Bukobawadau

Mrajis Msaidizi Kagera na njama za kuiangamiza KCU (1990) Ltd

Na Prudence Karugendo
BAADA ya malalamiko ya muda mrefu ya wanaushirika wa KCU (1990) Ltd., chama kikuu cha ushirika mkoani Kagera, kuhusu mwenendo mbovu wa chama chao, ubovu unaoletwa na uongozi unaokiendesha chama hicho kwa njia za kifisadi, sasa kumejitokeza tetesi kwamba kuna maagizo kutoka katika mamlaka ya juu serikalini yanayokitaka chama hicho kiitishe mkutano mkuu wa dharura kusudi ufanyike uchaguzi wa viongozi wapya watakaochukua nafasi za viongozi wa sasa wanaolalamikiwa kwa ufisadi.
Tetesi hizo zinaonekana kuwachanganya viongozi wa KCU (1990) Ltd., wa kuchaguliwa na wa kuajiriwa. Sababu kama ambavyo wameishatamka, Waziri Mkuu na Waziri wa kilimo, Chakula na Ushirika, kwamba wote wanaofanya ufisadi kwenye vyama vya ushirika wanapaswa kufikishwa mahakamani, ni wazi kwamba viongozi wote wa ushirika wanaojielewa wanafanya ufisadi na kuishi kwa kujineemesha kwa jasho la wakulima wapate kiwewe.
Kwahiyo habari ambazo zimeishasambaa Bukoba na maeneo yote yenye vyama vya msingi vinavyoiunda KCU (1990) Ltd. na kuthibitishwa na wanaushirika huo, ni kwamba uongozi wa KCU (1990) Ltd. umekula njama pamoja na Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Kagera za kuutibua mpango wa kuunusuru ushirika huo wa KCU (1990) Ltd..
Inasemekana uongozi wa chama hicho kikuu cha ushirika umetenga fungu kubwa la pesa, ambazo hazieleweki zinapatikanaje kutokana na uongozi huo kuwaeleza wanaushirika kuwa chama kiko kwenye ukata mbaya, na kumkabidhi Mrajis Msaidizi pamoja na gari ili akawazungukie wawakilishi wa vyama vya msingi katika maeneo yao na kuwahonga pesa hizo (rushwa). Lengo ni kuwashawishi wawakilishi hao, ambao ndio wajumbe wa mkutano mkuu wa chama kikuu cha ushirika, wayakatae mabadiliko ambayo yataagizwa kufanyika katika chama hicho.
Na kwa vile sheria za vyama vya ushirika zinawapa turufu wajumbe wa mkutano mkuu kulikubali au kulikataa jambo, ndiyo maana uongozi huo ukabuni njama za kuwahonga wajumbe hao. Sababu wajumbe wakilikataa jambo , ni kwamba ushirika kwa maana ya wanaushirika, ndio wanaokuwa wamelikataa. Na huwezi kuwaambia wanaushirika kuwa ushirika wenu unayumba wakati wao wakionesha kwamba hauyumbi halafu wewe ukaonekana una hoja.
Jambo linaoonesha hatari inayoukabili ushirika ni hilo. Wanaopewa jukumu la kuuongoza ushirika wanaufisidi kwa kuuendesha kwa maslahi yao binafsi, wawakilishi wa wanaushirika, wanaotumwa wakaukague ushirika wao, wanahongwa ili wakaubariki ufisadi unaofanyika kwenye ushirika huku wakifanya kila njia ili yasitokee mabadiliko ya kuuondoa ufisadi huo!
Mrajis Msaidizi ambaye ni mwajiriwa wa serikali aliyewekwa mahususi kuulea ushirika katika eneo husika na kuhakikisha unajiendesha kwa ufanisi huku maadili yote ya ushirika yakiwa yamelindwa, anahongwa na mafisadi ndani ya ushirika ili kwa mamlaka aliyopewa ahakikishe wanaushirika wanakubali kuubariki ufisadi ndani ya ushirika wao.
Ni kwamba wawakilishi wa vyama vya msingi wakishaubariki ufisadi ndani ya chama chao kikuu moja kwa moja inaonekana wanachama wote wameukubali ufisadi na hawana tatizo nao. Na haya yanafanyika kwa vile wakulima walio wengi hawana uelewa mpana wa masuala ya ushirika. Kwahiyo wajanja wachache ndani ya ushirika wanalitumia kiufisadi tobo hilo kwa manufaa yao wakiwa wamewatelekeza wakulima wavuja jasho.
Nilipojaribu kumpigia simu Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika wa Kagera ili kupata kauli yake kuhusiana na tuhuma hizo, mwanzoni hakutaka kuonyesha ushirikiano, simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa. Baadaye nikamtumia ujumbe wa maandishi, vilevile hakujibu. Nilipomtumia ujumbe wa pili nikimweleza kwamba kunyamaza kwake kunamaanisha kukubaliana na tuhuma dhidi yake, ndipo akajibu kwa ufupi kwamba amefuatilia mwenendo wa mahojiano yangu huo ni uzushi hakuna kitu cha namna hiyo.
Madai mengine yanayotolewa na wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. na kuonyesha ubovu wa chama hicho ni kuhusu upoteaji wa kahawa njiani wakati ikisafirishwa kwenda Moshi kwenye mnada. Wanasema kwamba limekuwa jambo la kawaida tani nyingi za kahawa kupotelea njiani bila uongozi wa chama chao kuwachukulia hatua zozote wafanyabiashara ya usafirishaji waliopewa kandarasi ya kusafirisha kahawa ya ushirika huo kwenda mnadani Moshi.
