Bukobawadau

UDINI TANZANIA: VIONGOZI A DINI ONENI HAYA.


Najua,najua kwamba hatutakubaliana wote lakini kwenye hili ni lazima ukweli usemwe na kama hakuna anayeusema ukweli basi tunabaki gizani na si rahisi kusogea na huenda hiki ndicho baadhi yenu mnachotaka, kwamba tuendelee kuwa gizani na ninyi mliopaswa kumulika mishumaa mwaiwasha huku mmeifunika vitambaa vyeusi. 

Tuwe wakweli, Tanzania inatafunwa na ugonjwa mbaya kuliko yote na huu ni ugonjwa wa ‘Udini’ na sina shaka kusema haya ni matokeo ya  matendo na hata maneno ya viongozi wa dini. Nakumbuka kipindi fulani Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliwataka viongozi wa dini wasiilaumu serikali kwa kuwapo kwa tuhuma nyingi za rushwa ndani ya taasisi zake kwa vile wala rushwa hao ni waumini wa viongozi wa dini na wako waliombeza, lakini nasema kwa hili Mheshimiwa Mizengo Pinda alisema ukweli isipokuwa tu kwa sababu wengi wa watanzania sasa hivi tunapenda kusikia maneno laini na matumaini matupu kuliko ukweli uumizao, basi alibezwa. 

Kwani ni kipi alichosema Waziri Pinda wakati huo ambacho hakikuwa na ukweli wowote?. Ebu tutafakari pamoja. Ni ukweli ulio wazi kwamba dini inayo athari kubwa ya jinsi ambavyo mtu anaishi na kuishi kunajumuisha kutekeleza majukumu yake ya kila siku akitumia elimu na vipawa vya kimaumbile aliyojaaliwa na mwenyezi Mungu. Hili si jambo la Tanzania peke yake, ni jambo linalogusa hata mataifa makubwa duniani kama Marekani  taifa lenye kujionyesha kuwa kinara wa demokrasia duniani. 

Kwenye gazeti la Los Angels Times la huko Marekani la tarehe 16/03/2007, msemaji wa mgombea urais wa wakati huo  na aliye sasa Rais wa taifa hilo Barak Obama, Bw. Robert Gibbs katika waraka wake kwa waandishi wa habari, aliwaambia wapiga kura kwa kuwahakikishia kwamba Barak Obama alikuwa Mkristo na kwamba hajawahi kuwa Muislamu. Alisema katika waraka huo kwamba “Obama siyo na wala hajawahi kuwa Muislamu” na walio wengi wakajiuliza kama ambavyo wanaendelea kujiuliza leo kwamba je, kama Obama angekuwa muislamu asingechaguliwa kuwa rais?. Je, ikiwa leo rais Obama atatangaza kubadili dini yake na kuwa muislamu basi ataondolewa madarakani? Na kadhalika na kadhalika. Jambo moja ni wazi hata hivyo, kwamba dini inao mchango mkubwa kwenye maisha ya kisiasa ya wanadamu na hatuwezi kuitenga dini na siasa. 

Binafsi naona dini na siasa kufanana kwenye maeneo mengi ikiwamo ukweli kwamba viwili hivi vinaendeshwa kwa misingi ya imani. Ndiyo. Mfuasi wa chama chochote cha siasa anaamini kwamba sera za chama chake na uongozi mzuri wa chama hicho ndiyo msingi wa maendeleo yake na  ndiyo maana anakipigia kura kimtawale. Vivyo muumini wa dini yoyote anaamini kwamba dini yake ndiyo bora kuliko ile ya mwenzake na ndiyo maana anayaacha mafundisho ya dini hiyo kutawala matendo na hata maneno yake. 

Kwa hiyo ni sahihi kusema dini ni siasa kama siasa ilivyo dini. Ni ukweli wa kihistoria kwamba kumekuwapo na tawala nyingi duniani kwa karne na miongo mingi zenye kujiendesha kwa kufuata mfumo wa kidini yaani ‘serikali za kitheokrasia’. Katika serikali hizi, huaminika kwamba Mungu (kwa tafsiri ya watu ama jamii inayoongozwa na mfumo huu) ndiye mwenye kuongoza taifa na kwamba kiongozi mkuu wa nchi ni mteule mwenye mahusiano ya hali ya juu na ya kipekee na mungu huyo na hata maelekezo yake kuhusu jinsi ya kutatua migogoro na matataizo ya jamii yake huaminika kuwa yanatoka kwa Mungu. Mifano iko mingi lakini mfano wa jinsi Mussa alivyowaongoza waisraeli kutoka mikononi mwa Farao ama Firauni kama ajulikanavyo na baadhi ya misahafu, unaweza kutuonyesha vyema jinsi dini ilivyo na siasa ndani yake. 

Lakini pia Siasa na Dini vyote hufanana kwa kuzingatia kwamba vyote huishi na kufaulu kwa kutumia nguvu ya ushawishi. Neno siasa linatafsiriwa na msomi wa kiarabu iliyo lugha yenye kuchagia maneno mengi kwenye Kiswahili kuliko lugha nyingine yoyote, Shaikh 'Alee Hassan Al-Halabee ya kwamba “ Ni kuhami na linda masuala ya umma”, neno Politics ambalo hutumiwa kumaanisha siasa kwa kiingereza linatafsiriwa kuwa ni ‘uwezo wa kuhamasisha jamii ya watu ama mtu mmoja katika kufikia malengo ya kiutawala”. Hivyo basi ni sahihi kusema kwamba dini na siasa haviwezi kutenganishwa na maisha ya kila siku ya mwanadamu kwa vile tunafanya vyote viwili kwa wakati mmoja tunapotenda majukumu yetu ya kila siku. 

Hayo hapo juu hata hivyo hayafanyi hoja ya waziri mkuu kuwataka viongozi wa dini wajitafakari wenyewe badala ya kuilaumu serikali kuwa na mashiko sana ila mantiki yake kwamba wala rushwa ni waumini wa dini hizi ndiyo hoja ya msingi. 

Viongozi wa dini ndiyo watu wenye dhamana ya kuamua muelekeo wa kidini wa watu wetu, na si hilo tu lakini kama alivyowahi pia kusema Rais wa awamu ya tatu Mh. Benjamini Mkapa kwamba maneno ya viongozi wa dini yanaaminika kuwa maneno ya Mungu miongoni mwa waumini, ni kweli kwamba sisi wengine kwa ujumla wetu tumewaachia viongozi wa dini watuongoze kuhusu masuala mazima ya kidini na bila kuwaingilia na hivyo ikiwa dini leo inageuka kuwa tatizo zito kiasi cha kutishia utaifa wetu, basi wa kulaumiwa wakiwa wa kwanza ni viongozi wa dini. 

Ndiyo, tunawalaumu wanausalama kunapokuwapo na uzagaaji wa siraha za moto na kuhatarisha usalama wa watu na hata usalama wa taifa si kwa kuwaonea bali kwa sababu kwa mwanachi wa kawaida hapa Tanzania hawezi kutofautisha hata milio ya risasi tu kutoka bunduki moja hadi nyingine kwa vile hiyo ni tasinia iliyo na wenye  taaluma, ujuzi na ufahamu nayo ambayo jamii nzima imewaamini na kuwapa jukumu siyo tu la kumiliki na kutumia siraha hizo kwa niaba yetu, bali kuhakikisha usalama wa siraha zenyewe, sasa kwanini mnataka tusiwalaumu wale waliopewa jukumu la kusimamia na kuhakiki usahihi wa mafundisho yatolewayo kwetu wakati jamii  inapohitaji miongozo ya kiimani?. 

Kuwaweka kando viongozi wa dini na kuilaumu serikali kwenye suala la udini ni sawa na kuibiwa mali kwenye ghala na kumweka kando mtunza ghala na kumlaumu muhasibu ati kwa vile tu majukumu yao yanaingiliana bila kuzingatia kwamba mtunza ghala alikabidhiwa majukumu maalumu kutunza ghala hilo hata kama muhasibu anahusika kusimamia matumizi ya rasilimali za shirika. 

Sisemi serikali haina sehemu katika madhila haya yanayoikumba jamii yetu leo, lakini nasema ikiwa kwa namna yoyote wanasiasa wametumia dini kujipatia matakwa yao ya kisiasa na hivyo kuyumbisha mfumo mzima wa jamii kwa kutojulikana mipaka kati ya dini na siasa, si kosa la wanasiasa bali la wanazuoni wetu ambao kwa makusudi ama kwa uzembe wameshindwa kusimamia misingi ya kiimani kuhusu uwajibikaji binafsi wa waumini wao kwa Mungu wao, waumini ambao ndiyo wanasiasa wanaolaumiwa.

Nasema ikiwa kiongozi anawalaumu wale anaowaongoza kwa kushindwa kutekeleza yale waliyopaswa kuyatekeleza, kiongozi huyu ameshindwa kuongoza hana budi kukaa kando awaanchie wengine waongoze. 

Yanayojitokeza leo kwenye majumba ya ibaada ni matokeo ya viongozi wa dini kujichanganya wenyewe na kushindwa kusimamia misingi ya utakatifu na heshima kwa Mungu waliyepaswa kumtumikia. Nani haoni vile ambavyo leo mimbari zimegeuka majukwaa ya kisiasa tena yakitumiwa na wanasiasa ambao wana tuhuma nzito kwenye jamii zao wakiwa wamejichafua kwenye ulingo wa siasa na kukimbilia kujiosha kwenye majumba ya dini!? 

