Bukobawadau

SIKUKUU YA MASHUJAA KAGERA

AMIRI Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, amewahakikishia Watanzania kuwa vikosi vya usalama nchini vipo tayari siku na saa yoyote, kuhakikisha amani inalindwa na havitakubali kuona nchi inamegwa na mtu yeyote.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mkoani Kagera jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa iliyofanyika katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyopo Kaboya, wilayani Muleba.
"Hatutaruhusu mtu yeyote achezee amani tuliyonayo wala kuruhusu mtu amege nchi yetu," alisema Rais Kikwete na kuongeza, "Kama tuliweza kwa Idd Amin hakuna mtu yeyote atakayechezea nchi yetu," na kuongeza;

"Wananchi laleni usingizi msisikilize maneno na vitisho nchi iko imara atakayejaribu atakiona cha mtemakuni."

Alisema jeshi lipo macho wakati wowote na atakayethubutu kutuchezea atakiona cha mtemakuni. Aliwataka wananchi wasiwe na wasiwasi wowote wala kuogopa vitisho kwani jeshi hilo lipo imara kulinda usalama wa nchi.

Alisisitiza kuwa kulinda nchi ni gharama kubwa, ndiyo maana wakati wa vita vya uvamizi wa Idd Amin wapo waliopoteza maisha, kupata ulemavu, lakini hatupo tayari kupoteza amani.

Kuhusu wanajeshi wastaafu waliopata ulemavu wakati wa vita, Rais Kikwete, alisema Serikali imekuwa ikiwahudumia na haitaacha kufanya hivyo, ingawa kuna manung'uniko katika baadhi ya maeneo.

"Tunawakumbuka na tutaendelea kuwahudumia kama kuna ambacho hakiendi vizuri niambieni ili tukae na wenzetu wa jeshi kuondoa malalamiko kwa kudhamini gharama za maisha yao waliojitoa muhanga kwa ajili ya nchi yetu," alisema Rais Kikwete na kusisitiza kwamba Serikali haitaki wasikitike.

Aliwakumbusha Watanzania sababu za Jeshi la Tanzania kupigana vita na Uganda mwaka 1978. Alisema Amin hakuheshimu mipaka iliyoachwa na Wakoloni. "Amin aliona Wakoloni wamekosea ramani kamili ya mpaka hivyo kuamini kuwa ni rahisi kwake kuonesha ubabe kwa nchi yetu,"alisema Rais Kikwete na kuongeza;
"Uongozi uliokuwepo wakati huo chini ya Mwalimu Nyerere (Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere) kila ulipomwambia aondoke alikataa na jawabu ilikuwa ni kumuondoa kwa nguvu ili kukomboa nchi, mali na wananchi wake."
Alisema baada ya kumuondoa nje tuliona ameacha amebomoa majengo yetu na kuharibu mali, hivyo na Tanzania iliamua majeshi yake yaingie Uganda yabomoe majengo ili nao wapate gharama za kujenga. "Hiyo ndiyo ilikuwa maana ya Masaka na Mbalala," alisema na kuongeza;"Baada ya kufika huko, tukaona tukimuacha ataendelea kuwa tatizo na usalama wa kudumu wa nchi hautakuwepo maana hata kwa Waganda waliokuwa wakishangilia ushindi wa majeshi yetu, Amin alianza kuwatisha kwamba watakiona baada ya majeshi ya Tanzania kuondoka."
Alisema hapo ndipo ilipotolewa amri ya saka joka popote lilipo likipatikana hata kwenye shimo likatwe shingo vinginevyo likimbie na kazi ilifanyika na hapo ndipo mashujaa wetu wengine walipoteza maisha na wengine kubaki na ulemavu.
Alisisitiza kuwa dhamira ya kulinda nchi bado ipo na atakayejaribu kumega ardhi ya Tanzania atakiona.
Next Post Previous Post
Bukobawadau