Pamoja na hayo yote jambo linaloonekana kuwatatanisha sana wanaushirika hao ni mwenendo wa kusuasua ilionao serikali juu ya masuala yanayowagusa moja kwa moja wananchi kiuchumi kama hili la KCU (1990) Ltd.. Wanasema tangu waliposoma kauli ya Waziri Chiza kwamba atamuamuru Mrajis wa Vyama vya Ushirika ahakikishe unaitishwa mkutano mkuu wa dharura wa chama chao sasa zimepita wiki tatu wakati Chiza alisema jambo hilo lingefanyika ndani ya siku 7.
Wanasema kwamba badala ya kuona mkutano mkuu wa dharura wanaishia kupata majigambo ya uongozi wa KCU (1990) Ltd. kwamba kama waziri mwenyewe kashindwa kuwafanya lolote itawezekanaje kwa Mrajis?
Eti viongozi hao wa chama chao wanatamba kwamba Chiza alitoa siku 7 na hakijafanyika chochote sasa nani mwingine wa kuwaletea maneno? Kwamba Chiza aliyasema hayo kuwafurahisha watu wa magazeti ili wapate cha kuandika lakini kimsingi hana lolote la kuufanya uongozi huo wa KCU (1990) Ltd..
Swali kwa Mheshimiwa Chiza ni kwamba; hivi ni kweli hana la kuwafanya watu hawa wanaowatesa wakulima kiasi hiki?
Wanaushirika hao wanasema kwamba mwenendo huu wa kusuasua ilionao serikali katika masuala nyeti, maana uchumi wa wananchi ni suala nyeti sana, ndio unaowasababisha hata wao, viongozi waandamizi wa serikali, wafikie hatua ya kupakwa matope na mafisadi kwa kuwafanya ni wenzao katika mikakati ya kifisadi.
Wanasema kwamba katika majigambo na tambo kama zile za kwamba Chiza hawezi kuwafanya lolote ndimo kunamojitokeza hisia za kwamba pengine kusuasua kwa waziri kuwachukulia hatua watu hao kuna anachokifahamu kinachoendelea kilicho cha manufaa kwake. Kwa hiyo wananchi watamuona waziri kama anaulinda uhalifu kwa sababu anazozijua yeye, kitu ambacho ni uamuzi wa wazi wa waziri husika kukubali kupakwa matope. Hilo ni jambo lisilopendeza hata kidogo.
Wananchi wanapokilalamikia kitu kinachojionyesha wazi ni vizuri wahusika wakakichukulia hatua mara moja bila kusita katika kuilinda heshima ya uongozi na kuulinda uongozi bora. Lakini wanapositasita kuchukua hatua ni lazima zijitokeze hisia za kwamba uhalifu unalindwa kwa makusudi, hiyo ni dosari katika uongozi bora, na heshima ya uongozi inakuwa imepata kutu.
Kwa msisitizo mkubwa, wananchi mkoani Kagera wanasema kwamba kwa kiasi kikubwa Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani humo, wanayemtaja kwa jina la Rwekiko Nestory Shoros, ndiye amekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo ya ushirika mkoni humo. Eti badala ya yeye kusimamia maadili ya ushirika jinsi wajibu wake ulivyo amegeuka na kuwa msitari wa mbele katika kuyapindisha maadili hayo.
Wanasema kwamba yeye ndiye amekuwa akizivuruga kanuni na taratibu za ushirika ili ziwalinde viongozi wabadhirifu wa mali za ushirika kusudi waendelee kukaa kwenye uongozi hata pale muda wao unapokuwa umeisha kikanuni.
Wengine wanasema kwamba hata pale zilipojitokeza fununu kuwa kuna uwezekano wa kuitishwa mkutano mkuu wa dharura wa KCU (1990) Ltd. kwa ajili ya uchaguzi mpya unaotakiwa kuuondoa uongozi uliopo kwa sasa, eti yeye Shoros ndiye aliyewambia viongozi wa KCU (1990) Ltd. kwamba hawapaswi kuwa na wasiwasi sana, kwamba kilichopo wamwezeshe ili akawazungukie wawakilishi, wajumbe, katika vyama vyao vya msingi na kuwashawishi wakajenge msimamo wa pamoja.
Hiyo maana yake ni kwamba wawakilishi wa wakulima wa kahawa wajenge msimamo wa pamoja wa kukiangamiza chama chao wakiwa wamewasaliti wakulima waliowatuma kukilinda!
Kwa maana hiyo, wakulima wa kahawa ambao ni wanachama wa KCU (1990) Ltd. wanasema kwamba kama kweli zipo jitihada za zozote za kuunusuru ushirika wao huo zingeanza kwa kuwaondolea tishio la Shoros.
Wanasisitiza kuwa Mrajs huyo Msaidizi ndiye amegeuka tishio la kwanza la ushirika wao. Eti hapaswi hata kidogo kuendelea kusimamia vikao vya chama chao kikuu cha ushirika kwa vile kaishajigeuza saratani katika ushirika huo, na kwamba yeye kama sehemu ya watuhumiwa wakubwa wanaokizorotesha chama chao anawezaje kuwa tiba ya ugonjwa unaokikabili?
Wanatoa angalizo kwamba mhalifu asiposhughulikiwa mapema akabaki kupokea tu makaripio yasiyoisha matokeo yake makaripo hayo yanamjengea sugu na kumfanya awe mhalifu wa jadi asiyeshtushwa na lolote, na hivyo kuendeleza uhalifu usiokoma wala kukomeshwa.
Kwahiyo jambo analoweza kulifanya Chiza na Wanakagera wasimsahau ni kuunusuru ushirika wao kwa kuwaondolea uongozi unaokaribia kukizika chama chao bila kukichimbia kaburi.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau