USHAGHALABAGHALA WETU NA HATMA YAKE
Na Prudence Karugendo
KILA nchi, duniani kote, huwa na mamlaka zinazohusika na mambo kama miundombinu, mipangilio ya makazi ya watu, mipangomiji nakadhalika. Mamlaka hizo huhakikisha, pamoja na mambo mengine, makazi ya watu yanakuwa nadhifu tofauti na ya viumbe wengine wasio na akili kama tulizojaliwa nazo sisi binadamu.
Lakini tofauti na nchi nyingine, hapa nchini kwetu mambo mengi yamekuwa yakifanyika kana kwamba hakuna kitu cha aina hiyo, yaani mamlaka zinazosimamia vitu kama miundombinu, mpangilio wa makazi ya watu mijini na vijijini nkadhalika. Inavyojionesha ni kama vile watu wanajiamualia kukaa namna kila mmoja anavyotaka bila ya mpangilio maalumu unaotakiwa kupata muongozo wa kitaalamu kutoka kwenye mamlaka husika.
Hata pale ambako muongozo hauepukiki, kama katika maeneo ya mijini au kwenye vitu kama barabara na miundombinu nyingine inayopaswa kupangiliwa kiutaalamu katika kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa maisha ya watu na mali zao, bado utaalamu unaotumika unaonekana kuacha maswali mengi kwa watu.
Nataka nilitazame jambo hili la ushaghalabaghala huu unaotusumbua kwa kulitumia Jiji la Dar es salaam ambalo, bila ubishi wowote, ndilo mama ya majiji yote hapa nchini.
Nianze kwa kuangalia miundombinu, hasa barabara. Mpangilio wa barabara za jiji la Dar es salaam, ninaoamini kwamba umefanywa na wataalamu katika fani hiyo, una utata mkubwa unaojionesha wazi hata kwa mtu asiye na ujuzi wowote wa masuala ya barabara.
Daima katika mpangilio wa barabara kuna alama zinazowekwa ili kuyarahisisha matumizi ya barabara ikiwa ni pamoja na kuepusha ajali zinazoweza kujitokeza baina ya vyombo vya moto, au kati ya vyombo vya moto na vitu vingine kama wanaendesha baiskeli, wasukuma mikokoteni na hata watembea kwa miguu. Alama kama zile za pundamilia, vivuko vya treni na taa za kuongoza magari ni vitu ambavyo visipozingatiwa uwezekano wa kuepusha ajali za barabarani unageuka kitu muhali.
Lakini hata alama hizo zinapozingatiwa na watumiaji wa barabara bado unakuta utata unajitokeza katika mpangilio wake uliotumika na kuonekana kama unalazimisha wakati mwingine kujitokeza kwa kile kilichokusudiwa kuepushwa, au kuepukwa, na alama hizo, yaani ajali.
Ni kwamba katika baadhi ya maeneo vituo vya mabasi vimewekwa karibu sana na taa za kuongoza magari. Katika vituo hivyo, magari hasa daladala, yanaingia na kutoka vituoni kwa ajili ya kushusha na kupakia abiria. Wakati mwingine abiria wanakuwa wengi vituoni hasa wale wanaogombania kuingia kwenye magari, kama ilivyo kawaida ya wakazi wa Dar ambayo imejitokeza kuwa kama jadi yao.
Hivyo ni lazima pale, kituoni, pajitokeze msongamano wa magari na watu. Sasa ikizingatiwa kwamba eneo husika liko umbali mfupi toka kwenye taa za kuongoza magari, adha inayojitokeza pale sio kitu cha kufikirika tena, isipokuwa ni mauti yanayojiweka wazi.
Sababu magari yanayokuwa yanasubiri zamu ya kuruhusiwa kuondoka kwenye taa za kuongoza magari yakisharuhusiwa inabidi yawe katika kasi fulani inayoyafanya yasizidishe msongamano kwenye eneo la makutano ya barabara. Sasa mita mbili mele kuna magari yanayoingia na mengine kutoka kwenye kituo cha daladala. Kwahiyo kasi inabidi ipunguzwe au wakati mwingine magari kulazimika kusimama kabisa ili kuyapisha yanayoingia na kutoka kwenye kituo cha daladala. Wakati huo magari yaliyoruhusiwa kuondoka kwenye mataa yanakuwa bado yameziba njia inayopaswa kutumiwa na magari ya upande mwingine ambayo nayo tayari yanakuwa yameruhusiwa kuelekea kwingine.
Kinachotokea hapo ni msongamano unaoishia kwenye kukwama kwa magari yasiweze kutembea “traffic jam”. Kisa sio wingi wa magari wala ufinyu wa barabara bali ubovu wa mpangilio wa miundombinu.
Adha ya aina hiyo imekuwa ikijitokeza sana katika vituo vya Studio, Barabara ya Kawawa Kinondoni, Buguruni Sheli na Chama, Barabara ya Mandela Buguruni, External Barabara ya Mandela, Shekilango Ubungo, makutano ya Morogoro na Shekilango, Bamaga, makutano ya Ali Hassani Mwinyi na Shekilango, Mwenge, makutano ya Bagamoyo na Nujoma, Tazara, makutano ya Nyerere na Mandela, Tabata Sheli, makutano ya Mandela na Segerea na kwingineko ambako vituo vya daladala viko karibu sana na taa za kuongoza magari.
Mpangilio huo mbovu, mbali ya kusababisha adha isiyo ya lazima ya msongamano wa magari, pia wakati mwingine unasababisha ajali mbaya ambazo zingeweza kuepukika kama wataalamu wetu wa mpangilio wa miundombinu wangekuwa makini.
Ajali kadhaa zimeishatokea katika maeneo yenye taa za kuongoza magari na mbele yake kuna vituo vya daladala. Mwaka 1989 ilitokea ajali katika makutano ya Barabara ya Morogoro na Mandela iliyolihusisha gari la mizigo aina ya Fiat na Landrover, chanzo cha ajali kikiwa ni kituo cha daladala cha Minazi ambacho kwa sasa hakipo tena.
Mwaka 1991 ikatokea ajali nyingine katika makutano ya Nyerere na Mandela, vilevile ikiyahusisha magari aina ya Fiat na Landrover, chanzo cha ajali kikiwa ni kituo cha daladala cha NMC ambacho kwa sasa kinaitwa Bakresa. Miaka kama mitano iliyopita ikatokea ajali katika makutano ya Uhuru na Mandela, chanzo ni kituo cha daladala cha Buguruni Sheli. Gari la mizigo baada ya kuruhusiwa na taa likakuta daladala zinaingia na nyingine zinatoka kituoni, gari la mizigo kwa kukosa breki za haraka likayavamia mabasi madogo manne aina ya hiace na kuua watu kadhaa.
Mara kadhaa kumetokea ajali na kupoteza roho za watu katika makutano ya Mandela na Segerea kutokana na vituo vya Tabata Sheli na Tabata Reli vilivyopo mita chache kutoka kwenye mataa.
Tukiliacha hilo la mpangilio mbobu wa barabara zetu, tujaribu kuliangalia la Mipango Miji. Rafiki yangu mmoja, Daniel Njuki, raia wa Kenya, alipofika Dar kwa mara ya kwanza mwaka 2000 kwa ajili ya kutafuta mambo mbalimbali yaliyomhusu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ambayo wanaojiita marafiki wa Nyerere kule Kenya walitaka wayaonyeshe katika kumbukumbu ya kwanza ya kifo chake, alishangazwa na mambo kadhaa aliyosema kwamba katika nchi mbalimbali alizozitembelea ndani na nje ya Afrika, ameyakuta Tanzania tu.
Mambo hayo yaliyomshangaza Njuki ni pamoja na mtu kwenda dukani akaomba kitu huku anatoa pesa, mfano naomba sukari badala ya kusema lete sukari, polisi na raia kushikana mikono na kutembea huku wakipiga soga, lakini kilichomshangaza zaidi ni kuliona jiji lenye jina kubwa duniani, Dar es salaam, likiwa halina mpangilio unaoleweka!
Njuki aliniomba nimtembeze katika maeneo ya viwanda. Nikampeleka Chang’ombe, Mwenge Mikocheni, Tabata Mandela Road, na Pugu Road. Lakini kote huko tulikuta makazi ya watu pia. Akaniuliza ina maana hata haya makazi ya watu ni sehemu ya viwanda? Mimi nikajifanya bubu sababu nilijua anataka kuona viwanda, na viwanda nilimuonyesha. Lakini swali la makazi ya watu kwenye sehemu ya viwanda lilikuwa nje ya uwezo wangu wa kulijibu, nikawa nafikiria pengine nimpeleke kwa Mstahiki Meya wa Jiji labda ndiye angeweza kulijibu.
Tutaona kwamba baada ya miaka zaidi ya 50 tangu Dar es salaam ilipopewa hadhi ya kuitwa jiji, mwaka 1961, jiji hili halina ramani inayoeleweka, ukiondoa ile iliyoachwa na wakoloni, ambayo nayo tumeishaivuruga, inayoonyesha utaalamu uliotumika katika mipango miji.
Mara zote, baada ya uhuru, ramani ya jiji la Dar es salaam imekuwa ikichorwa kulingana na matakwa ya wakazi wake, si kwa matakwa ya kitaalamu. Watu wanavamia sehemu wanatengeneza makazi. Wakati mwingine serikali inakurupuka kama iliyotoka usingizini na kuamuru watu wa eneo husika wahame au wakati mwingine kuamua kuyabariki makazi hayo yasiyopimwa kitaalamu kwa kuwawekea wahusika huduma muhimu za kijamii. Kwa mtindo huo maeneo hayo yanakuwa tayari yamehalalishwa na kujiweka kwenye ramani ya jiji.
Tatizo sio kwamba wananchi wanavamia maeneo ambayo hayajatengenezwa kwa ajili ya makazi kwa vile hawayapendi yaliyopimwa na kuwekewa miundombinu, wanayataka sana, isipokuwa hayapo. Yaliyopo kidogo hayapatikani kirahisi kwa mtu wa kawaida hasa mtu akiwa mlalahoi.
Nimetembelea eneo la Kunduchi Machimbo lilipo kati ya barabara iendayo Bahari Beach na iendayo Bagamoyo, nikajionea maajabu ya eneo hilo. Kusema ukweli eneo hilo halifai kabisa kuwa makazi ya binadamu. Fikiria watu wanajenga kwenye mashimo yaliyokuwa machimbo ya udongo mgumu “sedimentary rocks” ambao kutokana na eneo la Dar es salaam kutokuwa na miamba ya mawe, udongo huo ndio unaoitwa kokoto!
Nilipoongea na wakazi wa eneo hilo la Kunduchi Machimbo, wengi wameonyesha kutoridhishwa na ukaaji wao katika eneo hilo. Ila wanasema kwamba hawana jinsi. Sababu madai yao ni kwamba serikali inapotenga eneo kidogo kwa ajili ya makazi ya watu inawalenga tu wa kipato cha juu na cha kati. Eti serikali haiwatazami hata kidogo wale wa kipato cha chini. Kwahiyo eti baada ya kudunduliza visenti vyao katika shughuli zao ndogondogo ndipo watu hao, wanaojitambulisha kama walalahoi, wanapoamua kutafuta mahali popote na kuweka vibanda vyao kusudi nao wajaribu kumiliki makazi.
Vinginevyo eti watakuwa wanauunga mkono utaratibu wa kibaguzi wa Mipango Miji unaoonekana dhahiri kuwatenga watu wa kipato cha chini ukiwa umewanyima haki ya kuwa wakazi wa jiji la Dar es salaam.
Swali muhimu hapa ni kwamba kwa nini tuwe na mamlaka zisizokuwa na mtazamo mpana? Mamlaka zisizoweza kupanga walau mambo ya miaka 20 mbele!
Tunaona kwamba idadi ya wananchi inaongezeka, miji yetu inapanuka sanjari na ongezeko la watu wanaohamia mijini, sababu ni haki ya kila raia kikatiba, kuishi mahali popote nchini anakokutaka ilmradi hajavunja sheria. Na bahati nzuri ardhi bado tunayo ya kutosha.
Kwa nini yasipimwe maeneo kwa ajili ya watu kujitengenezea makazi yanayoenda na usasa wa karne hii tuliyomo kulingana na kipato cha mtu? Kwa nini tunapendelea mambo yetu yote muda wote yaende shaghalabaghala huku tukiwa kama tunalionea fahari jambo hilo?
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512