SEBASTIAN KINYONYONA ENZI ZA G55 BUNGENI;Tunataka serikali tatu si kwa sababu Zanzibar ina serikali yake.
Mbunge mashuhuri kutoka Bukoba, Sebastian Kinyondo, maarufu kama Mzee Mitemba, akipenda kuvuta kiko, naye alikuwa mmoja wa wachangiaji wa mjadala kuhusu Muungano, wakati wa vuguvugu la wabunge 55, maarufu kama G55. Yafuatayo ni maelezo yake kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za Bunge (hansard), kama yalivyoandaliwa na Godfrey Dilunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki kusahihisha lolote. Na sitaki kuleta blame kwa upande wowote. Tanzania kama Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, alivyosema, tumekuwa sisi tunachumbiana, tunaowana, tunazaa na kuzaliana na wote tumechanganyika vizuri ki-sociology na kidamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Khatibu mwenyewe amekubali kunogewa na Muungano. Na kwa sababu ya kunogewa na Muungano amedhamiria kuoa na sijui ataoa Kondoa au ataoa Dodoma au Uzaramoni, ili kuleta mshikamano wa Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania hii haijawahi kupata vita kwa sababu ya Muungano wake. Hivyo sisi hatukuwa au hatutakuwa Yugoslavia ambao wamefarakana kwa mapigo ya mizinga na vifaru. Na wala hatutakubali kuvunja Muungano huu kwa talaka ya Czechoslovakia, ambayo inaitwa velvet divorce. Mnavaa kama vile wanavyovaa mabibi harusi, halafu mnapeana mkono unakuwa na Czecho – kwa upande fulani na kule Blacksliva unakuwa na Slovakia, lakini wameachana. (makofi)
Ile haikuwa Jamhuri kamili hata Adolf Hitler aliita The Republic of Bohemia. Kwa hiyo sisi Watanzania tulivyo tukubali kuendelea na Muungano wetu. Kwa sababu huko tulikotoka katika majimbo yetu ya uchaguzi hakuna hata mmoja aliyesema nenda mkavunje Muungano. (makofi)
Hoja iliyo mbele yetu ni kwamba sasa Serikali ijiandae kupata maoni ya wananchi na taasisi nyingi zinazohusika. Wawe masheikh, mapadre, vyuo, CCM, vyama vingine vya siasa, kusudi kuweza kuleta haja ya Serikali ya Tanganyikaau Serikali ya Tanganyika kuwapo ili tuwe na utatu wa Serikali.
Vinginevyo kama Serikali mbili ndizo murua zilizopo, Zanzibar na Muungano, basi hoja ingeishatolewa humu humu. Kwamba mfumo huo uendelee. Lakini mfumo ule unaweza ukashamiri tu kwa kurekebisha hali iliyopo, kwa kusema labda patakuwa na Serikali yenye Rais mmoja, lakini yenye divisioning ya utawala Zanzibar na Bara. (makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunazo Katiba mbili, ya Zanzibar na Katiba ya Union. Maana yake kuna marais wawili. Fahari wawili hawawezi kuishi zizi moja hata kidogo. Pangekuwepo fahari mmoja haina tatizo. Na mimi ningelikubali kama kuna hoja ya mtu anayotaka kuileta hapa kwamba tuwe na Serikali moja ya namna hiyo ya One Commander in Chief, One Executive President, mimi Kinyondo nitakuwa tayari kuunga mkono hoja yake hiyo.
Lakini kwa hali iliyopo, ukiwa na nyumba umezaa watoto wawili peke yake, kila mara utasikia vurugu inayopatikana, huyu kanikwaruza hivi, huyu ameiba embe, huyu amenifanya nini, kushtakiana kila mara. Lakini ukitaka kujenga ujamaa wa nyumba moja kama ulikuwa umezaa watoto wawili na Mungu kakupatia nguvu za kibailogia, zaa watoto saba. Watakwaruzana kwa uchache kulikoni watoto wawili. (makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumewahi kusikia kauli ya Rais wetu mpendwa Rais Ali Hassan Mwinyi, amesema majuzi hapa nadhani ilikuwa mwezi Julai, 1993. Akasema wakati umefika wa kufufua Jumuiya ya Afrika Mashariki. Imevunjika mwaka 1977. Na kama ungelifufua Jumuiya ile basi ni Serikali ngapi zitaingia. Una Zanzibar inaingia, kuna hii Jamhuri ya Union Tanzania inaingia, kuna Uganda inaingia, kuna Kenya inaingia. Hoja hii tulikuwa nayo mwaka 1964. Na karibu Mzee Karume na Nyerere waahirishe Union ya Tanzania ili ku-accomodate the larger Shirikisho la Afrika Mashariki.
Na tuliishaunda vyombo kuelekea kule. Tulikuwa na East African Legislative Assembly (Bunge la Afrika Mashariki) makao yake makuu yalikuwa Arusha, Spika wake alikuwa ni Mhabeshi wa Tanzania Ndugu Herman Sarwart.
Tulikuwa tunayo East African Airways, Shirika moja la Ndege, tulikuwa na Harbours za pamoja, tukiwa na Posta na Simu za pamoja, tuna Idara ya Upimaji wa Hali ya Hewa na usalama wa anga moja, tulikuwa na Customs moja, East African Examination Board, East African Currency Board moja. Lakini East African Currency ilivunjika mwaka 1965. (makofi).
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo haja ya kuwa na Serikali ya Tanganyika kuziongeza kuwa tatu ni katika kuelekea au kusaidia kuwa na One East African Community. Ikiwa Rais Daniel Arap Moi wa Kenya anakerwa na upinzani na yeye siyo Kenyatta kupinga East African Community, ikiwa Rais Yoweri Museveni, amefika wakati wa Sabasaba hapa na akasema watu wanaofanya magendo sio watu wabaya wanasawazisha masoko juu ya mipaka. Na ikiwa hata historically zote ni Pan African, mimi sioni kwa nini tupinge haya ya kuwa na Serikali ya Tanganyika ndani ya mfumo wa Union of Tanzania, kama kianzio kuelekea East African Community. Labda nitulize baadhi ya wabunge kidogo kwa kusema haikuwa haja ya mtoa hoja hiyo tarehe 23 Agosti, 1993 kuleta mikwaruzano kwa kusema malalamiko makubwa juu ya Union yametoka Bara.
Na kwamba wananchi wa Zanzibar hawalalamiki. Hiyo haikuwa hoja yetu ndani ya hoja kwamba kule Zanzibar wanakataza Watanzania Bara kushika madaraka, kwamba Wazanzibar wakileta mambo fulani mabaya, hakuna anayewakemea, kwamba watumishi wa huku hawaendi kufanya kazi kule. Na kwamba bado kuna matatizo ya pasi, fedha za kigeni, ushuru wa forodha, bandari na kadhalika, malipo ya Posta, Simu na Umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya tuliishambiwa na Serikali humu humu, kwamba yanashughulikiwa kwa dhati. Na kama yanashughulikiwa kwa dhati. Na kama yanashughulikiwa sisi kwa nini tupige kelele. Hakuna mtu ana blame Zanzibar.
Zanzibar mimi nimezoea kuwatania. Kuna Mheshimiwa Waziri mwenye masharubu kama mimi. Ninamtania hanirushii ngumi, ninamtania kama ninavyotaniwa na Jaluo. Jaluo ninamtuliza kwa kumpatia samaki aina ya kamongo anatulia hapo hapo. (kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kusema kwamba tukiwa na Serikali ya Tanganyika tutachanganyikiwa, utaanza kuvunjika Muungano, halafu tunavunjika kama Tanganyika, hii si kweli. (makofi)
Kuna wakati fulani nilikwenda Bar, ilikuwa ni wiki moja iliyopita, nikakuta watu wanazungumzia juu ya hoja yetu. Walikuwa wakisema tukiwa na Serikali ya Tanganyika, maana yake tutakuwa na vurumai. Sasa kwa nini hawa watu wanaleta hoja hizo wanajaribu kutuharibu na wale walikuwa ni maaskari, lakini vijana, wakasema heri tuanze kufukuza watu wa mipakani waende huko kwao, tutakaobakia ndiyo sisi tutaunda Muungano, kwa sababu ndiyo kiini na mimi nikatizama ni kabila gani limewahi kuwa hapa zamani kuliko watu wengine, nadhani ni Wasandawi. (makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda Kiansopolojia na Kisosholojia na kwa Akiolojia, ukienda kitaaluma ukachimba na machimbo ukatizama ni nani kaja hapa kwanza labda ni Msandawi. Sasa wale vijana askari walikuwa wamelewa, wakasema watu wa Kaskazini kule kama vile Wachaga na watu wa Tanga waende huko Kenya ndiyo kwao.
