Muungano si kazi ya Mungu, uboreshwe
Na Msiba Pakia
KWA muda mrefu nilikuwa sijaandika makala
kuchangia mawazo yangu kwenye mwenendo wa mambo katika nchi yetu. Ni kutokana
na msuguano wa shughuli za maisha, nikatoweka machoni mwa wasomaji wangu.
Lakini sasa
kufuatia kuwepo kwa mchakato nyeti unaoendelea wa kuadika katiba mpya ya nchi
yetu, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimeona bora na mie nichangie
mawazo yangu nikiwa hasa nimeulenga muungano wa nchi yetu.
Muungano wa
Tanzania umekumbwa na misukosuko katika miaka ya karibuni kutokana na
malalamiko hasa yanayotokea upande mmoja
wa muungano. Wazanzibari wamekuwa wakiyalalamikia baadhi ya mambo katika
muungano na kuonesha kwamba hayautendei haki upande wa Zanzibar kutokana na
kuonekana yanakiuka baahi ya makubaliano
ya msingi yaliyomo katika Hati ya Muungano.
Kwahiyo
katika kujaribu kuuboresha muungano kupitia katika katiba mpya inayoandaliwa,
yakiwa yameondolewa mambo hayo yanayoonekana kuwa kero kwa muungano, Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba, imekuja
na rasmu iliyotokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na tume hiyo.
Moja ya
mambo yaliyomo katika rasmu hiyo ni muundo wa serikali tatu katika Muungano wa
Tanzania. Hilo ni jambo lililotokana na maoni ya Watanzania walio wengi na tume
kuamua kulitendea haki jambo hilo.
Kitu cha
ajabu ni kwamba rasmu iliyoletwa na tume iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, aliye pia mwenyekiti wa chama tawala, CCM, inaonekana
kupingwa kwa nguvu zote na chama hichohicho tawala! CCM inaipinga rasmu hiyo
hasa kwa upande wa serikali tatu zinazotajwa kwenye rasmu hiyo. Hapo ndipo
ninapotaka nijikite.
Muungano wa
aina yoyote unaohusisha pande mbili haunabudi
kuyaheshimu matakwa ya pande zote mbili bila upande mmoja kuonekana
unataka upewe ushawishi zaidi katika muungano husika huku upande wa pili
ukibaki kunung’unika. Ndiyo maana Tume ya Mabadiliko ya Katiba ikaona bora
ilete rasmu ya serikali tatu kama ilivyotolewa maoni na wananchi walio wengi,
kusudi pawepo na Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya
Muungano.
Lakini Chama
Cha Mapinduzi nacho kinakuja na msimamo wake kwamba liwe jua au iwe mvua ni
lazima muungano ubaki na serikali mbili tu.
Sielewi
msimamo huo wa CCM umelenga kumnufaisha nani. Angalia, Watanzania, ambao ndio
wenye nchi, wanasema tunataka serikali tatu, lakini chama tawala ambacho kinaonekana
kunogewa na utawala, kinasema ni lazima serikali mbili tu! Kwa maana hiyo
katika muungano huu chama tawala kiko tofauti na wananchi. Na kama ni hivyo
kinayoyafanya ni kwa manufaa ya nani?
Sijui
mtawala na mwenye nchi nani anapaswa kupewa kipaumbele katika maamuzi, hasa
ikizingatiwa kwamba hii ni karne ya maridhiano, wakati ubabe wa kiimla vimebaki
katika historia.
Ninaloliona
hapa ni kwamba watawala hawa na chama chao wanalenga kuulinda uwepo wa chama
chao kuliko wanavyofikiria kuulinda uwepo wa muungano na taifa la Tanzania kwa
ujumla. Wasiwasi wao ni kwamba nje ya serikali mbili, kama ilivyo kwa sasa,
chama chao kitakosa mizizi na kushindwa kuhimili changamoto zinazojitokeza kwa
sasa na hivyo kuishia katika kusambaratika.
Ni wazi
kwamba kwa wakati huu CCM imezidhibiti hizi serikali mbili, hata kama si kwa
ushawishi, ila kwa mabavu inaweza. Itakapojitokeza serikali ya tatu hata mabavu
ya CCM yatakuwa yamenywea kutokana na kukosa ngome maalumu.
Ikumbukwe
kwamba CCM ndiyo inayodhibiti madaraka katika pande mbili za muungano, kwa
maana ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Lakini CCM
haina uhakika mambo yatakuwaje iwapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano itasema kwamba
muungano wa Tanzania uendeshwe kwa serikali tatu, Tanganyika, Zanzibar na
Tanzania.
Hilo ni
jambo linaloitia CCM tumbo joto lakini likiwa limewapa faraja wananchi wa nchi
hizi mbili hasa Wazanzibari wanaojiona wamemezwa ndani ya Tanganyika.
Ni jambo la
ajabu kwamba Watanganyika hawalalamiki kuhusu nchi yao, Tanganyika. Tangu baada
ya muungano Watanganyika walitulia na kuiacha nchi yao isahaulike. Ni
Wazanzibari tu, ambao lakini nchi yao iliendelea kuwepo ndani ya muungano,
wanaolalamika kwamba muungano uliipokonya mamlaka nchi yao.
Muonekano
jinsi ulivyo ni kwamba Wazanzibari wanahisi kama vile iliyokuwa Tanganyika
ndiyo iliyoamua kubadili jina na kuwa Tanzania huku Zanzibar ikibaki na jina
lake lakini hadhi yake ikishuka na kukalibiana na hadhi ya mkoa. Hilo ndilo
tatizo kuu linalowasumbua Wazanzibari.
