Bukobawadau

Sheikh amwagiwa tindikali Arusha

WAKATI hali ikiwa bado tete mkoani Arusha kutokana na tishio la uwepo vurugu za kisiasa pamoja na kundi la watu ambalo halijafahamika linalotekeleza vitendo vya kigaidi, tukio lingine lenye mwelekeo na sura ile ile limetokea tena jana.

Katika tukio la sasa, Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Arumeru, Said Makamba, amemwagiwa majimaji yanayodaiwa kuwa tindikali na kumsababishia maumivu makali usoni na kifuani.

Tukio hilo limetokea wakati wakazi wa Arusha mjini wakijiandaa kupiga kura leo, katika uchaguzi wa madiwani wa kata nne ambao tayari umeonyesha dalili mbaya, kutokana na kuibuka vitendo vyenye kuashiria kuuvuruga.

Tukio hilo, ambalo hata hivyo haijajulikana kama limetokana na masuala ya kisiasa au la, linafanana mazingira na lile la bomu lililorushwa kwenye mkutano wa kuhitimisha kampeni za Chadema Julai 15 mwaka huu, kwani yote yametokea siku moja kabla ya uchaguzi.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza Sheikh huyo alikutwa na dhahama hiyo nyumbani kwake, huko eneo la Sombetini, wakati alipotoka nje ya nyumba yake kwenda kujisaidia, ndipo ghafla akatokea mtu akiwa na kikombe chenye majimaji hayo na kummwagia usoni.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Shaban Juma Abdalah, akizungumzia tukio hilo, alisema baada ya kumwagiwa tindikali, sheikh huyo alisaidiwa na majirani kukimbizwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, alikolazwa hadi hivi sasa.

Akizungumza kwa tabu na MTANZANIA Jumapili katika Hospitali ya Mount Meru, Sheikh Saidi Makamba, alisema tukio hilo lilimkuta akiwa anatoka katika Msikiti wa Jabal Hiraa Kwa Mrombo, ambapo mara baada ya kufika nyumbani aliingia ndani na kubadilisha nguo.

“Nilipomaliza kubadilisha nguo nilitoka nje kwa ajili ya kwenda msalani, baada ya kumaliza nikiwa natoka nje ghafla nilimuona kijana mmoja akinifuata kwa kasi huku akiwa ameshika kopo mkononi na alionekana mwenye shari.

“Nikiwa sijatafakari nini kinaendelea, ghafla niliona akinimwagia maji usoni, ambapo nilianza kusikia harufu kama ya spirit au petroli hivi, lakini hapo hapo macho yangu yalishindwa kabisa kufunguka na ndipo nilipoanza kupiga kelele.

“Nikiwa nje, mke wangu alikuja na kunichukua hadi ndani, baadaye ndio wakanileta hapa hospitalini kwa ajili ya matibabu,” alisema Sheikh Makamba.

Hata hivyo, Sheikh Makamba amesema kuwa hisia zake zinamtuma kuamini kuwa watu waliofanya hivyo huenda wakawa ni wale wanaotofautiana ndani ya dini ya Kiislamu.

Sheikh Makamba aliomba msaada wa matibabu zaidi kwa mtu yeyote ambaye ataguswa kumsaidia, kwani ameumia.

Tukio hilo lilimlazimisha Sheikh wa Mkoa kuitisha kikao cha dharura jana, kuzungumzia tukio hilo ambapo walivitaka vyombo vya dola kuwasaka wahalifu waliohusika katika tukio hilo la kinyama.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alipoulizwa juu ya tukio hilo alisema kuwa bado halijamfikia na kwamba kama tayari limeripotiwa atalifanyia kazi.

Matukio ya kigaidi kama kumwagiwa watu tindikali, milipuko ya mabomu na matumizi mengine ya silaha dhidi ya viongozi wa dini na wananchi katika mikusanyiko mbalimbali sasa yanaonekana kuanza kuzoeleka nchini.
Next Post Previous Post
Bukobawadau