Najua wako ambao mtasema si kazi ya viongozi wa dini kuwatenga wakosefu bali kuwapokea na kuwasaidia lakini nasema Mungu mwenyewe hatoi msamaha kwa wasiotubu na hata manabii na mitume walilifundisha hili na hakuna kati yao aliyesema unaweza kumsamehe mkosefu kimya kimya tu bali “akitubu msamehe” na mimi najiuliza hivi watuhumiwa hawa ambao  wamekataa hata kujibu tuhuma zao (japo kusema kweli si tuhuma za kisheria bali za kijamii) na kujisafisha mbele ya jamii na badala yake kukimbilia mbele ya viongozi wa dini ili wawasafishe, watazuiwa na nini kesho wapatapo nafasi kuvurunda tena na kuwataka muwasafishe kama mwanzo?.

Niseme kama alivyowahi kusema Yesu “…chumvi ikipoteza radha yake yafaa nini….” Na mimi najiuliza viongozi wa dini wanaofanya michezo hii wanajua madhara ya kukumbatia watu wenye tuhuma bila kuwawajibisha ma madhara yake?. Najiuliza itakuwaje ama mtamlaumu nani ikiwa tutafika mahala ambapo watu hasa vijana tutakataa kuja kwenye majumba yenu ya ibada kwa vile kumbe huko nako ni kunajisi kama ilivyo kwenye siasa na badala yake kuamua kubaki nje kwa vile ndani na nje kote kunanyesha na hivyo ni bora kulowa huku ukitembea maana mwisho utakuwa umesogea hatua kuliko kuloa ukiwa mahala pamoja?. 

Viongozi hawa wa dini ndiyo wanaoshadidia mafundisho yenye kusababisha mitafaruku mikubwa kwenye jamii yetu na si ajabu kwamba leo vijana wa kitanzania ni wazalendo zaidi kwa dini zao kuliko walivyo wazalendo kwa jamii yao. Si ajabu vijana wengi wa kitanzania wanaamini jamii yao ni wale wenye imani ya kidini sawa na wao na wale wenye imani tofauti si sehemu ya jamii yao na hivyo hakuna ndani ya akili za vijana hawa ile iliyojulikana miongoni mwetu kwa miaka mingi kama jamii ya Kitanzania.

Pita kwenye mahubiri na mihadhara mingi utawasikia viongozi wa dini wakiwahubiri vijana wao juu ya umuhimu wa kujitazama kwa “wao” kwa maana ya dini zao badala ya kutumia mwanya wa kuwafundisha imani ya dini ili kuitumia kutatua matatizo yao na jamii zao. Yako mabaraza mengi ya kidini nchi hii na yote yamengukia kwenye mkumbo ule ule. Si mabara ya maaskofu wala masheihk yanayochukua hatua kuwakemea wajinga wachache, natumia neno wajinga na si wapumbavu, wanaojaribu kueneza chuki miongoni mwetu na ndiyo maana kukawa na wachungaji wenye kutumia vituo vyao vya redio kutukana na kupandisha jazba waumini wa dini nyingine hadi serikali ilipoamua kuvifungia. Nauliza wakati wote wahubiri hawa wanahubiri sumu hizi ndani ya jamii yetu, mabaraza ya kidini ya dini hizi yalikuwa yakifanya kazi gani!? Kwani jukumu la mabaraza haya ni nini kama si pamoja na kuhakikisha kwamba mafunzo ya dini hizi hayapotoshwi?.
Kwani wale waliojiita masheikh waliokuwa wakiendesha mihadhara yenye kuchochea chuki na kusambaza CD za chuki hizo walikuwa kwa namna yoyote hawawajibiki kwa mabaraza ya kidini? Mbona viongozi wa mabaraza hayo wasikemee upuuzi huo hadi damu zimemwagika ndipo ati polisi inawatafuta na wao kukimbilia nje ya nchi?. Najiuliza je, viongozi wa kidini wanafurahishwa na  mafundisho haya yenye kuibomoa jamii yetu? Kwa faida ya nani!?

