MILANGO YA UTUMWA WA MILELE NA MSOMAJI WETU
Supu ya kongolo ni tamu uinywe ingali ya moto. Hivyo wakati bado Taifa limejawa na furaha kubwa ya hitimisho la “Ujio wa Ulimwengu” nchini Tanzania kama alivyosema Mh. Benard Membe, nimeona ni vema nihoji mambo kadha wa kadha ili nipate kujua kama kweli Watanzania wanastahili kufurahi na hatimaye kama ilivyo ada ya waungwana tumpongeze pia Rais wetu Kikwetebila kuchelewa.
Tunao watu wanaosimanga ujio wa viongozi wa nchi zenye nguvu kiuchumi, kisiasa na kijeshi duniani kutembelea Tanzania na pia wako wanaosifia na kupongeza kwa nguvu zote ziara hizi na kuzihesabu kama mafanikio ya kidiplomasia ambayo hayajapa kutokea tangu kuumbwa kwa nchi inayoitwa Tanganyika, nchiambayo baadae iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania. Kati ya pande hizi mbili hatuwezi kupata mshindi mpaka vigezo na madhumuni ya zaira za wageni wetu yamewekwa bayana na tathmini imefanyika baada ya safari kupima ukamilifu wa malengo na mafanikio. Hivyo basi ni muhimu supu yetu iandaliwe kwa kuanza na hojaji la malengo na maksudi ya ujio wa wageni wetu.
Nitatumia rejea ya safari ya Rais wa Jamhuri ya Watu wa China Ndugu Xi Jinping na hii iliyoitimishwa leo ya Rais Barack Obama wa Marekani kupika supu yetu ya leo.
Rais Xi Jinping alifika Tanzania tarehe 24 Machi 2013. Habari zinasema lengo la ziara ilikuwa kusaini miradi mikubwa ya ushirikiano inayogusa maswala ya uchumi, ujenzi, elimu na utamaduni. Hakuna linalojulikana rasmi kwa umma zaidi ya idadi ya mikataba kumi na sita (16) iliyosainiwa ndani ya siku moja! Ila kulingana na hotuba ya Rais Kikwete iliyosomwa katika utaratibu wake wa kila mwisho wa mwezi, lengo la ziara ya Rais Xi lilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na Tanzania. Rais Kikwete anatufahamisha kwamba ziara ya Rais Xi Jinping imeitengenezea Tanzania heshima kubwa na kumbukumbu isiyosahaulika. Ndiyo, haya ndiyo mafanikio! Rais anasema hii ni kwa sababu Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kutembelewa na Rais Xi, tena siku kumi tu baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi yake. Kwa furaha iliyoje, Jakaya wetu anaona fahari kubwa kwamba mgeni akiwa juu ya ardhi ya Tanzania, huku akiufurahia ulinzi wa dola yetu, alikwea kumpita Amiri Jeshi Mkuu na kutumia Tanzania kama Jukwaa la kuitangazia dunia Sera ya China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi wake. Siyo maneno yangu, rejea hotuba ya Rais ya mwisho wa mwezi Machi, 2013!
Na leo muda mchache uliopita, Rais Kikwete kampungia mkono wa kwaheri Rais wa “Ulimwengu” baada ya kuwepo nchi kwa tafsiri ya Kimataifa iitwayo “siku mbili”. Kwa mujibu wa Balozi wa Marekani Tanzania, malengo ya ziara ya Rais Obama yalijikitakatika mambo ambayo ni malengo ya Marekani kwa Afrika na Balozi aliweka wazi mapema kabisa kwamba asingeweza kutoa taarifa za kina juu ya ziara hii, kwani mambo yote yalikuwa yanaratibiwa na Ikulu ya Marekani. Tulichobahatika kukijua wengi ni sifa lukuki tulizomwagiwa Tanzania kwa hatua kubwa tulizopigakatika nyanja za maendeleo. Haya yote yamefahamika kupitia mawasilisho katika Majadiliano ya Ubia Makini (Smart Partnership Dialogues). Pia tumeahidiwa dola million 10 na Rais Obama za kupambana na ujangiri. Na kingine ambacho kila mwenye macho ameona na mwenye masikio kasikia ni ziara ya kutakaswa kwa mitambo ya iliyokuwa Richmond baadae Dowans na sasa Symbion Power. Kama alivyofanya Rais Xi Jinping akiwa Tanzania, pia Rais Obama akiwa Ubungo—pahala palipo najisiwa na mitambo haramu, alipageuza Jukwaa la Marekani na Kuzindua Mpango wa Maendeleo ya Nishati Barani Afrika (Africa Power Initiative).
Ukiyasikiliza na kuyasoma haya malengo ya ziara hizi mbili kwa kile kilichowekwa wazi kwa umma huna budi kuipongeza serikali ya Tanzania na hasa Rais Kikwete. Utaona tumeahidiwa maziwa na asali pasipo jasho. Ukarimu ulioje Wachina na Wamerekani watafanya kazi usiku na mchana, wakatwe kodi ili misaada itolewe kuleta maendeleo kwa Watanzania? Kabla ya kutoa pongezi, kama unashughulisha akili yako hata kwa kiwango kidogo tu lazima ujiulize; Kati ya hawa wageni, Je kuna hata mmoja ambaye ujio wake kweli ilikuwa ziara ya matembezi au mapumziko ya kuja kukwea bembea kama wafanyavyo viongozi wetu? Kama kuna mikataba ya miradi ya kiuchumi imefanyika, je ni rasilimali za nanizimefunganishwa kwenye hiyo mikataba, Je, kuna rasilimali hata moja ambayo ni mali binafsi ya Ndugu Kikwete, Salma na wanawe; ambayo si ya wananchi wa Tanzania? Au je, rasilimali hiyo haikuwepo kabla katika ardhi ya Tanganyika kaileta Rais Kikwete? Ni vema kujua kwa nini watangulizi wake, akiwemo wa zama za hivi karibuni ambaye naye alikuwa mlafi hakufikia kiwewe cha sasa katika kuzifungua na kuziwekea fungani rasilimali zetu kwa pupakubwa kama hii. Huwezi kupata neno bora zaidi ya uwendawazimu kwa mtu anayeshika hili na kabla hajakamilisha anaanzisha lile na kuacha hili likiwa bado halijapata muelekeo. Serikali ya Kikwete imekuwa kama vile imeambiwa baada ya 2015, vizazi vijavyo vitaletewa Tanzania nyingine yenye rasilimali tele, na kama haiwezi kuzimaliza sasa basi zitachacha! Kwa hiyo jukumu la serikali ya awamu yao ni kutapanya na kugawa kila kilichopo sasa. Kiwewe hiki ndicho kinafanya swali la nini kipaumbele cha maendeleo kwa uchumi wa Tanzania kuwa gumu kwa watunga sera wetu. Wakilala leo na MADINI, kesho wataamka na KILIMO KWANZA, keshokutwa watakuja na ELIMU KWANZA na mtondo watasahau watakuambia NISHATI KWANZA kabla hawajaota mchana na kusema AFYA KWANZA na mtondogoo wakakueleza MIUNDOMBINU KWANZA! Kwanza inatumika katika kila jambo jipya mpaka mwishowe kimantiki inasimama kumaanisha MWISHO-KWANZA.
Naamini tungeweza kupata fair deal na Wachina kupitia ujio wa Rais Xi kuliko Wamarekani na Obama. Lakini nashawishika kuhisi kwamba Taifa lililazimishwa kuingia mikataba ya nadhiri za ufukara kufuatia kichocheo kilichokua nyuma ya shinikizo la kufunganisha rasilimali zetu (mwenye ufahamu na kumbukumbu njema ameelewa). Ndiyo maana tumelazimika kumuondoa Marmo China na kumpeleka Mwandani wa Rais wetu, asiye na sifa za Kidiplomasia na aliyezungukwa na wingu jeusi la ukwasi wa kutetemesha usio na maelezo kuwa Balozi ili kuhakikisha tunalinda chanzo cha nadhiri ya ufukara bila kelele.
Inawezekana kabisa ziara za hawa marais wawili zinayo mengi makubwa ya kujivunia labda yako njiani yanakuja. Inawezekana pia niliyoandika ni hisia na si ukweli. Lakini ili kuthibitisha na kupata uhakika, kuna njia moja tu. Nayo ni Rais Kikwete kuweka mikataba yote wazi kwa wananchi. Ninapenda afanye hivyo ili tujue mbivu na mbichi na kama tumefunga mikataba ya shinda-nishinde (win-win) basi tumpongeze na kuacha kuzikebehi ziara hizi kwa kuzifananisha na ziara za kutafuta makoloni (exploration). Hii ndiyo tiba yetu watu walalamishi, wasioona jema na wasio na shukrani. Isitoshe hiyo mikataba hajafunganisha mali za familia yake bali rasilimali za Wananchi wa Tanzania ndizo zimewekwa rehani.