Ukienda Kusini kule kuna watu wa Ruvuma na sehemu za Mtwara, basi Wamakonde na wengine waende Msumbiji na wengine Malawi. Watu wa sehemu za Mbeya wakina Mwanakatwe na wengine wa Rukwa waende Zambia. Wahaya, Wahangaza na wengineo uwapeleke Uganda, peleka Burundi, peleka Rwanda, halafu Jaluo wa Rorya peleka Kavirondo. (kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hili si kweli hata kidogo. Ukinitizama mimi Kinyondo nilikotoka, baba yangu kazaliwa karne ya 19, anaitwa Mzee Makwaru Hamisi Rutirutungenya Kinyondo. Haya ni majina ya Tanzania yeye kazaliwa na Mzee Bishashaga Wakatano wa karne ya 19 wote wameishahama ulimwengu huu wako kwa Mungu, nadhani wana-administer to him.
Babu yangu Bishashaga aliuwawa huko Misenyi katika mapigano baina ya Wahaya na Waganda, tukateka ngome yao iliyokuwa inaitwa Kumbembe, mpaka sasa iko Chachifu na sehemu ya kwangu. Hivi mimi unipeleke Uganda kwenda kula nini. Uganda ninazungumza lugha tano za kwao. Lakini mimi ni Mtanzania kwa asili ya mama, baba na mababu. (makofi)
Kwa hiyo mtu yeyote ambaye atasema kuingiza Serikali ya Tanganyika kutaleta mfarakano by centrifugal process or by dominal theory fall, huyu haelewi mazingira tuliyonayo. (makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nizungumzie kidogo watu ambao wamekuwa na umoja lakini umesambaratika. Ukienda India kuna makabila mengi. Kuna watu tofauti kulingana na mahali walipozaliwa, wanapokaa kwa sababu za kikabila za kidini na lugha.
India Waislamu wakitaka kuwachokoza Wahindu walio wengi, basi wanachinja ng’ombe wanamtupa katika Hekalu la Wahindu, vita inazuka. Kwa sababu ng’ombe amechinjwa ni Mtakatifu wa Wahindu. Lakini Wahindu wakitaka kufanya mzaha wanakamata nguruwe wanamtupa kwenye matope, wanampeleka kwenye Msikiti, basi ndiyo utasikia; lahaulah, audhubilahi, astafirurai.
Na nchi nyingine kama vile Ubelgiji unasikia kuna makabila Laluzi, hawa ni Walatini wa asili ya Kifaransa na kuna hawa Waflemeshi ambao Tutonic or Germanic wanazungumza Kidachi na hawasikilizani, taifa la Ubelgiji karibu litasambaratika, sidhani kama Tanzania tutasambaratika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichopo tukubali kwamba Zanzibar na wenyewe wamekuwa wanalalamikia mambo ambayo ni dhahiri. Kama Tanzania hii ndani ya Muungano imehodhi mambo ambayo Zanzibar ni ya kwao, basi katika kuleta suluhu Wazanzibar wapewe wanachohitaji, ndio suluhu.
Kwa nini kuwanyima. Mimi ninakubali kwamba Zanzibar haikuteka Tanzania Bara, maana yake kuteka ni maneno ya Field Marshal Idd Amin Dadaau Field Marshal Sadam Hussein wa Baghdad, yeye akija amekuja, anapiga. Hoja ya mazungumzo baadaye. Sidhani kama Zanzibar ina uwezo ule wa kuteka. Na misingi ile sidhani Bara imetekwa kule lakini Tanganyika pia haikuimeza Zanzibar. Mambo ya kumeza ni ya kiboko ni ya chatu na ni ya mamba. Ukishaingia ndani ya tumbo umemezwa basi unasagwa na madawa yale yaliyomo ndani ya tumbo la mnyama yule, huzuki tena, huonekani wala huzungumzi. (makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaomba Waheshimiwa Wazanzibar ninaomba radhi. Ndugu yangu Nzori, Trade Unionist kama mimi, tukubali hii hoja ya Khatib, kwamba Muungano pamoja na matatizo yake, umeanza kushamiri, kwa kiasi ya yeye kutaka kuoa Kimuungano, japo Mbunge wa Rorya amemtangulia katika suala la kufungamanisha Jamhuri hii.
Lakini bado yeye ni kijana. Ndugu yangu Nzori, ukubali kwamba tunazungumza kitu cha kuleta umoja na si cha kututengamanisha. Mimi mwenyewe Ndugu Nzori wakati nimetembelea Zanzibar kwa mambo haya ya Trade Union yeye mwenyewe aliniletea sahani ya pweza. Ungeliona mdomo wangu ulivyokuwa unashughulika kumeza na kutafuna wale pweza, ungelisema huyu siyo Kinyondo ambaye anatoka over the lake Victoria. Na Mimi katika hali ya kudumisha Muungano ninakubali kumletea gunia la senene atafune kwa wakati wake. (kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningelisema mjadala huu umewezekana kufanyika kutokana na muafaka murwa tuliofikia siku ya tarehe 22 Agosti, 1993 tulipokaa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya CCM. Muafaka huo ndiyo umewezesha hata Mheshimiwa Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba kusimama hapa bungeni hiyo tarehe 23 Agosti 1993 kwa niaba ya Serikali na kuunga mkono hoja hii. (makofi)
Hivyo kama tumekuwa na muafaka wa pamoja siku ya tarehe 22 Agosti 1993 tukaimba wimbo wa umoja, vipi sasa tuanze kusikia mapigo kutoka huku na kule, tuingize mjadala mwingine ambao haulengi muafaka ule wa Jumapili. (makofi)
Baada ya muafaka kupatikana hatukuwa na nia wala sababu ya kuiwasilisha hoja hii au kusababisha ijadiliwe kwa njia ya mapambano wala malumbano. Na kwa hakika kama tulivyoelewana. Na pia kama hoja yenyewe inavyojieleza, hatupendekezi kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika kwa sababu tu eti Zanzibar inayo Serikali yake. Tunapendekeza kuwapo kwa Serikali ya Tanganyika kwa sababu ya matatizo ya muundo wa sasa wa Muungano. Hoja ni kuimarisha Muungano na hili ndiyo jambo lililotuletea muafaka katika kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja ya kuwa na Serikali tatu ndani ya Muungano uliokamilika na kwamba Serikali itatuletea rasimu ya kutekeleza jambo hilo kabla ya mwezi Aprili, 1994. lakini tukiomba Serikali ya Jamhuri ya Muungano itakayoundwa iwe na Serikali isiyotetereka. It should be nimble, meaning widely equitable and providential. Lakini yenye kuweza kudhibiti centrifugal tendencies kwa wale waliomo humo.
Hoja ya kwamba Serikali tatu zitakuwa na gharama kubwa hii ni kweli. Nadhani kitu ambacho ni cha kufanya, ni kufinyanga mfumo wa Serikali utakaokuwapo wakati ule, au kufinyanga tu zilizopo, na kuboresha muundo wa utawala uliopo kusudi unyambukie mfumo unaoendana na matakwa ya wakati huu kuondoa mikwaruzano. Na ndiyo sababu nikalinganisha na familia. Nikasema ukiwa na watoto wawili wanakwaruzana sana maana yake ni wao kwa wao.