Ni unafiki. Ni unafiki leo viongozi wa dini kusimama na bila aibu kuilaumu serikali kwamba ndiyo inayochochea udini wakati dini ni tasnia pekee ambayo kwa miaka mingi haikuingiliwa na serikali ndani ya nchi hii hadi pale wenyewe wanaposhindwa kuendesha mambo yao na kusababisha vurugu. Ni ajabu kwamba hata inapofikia hapo bado serikali inapoingilia utawasikia viongozi hawa hawa wakilalamika kwamba serikali inaingilia uhuru wa kuabudu wakati wameshindwa kuutumia uhuru na kuufanya kuwa uendawazimu. Maana uhuru usio mipaka ni uendawazimu.
Wakati viongozi wa dini wanapojitafutia umaarufu kwenye vyombo vya habari kwa kuzungumzia masuala yasiyowahusu kana kwamba wao ndiyo wasemaji wa taasisi za umma ama kujitokeza kwenye vyombo vya habari kuzitaka taasisi za umma kujibu hoja zao na bado wakaendelea kudai wasiingiliwe uhuru wao wa kuabudu, binafsi ninaona kama wameiondoa ibada kwenye milango ya mahekalu na masinagogi na kuipeleka kwenye malango ya ikulu jambo ambalo ni kinyume na katiba na ni kuingilia uhuru wa taasisi nyingine. 

Wako ambao hadi leo wanalalamikia kauli za kiongozi mmoja wa dini ya kikristo kufuatia vurugu za Mwembechai mnamo February 13, 1998 ambapo baada ya vurugu hizo, kiongozi mmoja wa dini alijitokeza mbele ya waandishi wa habari akisema “jeshi la polisi halikutumia nguvu kubwa bila sababu na kwamba ilikuwa sahihi kutumia siraha za moto kwa sababu raia(akiwataja kwa dini yao) nao walikuwa na mawe na kwamba mawe nayo yanaweza kuua….”. Ni kauli za jinsi hii na zifanazo ambazo zimechangia kuchochea migogoro ya kidini kufikia hapa ilipo leo kwa sababu kiongozi huyu hakupaswa kwa namna yoyote kusema aliyosema hata kama yeye aliamini ni sahihi na hata kama kwa mujibu wa katiba anao uhuru wa kutoa maoni yake, lakini alipaswa kuzingatia nafasi yake na kutafakari madhara ya yeye kutoa maoni hayo maana hekima ni uwezo wa kusema neno sahihi, mahala sahihi kwa wakati sahihi na kwa namna sahihi. Ikiwa utanisalimu salamu ya asubuhi wakati wa machweo, utakuwa umefanya kitu sahihi kwamba umenisalimia, ila utakuwa umekosa hekima kwa kunisalimu salamu ya asubuhi wakati wa jioni. 

Ni wakati sasa viongozi wa dini wajichunguze na warudi nyuma kufanya mambo kadhaa waliyoyaacha. Viongozi hawa waache kukubali kuwa daraja la wanasiasa na wahakikishe kwamba wanawaunga mkono wanasiasa katika mambo ya maendeleo lakini pia wapime upepo na kutazama sifa ya mwanasiasa katika jamii na ni lazima wahakikishe kwamba wanasiasa wanajua kwamba ikiwa watajichafua kwenye utendaji wao, dini hazitakuwa mahala pa kujisafishia.
Viongozi wa dini wakemee watu wanaoibuka kila leo na kufundisha mambo yaliyo kinyume na upendo na amani na hata mshikamano wa watu wa jamii yao badala ya kuingia kwenye makundi ama kuoneana aibu ati kwa vile huyo anayekosea ni wa mlengo wa dini yangu na hivyo siwezi kumkosoa hadharani. Ni lazima viongozi wa dini wanaopotoka kutoka kwenye misingi ya kidini na kuvunja hata sheria za nchi kwa mahubiri ama mafunsidho yao wakemewe na viongozi wenzao wa dini na ikibidi hadharani ili dini zirudi kuwa mahala ambapo mizaha ya hatari haiwezi kuruhusiwa kamwe. 

Ni lazima tuache kuwashabikia watu wenye kufanya vitendo vya kipuuzi na kuumiza binadamu wenzao ati kwa kisingizio cha dini lakini pia tusiwakalie kimya na kisha kusimama tukijiosha kwamba hao ni “wahuni” maana wanachofanya hakikubaliki na dini, ni lazima tuseme hadharani mapema kwamba hawa wanachofanya hakikubaliki na tuwapinge badala ya ama kuwavisha mavazi ya heshima ama kuwakalia kimya hadi serikali inapoonyesha kukasirika ndipo ati na sisi tunaibuka na kauli za kujiosha. 

Viongozi wa dini walinde heshima ya mimbari na pia wasimame ndani ya mipaka yao badala ya kujitwalia mamlaka ya kusema kuhusu kila kitu maana miluzi mingi humpoteza mbwa na ni busara kunyamaza kuliko kusema ikiwa kusema kwenyewe ni kwenye kuchochea moto unaochoma nyumba tayari. Ikiwa bado viongozi wa dini mnataka kujiingiza kwenye siasa na kisha kuwalaumu wanasiasa mi nadhani ni wakati sasa mfike mahala muone haya kwa haya yanayotokea.
Next Post Previous Post
Bukobawadau