Bukobawadau

TIDO MHANDO;Uso kwa uso na Idd Amin Dada

Kwa miaka mingi Tido Mhando amekuwa akivuruga anga za redio kwa kuendesha na kutangaza vipindi mbalimbali vilivyopendwa sana nje na ndani ya Tanzania. Katika kipindi hicho kirefu, mtangazaji huyu mahiri ameweza kufanya mengi ya kusisimua. Kwenye makala zake hizi za kila Jumapili, Tido anadodosa tu baadhi ya yale ambayo labda shabiki wake hakuwa anayafahamu kumhusu. Jumapili iliyopita, aliendeleza hadithi ya safari yake ya kwanza nje ya Tanzania kwa ndege alipokwenda Uganda kutangaza mashindano ya mpira mnamo Septemba 1973. SASA ENDELEA…
Naam, tuliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Entebbe majira ya saa tatu asubuhi siku ya Alhamisi, tarehe 20 Septemba mwaka huo wa 1973, kijua cha asubuhi kikianza kuchomoza kwa chati huku mionzi yake dhaifu ikilimulika Ziwa Victoria ambalo ni miongoni mwa maziwa makubwa duniani.
Entebbe haukuwa uwanja wa kuvutia hivyo, lakini viwanja karibu vyote vya nchi hizi tatu za Afrika ya Mashariki havikuwa vyenye mvuto sana, ingawa kwa kiasi fulani, ule wa Embakasi, pale Nairobi, ulikuwa na afadhali, nilijisemea kimoyomoyo.
Kulikuwepo na watu wengi waliokuja na ndege ile ya DC – 9 ya Shirika la Ndege la Nchi za Afrika ya Mashariki (East African Airways) kutoka Nairobi asubuhi ile, wengi wakiwa wamekuja kushiriki kwenye kinyang’anyiro hicho cha mashindano ya Kombe la Challenge.
Tulijipanga kwenye mistari mirefu tayari kwa kuonyesha pasipoti zetu kwa maofisa wa Uhamiaji wa Uganda ili tuweze kuruhusiwa kuingia kwenye nchi ya Jenerali Idi Amin Dada. Moyo ulinidunda sana.
Mara zamu yangu ya kufika kwenye kidirisha cha ofisa wa Uhamiaji ikawadia, nikakitoa kile kikaratasi changu cha pasipoti ya muda kusafiria Afrika ya Mashariki. Hata sikuwa na uhakika kama kitakubaliwa maana wasafiri wengine wote walikuwa na vijitabu rasmi.
Alikuwa pande la mtu huyo ofisa muhusika, mweusi tii. Nilikuwa nimekwishawaona baadhi ya Waganda kule Dar es Salaam, na hasa wakati huo hata pale RTD ambako walikuwepo kadhaa wakifanya kazi ya utangazaji.
Serikali ya Tanzania ilikuwa imekubali kuwaruhusu wapiganaji wa Milton Obote aliyepinduliwa na Amin kutangaza propaganda zao kwa kupitia mitambo ya RTD, kama walivyokuwa wakifanya wapigania uhuru wengine wa nchi za Kiafrika zilizokuwa chini ya tawala za kibeberu.
Kwa hiyo na hawa Waganda tulikuwa tukiwasaidia katika kutayarisha vipindi vyao vilivyokuwa kwenye lugha mbalimbali za Uganda hasa ile ya Luganda. Nikapata rafiki mmoja, Emilie, aliyependa kuja ofisini kwangu kuzungumza nami kila jioni.
Yeye alikuwa mng’avu kiasi, siyo kama huyo aliyekuwa pale dirishani Entebbe. Zaidi alikuwa amejaa vizuri binti huyo wa Kiganda aliyekuwa anavutiwa na lafudhi ya Kiswahili changu cha Tanga,
Nikawa namfundisha-fundisha Kiswahili, tena kile cha bandarini, na yeye akawa ananipatia maneno mawili matatu ya Luganda na hasa baada ya kufahamu ya kwamba nitakuwa na safari hii ya kwenda kwao.
Mara kwa mara alikuwa anapenda kuniita “Ssebo”, neno la kuheshimiwa sana la Kiganda hili kwa mwanaume, maana huyu mwanadada alikuwa pia na heshima kupita kiasi, akipiga magoti ya nguvu sana kila akusalimiapo.
Kwa hiyo, pamoja na wasiwasi niliokuwa nao wa kwenda Uganda, pia nilikuwa na hamu ya kuona iwapo wanawake wote wa nchini humo walikuwa na nidhamu hii ya hali ya juu kama Emilie.
Lakini sasa tayari nimekutana hapo dirishani na pande la mtu huyu. Amekwenda juu utadhani Idi Amin mwenyewe. Nikakumbuka kwamba hawa ni Wanubi wanaotokea Arua, kule mpakani na Sudan.
Nikaona kama nakutana na Amin mwenyewe, kihoro kikaanza kunipanda tena. Halafu hali hii ya karatasi yangu; duu! Mambo yakawa yanazidi kunielemea tu. Kwa bahati nyuma yangu alikuwepo mwenzangu Mshindo Mkeyenge.
Nikamkabidhi ofisa ile pasi yangu. Akaangalia picha halafu akaniangalia na mimi, Akawa anaandika-andika kwenye kitabu alichokuwa nacho hata bila ya kuniuliza ama kuzungumza lolote.
Mara akaigonga mhuri ile karatasi na kunirudishia mwenyewe haraka hata nikadhani labda amenikatalia kuingia nchini kwao. Wakati nikiwa natafakari haraka haraka akaongeza kwa kusema kwa Kiswahili, “Karibu.” Nikafarijika.
Nikaenda mbele kidogo na halafu nikasimama kumsubiri Mshindo ambaye na yeye alikuwa anapatiwa huduma na huyu huyu jamaa ambaye mimi tayari nilikuwa namwita nduguye Idi Amin.
Nilifurahi wakati tulipotoka nje ya Uwanja wa Entebbe na kuwakuta maofisa wa Chama cha Mpira cha Tanzania (FAT), wakiwa wanasubiri kutupokea, tena wakiwa hawana ishara ya kuwa na wasiwasi wowote.
Tuliingia kwenye gari walilokuja nalo kuelekea Kampala, kilomita kama 40 hivi. Nililiona vyema sasa Ziwa Victoria. Nikawa nawaza sijui ni kwa nini ziwa kubwa kama lile lililotanda vyema kwenye nchi zetu zote za Afrika Mashariki likapewa jina la mtawala wa kikoloni.
Nikaamua kuyapuuza mawazo haya haraka-haraka na kuanza kuuangalia vyema mji wenyewe wa Entebbe. Barabara ya kwenda Kampala ilikuwa pana na nzuri, iliyoanza ikiwa na lami uchwara lakini ghafla lami hiyo ikapotea, tukajikuta kwenye barabarani ya udongo.