Lakini ukiongeza hadi wakawa sita kuna kuoneana haya, kwa hiyo kudhibiti unakuwa ni rahisi. Nitaomba wakati tunaelekea katika Serikali tatu sisi wenyewe ambao tumeungana tuonyeshe nidhamu yetu. Kitabia, kimkao, kimwelekeo, kiusemi na kimazingira na kiutamaduni, tuwe wabunge au mawaziri au marais.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema kwamba yeyote atakayeleta chokochoko Serikali isisite kumwangushia blanketi la moto pale pale. Hoja hii tunaipata kwa Mheshimiwa Mtukufu Rais Ali Hassan Mwinyi kunako mwaka 1986, ameshika madaraka mwaka mmoja kidogo. Aliwaita viongozi wote wa Jamhuri, majaji, makamanda wa majeshi, mawaziri, wakuu wa mkoa, makatibu wakuu na wengine mkiwamo leaders wa secretariate.
Katika mazungumzo hayo alisema kitakachotuongoza kama dira yetu katika utendaji ndani ya Serikali na taasisi zake, kwanza itakuwa ni Katiba ya Jamhuri ambayo wote tumeamsha mkono kuapa kwa misahafu, ndani ya Bunge hili. Baada ya Katiba tutazingatia sheria za Bunge hili, Parliamentary Acts. Na tatu tutazingatia kanuni za taasisi zetu na Serikali, Standing Orders, General Orders na By Laws. Hivi tabia hii imekwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiyumba huko nyuma kwa kutokuzingatia mfumo huu. Mtukufu Rais amekuwa mtu wa kwanza, na ametoa kijitabu kinachosema kuwajibika, wewe umepewa madaraka. Wewe una uwezo, wewe una wajibu, wewe una sifa za kutosha, sasa zingatieni haya yote, ukienda nje yake utaleta matatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi huwa sikubaliani na kauli ya talaka. Kwanza mimi mwenyewe ninayo dini yangu, inaitwa Katoliki. Mkatoliki maana yake ni muumini. Yeye anafuata tu amri ili mradi Baba Mtakatifu amesema there is an assumption kwamba amewasiliana moja kwa moja na Yesu na kwa hiyo mliobaki nyinyi mlio chini ni kusujudu na kusema Amina, au mkaimba Aleluya, kwa sababu eti yeye hawezi kukosea ni Sacrosanti, akizungumza Ex-Cathedral kutoka enzi za kiti. Na katika Mkatoliki wanasema ukishakuowa au kuolewa huwezi kuchomoka kumtaliki mwenzako.
Na kwa sababu ya kauli ile, lakini mambo ya dini ninaulizia uliza. Muungano siulizi, maadam niliingia Muungano kwa hiari, na wakati ule nilikuwa ninamalizia Secondary School kunako mwaka 1964 mimi mwenyewe sitataliki Tanzania. Na ninaomba Zanzibar isitaliki Jamhuri ya Muungano na ninaomba Tanganyika isitaliki Jamhuri ya Muungano, ila tutumie hii kama msingi wa kupanuka katika spirit of Pan Africanism kuingia hata Shirikisho la Afrika Mashariki na tukawa na soko la pamoja la Afrika Mashariki, halafu tukapanuka ki-PTA na SADC, ili tuwe na muundo tunaokubalika katika umoja wa Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya, niseme nini, nikufurahi, nikumuona mwenzetu Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, amedhibiti pasipo kuyumba yumba, ametetea demokrasia hata kuliko huko nyuma. Yeye na timu yake na mawaziri, kushikamana na wabunge kuunga hoja hii pasipokutetereka haijawahi kutokea katika Jamhuri ya Muungano. Watu walioko nje, wako Bukoba, Kaliua, Mpanda, Mbambabay, even for micro second. Sasa mshikamano maana yake ni nini. Muungano sura yake si tu naiona hapa. Tuendelee hivyo na Amina Mungu atutakie neema zaidi na amwongezee Mheshimiwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, neema nyingi hapa ardhini ili kusudi tuimarishe Muungano wetu. Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja hii mkono. Ahsante sana. (makofi)
Via Raia Mwema