Bukobawadau

Ujio wa Obama, tunayofanyiwa na Wamarekani hata Mungu hayafanyi!

Na Prudence Karugendo
NIANZE  kwa kutofautiana na watu wanaodai na wengine
wakidhani kwamba ziara ya rais wa Marekani, Barack Hussein Obama, ambaye ni mtoto
wa marehemu Dk. Hussein Baraka Obama, Mjaluo na raia wa Kenya, hapa nchini
kwetu, ilikuwa ni baraka kama jina lake lilivyo, iliyojaa neema tele! Lakini
kwangu mimi na kwa mamilioni ya Watanzania wengine wasioweza kutambua na
kuelezea hisia zao, ziara hiyo ilikuwa ni karaha tupu iliyojaa manyanyaso ya
kimwili na kiakili.
Hivi ni namna
gani unavyoweza kumshawishi mtu  aliyeshinda na kulala njaa kutokana na ujio wa
mgeni kwamba mgeni huyo ni neema kwake? Ni namna gani unavyoweza kumweleza mtu
aliyemuona mgonjwa wake anakaribia kukata roho au mwingine kufa kabisa kutokana
na kukosa njia ya kupitia  kumwahisha
hospitali, kisa kuna mgeni njia zote zimefungwa, kwamba mgeni huyo ni neema
kwake?
Ziara ya
Rais Obama, ambayo mimi naichukulia zaidi kama ziara ya kifamilia, nitaeleza,
imeambatana na mambo mbalimbali ya mbwembwe, mikogo na dharau kwa wenyeji.
Mambo hayo ni pamoja na ulinzi usio wa kawaida wala usio wa lazima,
kuwanyanyapaa wenyeji na kufanyika usafi wa kufa mtu. Usafi uliowalazimisha
wenyeji nao waonekane ni sehemu ya uchafu!
Watu
wakafungiwa sehemu zao za kujitafutia riziki na kuamuriwa watoeke kabisa
wasionekane katika maeneo yao hayo kwa muda wote ambao kigogo huyo wa dunia
angekuwa nchini. Kibaya zaidi maeneo mengi ambayo yalikuwa yanatumiwa na
wananchi walalahoi kama ofisi zao za kuwaingizia mkate wa kila siku zikavunjwa
na kusombwa kama takataka vikiwemo vitendea kazi vyao.
Katika
maeneo ya Mwenge, kwa mfano, niliwashuhudia kina mamalishe wakiomboleza kama
watu waliofiwa na wapendwa wao wakati zana zao za kazi, masufuria, sahani,
vikombe, majiko ya mkaa, meza, viti nakadhalika, vikiwa vimepakiwa katika
malori, ambayo sikuelewa kama ni ya hapa au nayo yametoka Marekani. Malori hayo
yalikuwa yamelindwa na askari wa kikosi cha “kuzuia au kuleta fujo?”, wakiwa na
silaha za moto kana kwamba wako kwenye vita! Wakati huo mgambo wa jiji wakiendeleza
manyanyaso yao kwa kina mama hao walalahoi wakitamani hata kuwapora pesa zao
walizokwisha dunduliza.
Ndani ya
hali hiyo ambapo wananchi hawaelewi kama madhara na hasara walivyovipata
vitafidiwa na ujio wa Obama, unawezaje kuwashawishi kwamba ujio huo ni neema
wakuelewe kwamba wewe ni binadamu mwenzao na si shetani?
Kitu ambacho
kilikuwa kimetushtua zaidi ni kauli ya Waziri wa Mambo ya Nchi za  Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, ya kwamba watu wa mikoani waliokuwa na safari za kuja Dar wazifute
safari zao hizo na wakazi wa Dar ambao hawakuwa na shughuli maalumu katikati ya
jiji wabaki wamejifungia majumbani mwao kwa kipindi chote cha uwepo wa Obama
hapa nchini!
Kauli hiyo
ya Membe ndiyo ikachochea hisia za kwamba kumbe ziara hiyo ya Obama ilikuwa ya
kifamilia. Sababu pamoja na Membe kueleza kitu kilichojionyesha kuwa wananchi
ni kama hatakiwi kumuona Obama, ilishatangazwa tangu mwanzo kuwa rais huyo
alikuwa ameongozana na familia yake, mke na watoto. Halafu kupitia kwenye
luninga tukawaona mabinti wengine wawili, weusi, mbali na mabinti wa Obama,
Shasa na Malia, wakati wakiteremka kwenye lidege lao nyuma ya Obama na mke
wake. Lakini hatukuambiwa mabinti hao wengine ni kina nani na wana uhusiano
gani na Obama. Ndipo kubuni kukaanza kufanya kazi kuwa pengine ni watumishi wa
ndani, familia imekamilika.
Huko nyuma,
tangu enzi za Mwalimu, Tanzania tulizoea kuwapokea wageni mbalimbali kutoka
mataifa ya nje yakiwemo mataifa makubwa. Wageni hao walikuwa wakihesabika kama
wageni wa Tanzania na Watanzania kwa maana halisi.
Walipokuwa
wakifika nchini jukumu la kuwapokea, kuwakaribisha, kuwaburudisha na kuwakirimu
pamoja na kuwalinda lilikuwa ni letu sisi wenyeji.
Kutoka
uwanja wa ndege wageni hao walikuwa wakipandishwa kwenye gari la wazi wakiwa na
mwenyeji wao ili waweze kusalimiana na wananchi waliokuwa wanajipanga njia
nzima kuanzia uwanja wa ndege mpaka Ikulu. Kweli hao walikuwa ni wageni wa
Watanzania na wananchi waliliamini hilo baada ya kulihakikisha kwa njia hiyo.
Wageni hao
walikula tulichowaandalia bila kukinyanyapaa. Na katika historia ya Tanzania
hakuna mahali panapokumbusha kwamba kuna wakati mgeni aliwahi kula chakula
chetu akadhurika.
Tuliwapokea
wafalme, malikia, marais, mawaziri wakuu nakadhalika. Hawakutunyanyapaa hata
mara moja wala kudhurika na makaribisho yetu.
Hebu sasa
tuangalie ujio wa rais wa Marekani. Yeye akifika tunalazimika kumkabidhi nchi,
yeye anageuka  mwenyeji na wenyeji
tunageuka wageni ndani ya nchi yetu! Ulinzi wote anakabidhiwa yeye ili
ukafanywe na makachero wake! Walinzi wetu wanasukumwa mbali huku wengine
wakikaguliwa kama “vibaka”.
Hakuna
mwenyeji anayeaminika mbele ya Wamarekani. Hata viongozi wetu waandamizi, kama
mawaziri, wanashushwa hadhi na kuwa sawa na raia wa kawaida wa mitaani! Sisi
wenyeji tunabaki kupangiwa nini kifanyike na kwa namna gani na wababe hao wa
Kimarekani.
Kuna habari
kwamba hata mazingira yamelazimika kuonja joto ya ubabe wa Wamarekani,
yamebadilishwa katika baadhi ya maeneo ili yaendane na vionjo vya wakubwa hao.
Baadhi ya miti yetu imelazimika kukatwa kinyume na mapenzi yetu ili
ikawaondolee kiwingu Wamarekani hao. Vilevile mpangilio wa baadhi ya mambo
umelazimika kubadilika kulingana na matakwa ya muda ya Wamarekani wakati mambo
hayo hayawezi kurudi tena kwenye mfumo wake wa kawaida tunaoutaka sisi.
Lakini kwa
nini, Watanzania tunaojiona tuko huru, tukubali kuushusha hadhi utu wetu kiasi
hiki katika kuikumbatia jeuri inayotokana na mafanikio ya nchi nyingine? Hali
hii ya kuukubali udhalilishwaji wa jinsi hii kwa tamaa ya kwamba wenzetu
watatumegea sehemu ya mafanikio yao,  inautofautishaje uhuru wetu na unyonge wa
mababu zetu uliowafanya wakambebe mzungu kwenye machela ili aweze kukagua
maendeleo yao?
Obama katoa
ahadi kadhaa zinazodaiwa kwamba zimelenga katika kuyainua maisha ya Mtanzania.
Ahadi hizo zinashangiliwa hata na watu ninaowaona ni wanazuoni! Watu hao
wanazishangilia ahadi za Obama bila kujiuliza kwa nini ahadi hizo zitolewe kwa
wakati huu wakati nchi hizi mbili, Marekani na Tanzania, zimekuwepo miaka yote!
