Mbowe adai polisi walivamia usiku makazi yake D’Salaam
Dar es Salaam. Polisi kadhaa wanadaiwa kuvamia nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kwa lengo la kumkamata.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mbowe mwenyewe zinaeleza kuwa askari hao waliokuwa na silaha walivamia nyumba hiyo iliyopo eneo la Mikocheni, jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia jana wakiwa na silaha.
Mbowe alisema hata hivyo walikwama kumkamata, kwa sababu alikuwa nje ya Dar es Salaam kwa shughuli za chama.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alikataa kuzungumzia zaidi suala hilo akieleza kuwa anayeweza kulizungumzia zaidi ni Ofisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Camillius Wambura alipoulizwa alisema kuwa hana taarifa za polisi kumtafuta Mbowe.
“Sina taarifa polisi wangu kumtafuta Mbowe,” alisema Wambura.
Lakini Ofisa Habari wa Chadema Tumaini Makene aliliambia Mwananchi Jumapili jana kuwa askari hao walifika nyumbani kwa Mbowe saa 7:16 usiku, wakidai kuwa na hati ya kumkamata Mbowe kutokana na makosa ambayo hata hivyo hawakuyabainisha.
“Ni kweli askari walifika nyumbani kwa Mwenyekiti wakidai walikuwa wakihitaji kumkamata. Kinachotushangaza ni kwamba mtu ambaye anafahamika na wanajua ni mbunge na kiongozi wa chama, lakini wanakwenda kumkamata kama jambazi, usiku wa manane,” alisema Makene.
Alisema kuwa polisi hao walifika nyumbani kwa Mbowe na kukutana na walinzi katika nyumba hiyo, waliowaeleza kuwa mwenyekiti huyo wa Chadema alikuwa safarini.
Makene hakuwataja majina walinzi waliokutwa , lakini nalisisitiza kwamba polisi hao waliacha namba za simu kwa walinzi hao, wakitoa maelezo kuwa pindi Mbowe atakaporejea wamwarifu na kuwapigia polisi kwa kuwa alikuwa akihitajika kituoni.
Ofisa huyo alieleza kuwa wakati wa tukio hilo Mbowe hakuwapo nyumbani na alikuwa safarini mkoani Kilimanjaro, kuhudhuria vikao vya Halmashauri ya Hai.
Makene alisema wanashangazwa na vitendo vya Polisi kusaka viongozi wao usiku wa manane kama majambazi sugu, wakati wakifahamika ni wabunge.