Wao wanasema
kwamba Watanganyika hawapigi kelele kuhusu Tanganyika yao kwa sababu kila
kilichokuwa chao walibaki nacho. Watanganyika walibaki na sarafu yao, Benki kuu
yao, wakabaki na uhusiano wa kimataifa, wakabaki na kiti chao Umoja wa Mataifa
ambako ilipelekwa taarifa tu kwamba Tanganyika imebadili jina na kuwa Tanzania
huku kiti cha Zanzibar kikiyeyuka kiana, nakadhalika.
Lakini
Zanzibar inaonekana kupoteza vyote ila ikibaki na jina tu ambalo inashindwa
kulitumia kufanikisha malengo yake kwa vile sio nchi kamili inayotambulika
kimataifa. Hili jina la nchi isiyotambulika ni sawa na kilemba cha ukoka.
Ieleweke
kwamba Wazanzibari hawawezi kuendelea kukifurahia kilemba hiki cha ukoka cha
kuwa na serikali yao ya mapinduzi, rais wao, Bunge lao – Baraza la Wawakilishi,
kama hawayaoni yanayofanana na hayo kwa upande wa washirika wao, Watanganyika, ili waweze kuyaangalia yaliyo
ya muungano wakiwa wameyatofautisha na ya Watanganyika.
Ni dhahiri
Wazanzibari wataendelea kuamini kwamba yanayoonekana yakiitwa ya muungano kumbe
ndiyo ya Watanganyika. Hata serikali inayoitwa ya muungano kumbe ndiyo serikali
ya Tanganyika. Hapo ndipo umuhimu wa seriakli tatu unapojitokeza kama kweli
tumedhamiria kuulinda muungano wetu.
Kwa matiki
hiyo, malalamiko ya Wazanzibari kwamba wanapunjwa sana ndani ya muungano
hayawezi kuisha, wala hayawezi kumalizwa na kilemba cha ukoka cha kwamba
Zanzibar ina serikali yake ambayo lakini inatambulika Zanzibar tu. Serikali
isiyokuwa na mahusiano ya moja kwa moja na nchi nyingine za nje kwa vile siyo
serikali kamili.
Tukumbuke
jinsi Zanzibar ilivyokataliwa kujiunga na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu, OIC,
kwa kigezo kuwa siyo nchi kamili wakati Wazanzibari kwa karibu asilimia 98
walikuwa wanakubaliana na mpango huo. Sasa inawezekanaje watu hao wakadaiwa
kwamba wana serikali yao ilhali wanashindwa kujiamualia wanayoyata wao kwa
kisingizio kwamba hawana mamlaka kamili, mpaka wapate baraka za washirika wao,
Watanganyika, kwanza?
Kwahiyo
rasmu inayotaja serikali tatu inapaswa kuchukuliwa kwamba ndio muarobaini wa
kero hizi za Muungano. Wazanzibari wanataka wakione kilicho chao na kukitambua
na iwe haki yao kukitumia kadiri ya matakwa yao yalivyo, kuliko kuendelea
kuuziwa mbuzi kwenye gunia. Vilevile wakione na kukitambua kilicho cha
washirika wao, Watanganyika. Ndipo
waelewe wanachangia nini kwenye muungano bila upande mmoja kuonekana unaupunja
upande wa pili.
Sielewi kwa
nini CCM inaona tatizo hapa! Ila ninachoweza kukichungulia na kukielewa, ingawa
kimefichwa gizani, ni kwamba CCM wanautaka muungano kwa manufaa ya chama chao,
wakati Wazanzibari wanautaka muungano kwa manufaa ya taifa lao. Swali langu
liko hivi: Je, kati ya pande hizi mbili,
CCM na Wazanzibari, ni upande upi unaoonekana kuupenda muungano kwa nia njema?
Izingatiwe
kwamba muungano ni mali ya watu iliyotengenezwa na watu kwa manufaa ya watu.
Katika muungano huu hakuna Umungu wowote uliotumika kuufanya uwepo, haya
yalikuwa matakwa ya binadamu tu, tena enzi hizo.
Uliundwa
kukidhi mahitaji ya kibinadamu ya wakati huo. Kwahiyo lolote linaweza kufanyika
katika kuuboresha ili uendelee kukidhi matakwa ya watu kwa wakati huu tulio
nao. Na katika kuuboresha tunaweza kuufanyia marekebisho ya hapa na pale bila
kulazimika kuyafuata yote ya wakati ule, wakati unaanzishwa, kwa vile sababu zilizochochea mpaka muungano
huu ukapatikana zimebadilika sana kulingana na mabadiliko ya nyakati.
Sioni sababu
ya watu kuendelea kuishi katika karaha kwa madai kwamba sababu zinazowafanya
wakarahike haziwezi kubadilishwa kwa vile zimejifunga katika muungano kana
kwamba muungano huo umeumbwa na Mungu.
Ni lazima
muungano uwepo kuwanufaisha watu, kama kuna mambo yaliyopitwa na wakati na
kuwafanya watu wauchoke basi yabadilishwe kwa lengo ya kuyaboresha iliyaende na
wakati, au yaondolewa kabisa kusudi watu waendelee kuufurahia muungano.
Vinginevyo ngalawa ivunjwe ili kila mmoja aondoke na ubao wake, kwa maana ya
kuuvunja muungano. Naamini tutakuwa hatujakufuru maana muungano huu haukuumbwa
na Mungu.
0718279346