Bukobawadau

Neno La Leo: Mugabe Ni Giza, Mandela Ni Nuru...!

Na Maggid Mjengwa
DAIMA Mzee Nelson Mandela atabaki kuwa nuru kwa Wana wa Afrika na hata watu wa dunia. Hata siku atakapotutoka duniani, basi, itakuwa kimeondoka kiwiliwili chake tu, lakini, fikra za Mandela zitabaki nasi, hivyo Mandela ataishi milelele.

Mandela atabaki kuwa nuru yenye kutuangazia na kutupa matumaini. Mwanga wake hautafifia, bali, nuru yake itaambukiza wengine, hivyo, nuru nyingine zitachomoza. Mandela ni matumaini. Ni matumaini ya uwezekano wa uwepo wa jamii yenye kuishi pamoja bila ubaguzi wa rangi, dini, kabila. Na pia, jamii isiyo na ubaguzi wa kisiasa. Mandela ametufundisha, kuwa jamii kama hiyo inawezekana kuwepo.

Lakini ona mfano wa viongozi wenye kuleta giza badala ya nuru ya matumaini; Robert Mugabe ni mfano wa viongozi hao. Tunaona , kuwa Mugabe amedhamiria kufia madarakani. Na anafanya yote kuhakikisha hilo linawezekana, bila kujali Wazimbabwe wengine.

Mugabe amevidhibiti vyombo vya habari na anawaandama wote wenye kupingana nae. Kuna Wazimbabwe waliopoteza na wanaoendelea kupoteza maisha yao kwa kupingana na Mugabe. Kuna wengi pia walioikimbia nchi yao.

Mugabe kama ilivyokuwa kwa Mobutu wa Zaire na madikteta wengine wa Afrika, naye anataka na anapenda, Wazimbabwe wamuimbe yeye. Wampigie makofi hata kwa kauli za kipumbavu. Mugabe anashindwa kuelewa, kuwa unaweza kumpeleka punda mtoni, lakini kamwe huwezi kumlazimisha kuyanywa maji. Kwamba unaweza kumlazimisha mwanadamu kukupigia makofi, lakini kamwe si kutabasamu. Hilo la mwisho hutoka moyoni.

Mara kadhaa Mugabe na kundi lake wameshiriki kuendesha chaguzi za kihuni. Kuna kila dalili, kuwa mwanzo wa mwisho wa Mugabe umefikia. Mugabe amewatumbukiza Wazimbabwe kwenye shimo refu na lenye giza nene. Hakika, Mugabe amewapeleka Wazimbabwe wengi motoni wangali bado duniani. Ndipo hapa unajiuliza busara za kutamka kuwa mtawala ni chaguo la Mungu! Hivi Mugabe nae ni chaguo la Mungu? Mobutu na Idi Amin nao walikuwa chaguo la Mungu?

Hakika, Zimbabwe ni mfano wa kutia majonzi. Nilibahatika kufika Zimbabwe kwa mara ya kwanza mwezi Desemba mwaka 1987. Ni miaka 26 iliyopita. Niliyoiona wakati huo ni nchi ilionyesha dalili zote za kunawiri kiuchumi. Niliiona Zimbabwe yenye umri wa miaka 7 tangu ipate uhuru wake. Kama ni mtoto , basi ulikuwa ni umri wa kwenda shule. Ndio, nchi ilinawiri, kwa dola moja ya Zimbabwe mfukoni niliweza kula mlo mmoja wa mchana na chenji ikabaki.

Miaka 26 iliyopita sikuishia Harare tu, nilifika mji wa Bulawayo pia katika Zimbabwe hiyo hiyo. Huko nikaona dalili hizo hizo za matumaini. Nikaenda hadi vijijini, sehemu za Mberengwa karibu na mpaka wa Msumbiji. Huko nikaona pia dalili za matumaini. Watoto walikwenda kwenye shule zenye kutoa elimu bora kuanzia ngazi ya msingi. Huduma za afya nazo zilikuwa bora. Kwa wakati huo, Mugabe na chama chake ZANU walijitahidi kuhakikisha Wazimbabwe wanapata elimu bora na huduma nyingine kama vile afya.

Miaka kumi baadae, mwaka 1997 nikafika tena Zimbabwe. Nikaanza kuona dalili za treni inayoacha njia. Niliyaona hayo Harare, Bulawayo na kule Nyanga, mbali sana na mjini. Ikawa ni tofauti kubwa na 1987. Kinachomtokea Mugabe leo ni kile alichokipanda mwenyewe lakini anaogopa mavuno yake. Watoto wale niliowaona kule kijijini Mberengwa miaka 26 iliyopita ndio "Wanaomsumbua" Mugabe sasa. Wamepata elimu bora, sasa wanayaona mapungufu pia. wanataka kushiriki siasa za nchi yao kupitia vyama vingi.

Mugabe ameshindwa kusoma alama za nyakati. Wengi wa vijana wale aliowasomesha wakaja kuwa manesi bora barani Afrika, walimu bora pia. Leo wengi wao wamekimbilia ughaibuni, Mugabe hawataki tena. Kwa Mugabe, hao "wameelimika sana!" Lakini, waliokimbia Zimbabwe nao wanawaamsha wenzao walio nyumbani, vuguvugu la kutaka mabadiliko linaendelea.

Mugabe nae anakikimbia kivuli chake. Hata kama amedhamiria kufia madarakani, kifo chake kitabaki kuwa ni cha aibu. Mugabe wa sasa anarudisha nyumba mshale wa saa ya kuelekea kwenye maendeleo ya Zimbabwe na watu wake. Huu ni wakati wa Wazimbabwe kuongeza ari ya mapambano yao dhidi ya utawala dhalimu wa Mugame na kundi lake. Ni wakati wa kufanya mabadiliko.

Na somo kubwa tunalojifunza hapa, ni namna gani mtu mmoja au kikundi cha watu kinavyoweza kuiingiza nchi shimoni kwa sababu za kifisadi. Ni imani yetu, kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho. Nuru ya Mzee wetu Mandela inatuangazia, na tunauona sasa mwanzo wa mwisho wa Mugabe. Si mwisho wa mwanzo wa Zimbabwe.

Naam, Mugabe ni giza, Mandela ni nuru.


Mungu Ibariki Afrika.
0754 678 252"
Next Post Previous Post
Bukobawadau