Bukobawadau

Utukutu wa mtoto Range wamrudisha mzazi darasani


Range Jackson anaonekana kwenye banda la maonyesho la Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kwenye Viwanja vya Sabasaba , Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Anaonekana kama fundi mahiri kwa jinsi anavyofanya kazi kwa bidii. Hata hivyo, Range mwenye umri wa miaka 18 ana historia ndefu ya matatizo ya akili.
Baba yake mzazi, Jackson Range ambaye ni mfanyabiashara, ameachana na biashara na kurudi darasani kwa masomo ya ufundi.
Ni nini kimemsibu mzazi huyo hadi kurudi darasa la ukubwani?  Yeye anajibu kuwa ni kuwa karibu na mwanaye, walau apate ujuzi wa kumsaidia kimaisha.
“Nina watoto sita na huyu ni wa pili. Hata hivyo, tangu azaliwe, hajaweza kupata elimu rasmi kutokana na matatizo ya kiakili.
Niligundua tatizo lake nilipowaanzisha shule ya awali yeye na dada yake ambaye sasa amemaliza kidato cha sita,” anasema Jackson na kuongeza:
“Alikuwa na utukutu uliopita kiasi. Awali, nilidhani ni utoto, lakini baadaye niliona anashindwa kabisa kuendelea na masomo.”
Mzazi huyo anasema wakati huo walikuwa wakiishi Morogoro, aliamua kumpeleka hospitali baada ya kushauriwa na wataalamu ya afya.
“Nilishawishiwa na muuguzi mmoja kumpeleka hospitali ili apimwe, wakati huo akiwa na miaka miwili na nusu. Kule hospitalini walimpima kama kwa ‘x-ray’ kama ubongo wake unaathari  lakini hawakuona tatizo lolote, wakanipa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam ambapo alipelekwa wodi ya wagonjwa wa akili na kuanzishiwa dozi ya kutuliza akili,” anasema na kuongeza:
“Dawa alizopewa zilikuwa zinampa usingizi mzito, hivyo akawa analala na ilifika mahali akazizoea dawa, hivyo akizikosa anasumbuka.”
Anaendelea kusema kuwa alilazimika kumwona daktari bingwa anayemkumbuka kwa jina la Profesa Kilonzo (Gadi Paul) na kumwomba ambadilishie dawa.
“Profesa Kilonzo alisema kuwa hizo dawa za kumtuliza, hivyo nina hiari ya kumpa au kutompa. Kuna siku niliamua kutumia zile dawa name nikalala  kupita kiasi. Nikaamua kumwondoa hospitali na kumpeleka kijijini kwetu, Nyamongo wilayani Tarime, Mkoa wa Mara,” anasema.
Anasema walipofika kijijini kwao aliwakabidhi wazazi wake ili wamtibu kwa njia za kienyeji, ambazo nazo pia hazikufaulu.
“Baada ya wazazi kuhangaika naye, nao wakashindwa, wakaniambia tu nirudi kanisani nimwombe Mungu.
Hapo niliwaza sana, kisha nikaamua kwenda kutafuta tiba Nairobi, Kenya, hiyo ilikuwa mwaka 2001,” anasema na kuongeza:
“Nilimpeleka Kituo cha Epren Academy Ltd kilichopo Nairobi ambako alipimwa na nikaambiwa kuwa ana tatizo la utukutu uliopita kiasi na kwamba hawezi kutulia ili kusoma. Nikaambiwa kuwa tatizo hilo linaitwa kitaalamu, hyperactive and destructive disorder.
Wao walinishauri nimpeleke Hospitali ya Aga Khan huko huko Nairobi ambako nako alipimwa na kuwa matibabu.”
Baada ya matibabu hayo, Jackson anasema alimtafutia shule huko huko  Kenya, lakini Wizara ya Elimu ilimtaka awe na uthibitisho wa uraia wa Kenya, jambo ambalo lilimshinda.
“Niliporudi Dar es Salaam sikufanikiwa kupata shule inayomfaa kwani kuna Shule ya Uhuru Mchanganyiko inahudumia walemavu wa macho, wasiosikia na Shule ya Jeshi la Wokovu (Salvation Army) inahudumia walemavu wa viungo. Nikampeleka Shule ya Msingi Msimbazi, lakini walimu walishindwa kummudu kwani wakati wenzake wakiwa wapole, yeye alikuwa mtukutu,”
“Nilimpeleka Shule ya Sabasaba ambako iliwabidi kuajiri mtu wa kushinda naye, mwisho wakashindwa ndipo nikampeleka kwenye Shule ya Euris iliyoko Mbagala Zakhem, nako wakashindwa.”
Anaendelea kusimulia kuwa, mwaka 2003 kuna jirani yake anayeishi Mbagala alianzisha shule ya watoto wenye mahitaji maalumu, hivyo akamchukua Range ili amsaidie.
“Kuna siku alitoroka shule akaenda dukani na kuchanganya sukari na mchele, mwenye duka akakasirika na kumpiga na fimbo kichwani.
Anasema mtoto wake (Range) alilia kwa sauti kali, hadi jirani yake aliposikia na kwenda dukani ambako alipata mshtuko na kuanguka kwa alichokiona,” anasema Jackson na kuongeza:
“Baada ya hapo tukamwachisha shule na kuanza kumfungia ndani. Hapo nyumbani tunafuga ng’ombe, kwa hiyo alizoeana na mlisha ng’ombe wetu. Siku mlishaji huyo alipoacha kazi na kuondoka, Range alimtafuta hadi akapotea.”

Next Post Previous Post
Bukobawadau