Hakuna
anayejiuliza kwa nini baada ya kugundulika kuwa Tanzania imekalia kiasi kikubwa
cha neema ndipo ikaonekana inapendeza sana machoni mwa Wamarekani kiasi cha wao
kulazimisha urafiki wa kibabe? Je, Watanzania wa sasa tutakuwa na tofauti gani
na wale wa zaidi ya  miaka  70 iliyopita walioletewa gololi za kuchezea
bao na Dk. John Williamson, mwana jiolojia wa Canada, wakamuachia mgodi wa
almasi?
Tunajiridhisha
vipi kwamba urafiki wetu huu wa kitimtimu na Wamarekani ni wa kutuinua sisi na
kutuleta karibu na wao wakati wao wakibaki palepale walipo wakitusubiri kwa
mapenzi mema?
Mwaka 2009
niliandika makala iliyokuwa ikisema kwamba “Marekani ni taifa nyamaume”. Siku
makala hiyo ilipotoka gazetini baada ya masaa mawili nikapigiwa simu na maofisa
wa ubalozi wa Marekani wakinieleza kwamba Kaimu Balozi alikuwa anaomba kukutana
na mimi. Kumbe makala hiyo ilishatafsiriwa kwa Kingereza naye akaisoma.
Nilipofika
ofisini kwake, Kaimu Balozi, akanikaribisha kwa bashasha, baadaye akaniuliza
kwa nini nakuwa na mtazamo hasi kwa nchi yao kiasi cha kuifananisha na wanyama.
Akaniuliza kwa nini niliamua kutumia neno “nyamaume”.
Ndipo
nikamweleza kwamba nyamaume ni mnyama asiyetabirika, kama simba, chui, puma au
jagwa. Yaani wanyama walao wanyama wengine. Kwamba mnyama wa aina hiyo akifanya
urafiki na mnyama kama kondoo au mbuzi usalama wa kondoo au mbuzi ni lazima uwe
mashakani. Sababu nyamaume akihisi njaa hakumbuki tena kuwa huyu ni rafiki
yangu, isipokuwa atakachoona kinafaa ni kumtumia rafiki yake huyo, mbuzi au
kondoo, kutuliza njaa yake kwa maana ya kumgeuza chakula. Nyamaume hatabiriki.
Kwahiyo
nikamwambia Kaimu Balozi kuwa hivyo ndivyo ninavyoichukulia Marekani kutokana
na matukio mbalimbali yanayotokea duniani yakilihusisha taifa lao hilo.
Ingawa Kaimu
Balozi hakukubaliana moja kwa moja na mtazamo huo, lakini kwa kiasi fulani
alionyesha kuniunga mkono. Alisema kwamba Marekani hawana rafiki wala adui wa
kudumu. Kwamba rafiki yao wa leo anaweza kuwa adui yao wa kesho. Vivyo hivyo na
kwa adui.
Akasema wao
wanaangalia maslahi na ukubwa wa tishio kwa maslahi yao. Kwahiyo kwa kiasi fulani
tukawa tumekubaliana kwamba nilikuwa sahihi, na tokea hapo tukawa marafiki.
Kwa maana
hiyo nachelea kujiunga katika kundi la watu wanaoshangilia kwamba Obama kaleta
neema Tanzania. Neema kwa ajili ya nani? Kwa ajili ya watu ambao hataki waonane
walau wampungie mkono! Watu waliokuwa na hamu ya kumuona wakidhani ni mwenzao
kwa vile ana asili ya nchi jirani ya Kenya, lakini yeye akiwachukulia kama
magaidi wasioweza kuwa salama kwake na familia yake!
Wakati
namalizia makala hii rafiki yangu mmoja, Salumu Kiyangayanga, kanitumia ujumbe
wa maandishi ukisema kwamba “njoo upewe masharti nafuu kama Tanzania wanayopewa
wakiita misaada kumbe ni mikopo itakayokuja kutumaliza bila sisi kujijua!
Huyukaelewa somo.
Lakini
hatahivyo ujio huu wa Obama, kwa vyovyote vile, gharama yake ni kubwa sana
kwetu kuliko thamani ya yote aliyoyaahidi. Sielewi mtu anaweza kukuahidi kitu
gani kilicho na thamani sawa na utu wako. Nadhani ndiyo maana hata Mwenyezi
Mungu hajitokezi mbele yetu, kwa vile anatupenda na kututhamini. Bora misaada
ya Obama, kama kweli ipo, angeitolea Washington DC  kuliko kuja huku kwetu kutuvua utu wetu.
Prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512  
Next Post Previous Post
Bukobawadau