Tena udongo wake ulikuwa mwekundu kama ule wa kwetu Muheza. Nikajua ni kwa nini nchi hii ya Uganda inaelezwa kuwa na rutuba sana zikipatikana ndizi mshike mshike kama vile machungwa yanavyopatikana mwaka mzima kule Bonde mkoani Tanga,
Karibu njia nzima kutoka Entebbe hadi Kampala ilikuwa imejaa nyumba zilizokuwa zimeshikana, kukiwa na maeneo machache sana yaliyokuwa tupu na kwa kiasi kikubwa yakiwa ni mashamba ya migomba.
Mle ndani ya gari, wenzetu wa FAT walikuwa wanatufahamisha hali ya mipango ya mashindano yenyewe na kututhibitishia kwamba mgeni rasmi katika siku yenyewe ya ufunguzi yaani siku ya Jumamosi tarehe 22 Septemba, angekuwa ni Rais Idi Amin Dada.
Walitufahamisha mengi zaidi ikiwa nipamoja na kututaka kujihadhari sana na masuala ya usalama ikiwa ni pamoja na kutotembea-tembea ovyo, hasa wakati wa usiku.
Tuliwasili kwenye hoteli tuliyopangiwa kama saa tano hivi na baada ya kukamilisha taratibu zote na kupatiwa vyumba, Mshindo aliyekuwa mkuu wetu wa msafara alisema tupumzike hadi wakati wa chakula cha mchana ndipo tukutane tena.
Niliingia chumbani kwangu kwa tahadhari kubwa huku nikijaribu kuchunguza kila kitu mle ndani ili nijiondolee wasiwasi wowote niliokuwa nao, Ghafla nikapitiwa na usingizi.
Kushtuka simu ya chumbani ilikuwa inalia, alikuwa ni Mshindo, ambaye alikuwa amenisubiri kiasi pale mapokezi ili twende kupata chakula cha mchana. Kumbe muda ulikuwa umekwenda!
Nilinawa uso haraka-haraka, nikatoka kwenda kuungana na wenzangu. Nilimkuta Mshindo akiwa na mwandishi mwingine wa habari kutoka gazeti la Daily News, Stephen Rweikiza, ambaye alikuwa ametutangulia kwa siku moja.
Tulikwenda sehemu ya mgahawa wa karibu tu na hoteli yetu tukiwa tunazingatia ile tahadhari tuliyokuwa tumepewa na wenzetu wa FAT ya kuwa waangalifu na kujihadhari iwezekanavyo.
Wenyewe tukawa tumejiamulia pia ya kwamba labda kuwe na jambo la lazima lakini kwa kipindi chote cha mashindano hayo utaratibu wetu wa kila siku utakuwa hotelini hadi kiwanjani, kiwanjani hadi hotelini.
Pale kwenye mgahawa wa chakula sikufanikiwa kupata pilau ama wali kama nilivyozoea. Maana wale Waganda pale walituambia kwa Kiingereza kwamba hicho kilikuwa chakula cha Waswahili tu.
Basi nikaamua kuungana na wenzangu, wakiongozwa na Rweikiza, kuchagua mlo wa matoke. Mmm! Nikajisemea “wacha nile nisife”, maana mimi na ndizi hizi aina hii ya matoke ni “vitu viwili mbalimbali.”
Baadaye mchana, nilikwenda kwenye makao makuu ya Redio Uganda (Uganda Broadcasting Corporation – UBC) kuanza maandalizi ya kutangaza mechi hiyo kama tulivyotakiwa. Wenzetu pale UBC walikuwa watu wa msaada mkubwa.
Siku iliyofuata yaani siku ya Ijumaa tulitumia muda mwingi kwenye uwanja wa Nakivubo kukamilisha mipango yote mingine muhimu. Na baadaye wakati wa mchana tulikwenda kwenye hoteli iliyofikia timu ya Tanzania ili kujua hali ya timu ilivyo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau