasa wezi wenyewe hawajawahi kuonekana.

Ni katika Tanzania tu ndiyo tumeshuhudia utamaduni wa wezi kuombwa kurejesha walichoiba na kusamehewa na rais kimya kimya. Je, utaratibu huu ndio rais anataka kuutumia kumlinda kigogo huyu wa Polisi?

Rais Kikwete anakubaliana na utaratibu huu? Sakata hili la kuchangishwa vijana pesa kwa ajili ya kupelekwa Chuo cha Polisi ili baadaye watafutiwe kazi za usalama au TAKUKURU lilichafua nchi yetu na Idara ya Usalama wa Taifa kuonekana si sekta nyeti kwa usalama wa nchi. Kwanini Kikwete hachukui hatua?

Askari wote walibainika kuwa na makosa kwa wakati mmoja, wangekuwa chini ya Nchimbi wote wangefikishwa katika mahakama za kijeshi na kutimuliwa kama walivyofanyiwa wengine. Haki iko wapi kumfukuza mmoja na kumwacha mwingine?

Jeshi la Polisi na serikali siku za hivi karibuni wameonyesha kuwa wapo makini kutafuta ushahidi wa matukio mbalimbali.

Taarifa za kutapeliwa vijana wapatao 120 kwa ahadi ya kuwapa ajira katika Idara ya Usalama wa Taifa na TAKUKURU zilisharipotiwa tangu mwaka jana.

Kati ya Agosti 5 na 7, mwaka jana vijana hao 120 kwa nyakati tofauti walipata taarifa kwamba kuna nafasi za kazi Idara ya Usalama wa Taifa na TAKUKURU na kwamba nafasi hizo zinapatikana kupitia kwa vigogo wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Kwa kupitia kwa vigogo wa polisi na mke mmoja wa kigogo wa polisi, inadaiwa kwamba watu hao ambao wengi wao ni wenye elimu ya chuo kikuu walielezwa kwamba ili kupata kazi hizo ni lazima watoe fedha kati ya sh 700,000 hadi sh milioni moja.

Walielezwa kuwa mafunzo ya kazi hizo yatatolewa kwa miezi minne katika vyuo vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vilivyopo eneo la Mbweni (Dar es Salaam), Zanzibar na Monduli (Arusha).

Siku ya kwanza ambayo waliambiwa kukutana katika viwanja vinavyozunguka Uwanja wa zamani wa Taifa, karibu na Ofisi za Baraza la Michezo Tanzania (BMT), ili wapelekwe Mbweni kwa ajili ya kupangiwa vituo vyao vya kazi walielezwa kwamba baadhi yao majina yao yalikuwa hayajaingizwa katika mfumo.

Baada ya wiki moja walitakiwa kukutana tena eneo hilo ili kupelekwa, lakini walielezwa kuwa wangepelekwa Septemba 2, mwaka huu kwa kuwa baadhi yao hawakuwa na namba.

Ilipofika Septemba 2, vijana hao wakati wakielekea Mbweni, walielezwa kuwa muda umekwenda na hawataweza kupokewa katika kambi hiyo hivyo kupangishiwa nyumba za kulala wageni maeneo ya Tegeta.

Hizi hazikuwa taarifa za kupendeza hata kidogo kwani hata Chuo

cha Polisi, Waziri Nchimbi aliutangazia umma kuwa waliwaondoa vijana wapatao 95 ambao waliingizwa kwa utaratibu kama huu. Rais alikwisharudi nchini, kwanini asichukue hatua? Anasubiri nini?
Next Post Previous Post
Bukobawadau