Bukobawadau

Agizo la JK lapuuzwa Bukoba

NA MASHAKA MGETA
Balozi Kagasheki atajwa kumgomea Kikwete
Meya Amani: Hofu yake ni kupoteza ubunge 2015

Balozi Kagasheki
Agizo la Rais Jakaya Kikwete, kutaka mgogoro unaomhusisha Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani kumalizwa, limepuuzwa, NIPASHE Jumamosi limebaini.

Matokeo yake, viongozi hao wanazidi kukiweka hatarini Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho Rais Kikwete anakiongoza akiwa Mwenyekiti wa Taifa, na kukifanya kizidi kupoteza mvuto wake kwa umma wa Bukoba na mkoani Kagera kwa ujumla.

Mgogoro huo unatokana na viongozi hao wanaodaiwa kuligawa baraza la madiwani na CCM katika manispaa ya Bukoba, kutofautiana kuhusu masuala ya maendeleo yanayohusu ujenzi wa soko la kisasa, ugawaji viwanja vilivyopimwa na kituo cha mabasi.

Amani anatetea utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohusu maeneo hayo, huku akipingwa na Balozi Kagasheki anayeungwa mkono na baadhi ya madiwani wa CCM, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lakini wapo madiwani kupitia Chadema wanaotajwa kutoiunga mkono kambi ya Balozi Kagasheki, kwa kigezo kwamba, pamoja na tuhuma zilizozopo kuibuliwa na madiwani wa chama hicho (Chadema), ajenda ya kumuondoa Amani kwenye Umeya inatoka ndani ya CCM.

Mjumbe wa halmashauri ya CCM mkoani Kagera, Philibert Katabazi, alisema mgogoro huo hauna maslahi na kwamba wanaoshirikiana na madiwani wa upinzani kutaka kumng’oa Meya Amani, hawana mapenzi mema kwa chama hicho.

“Ungefanyika uchunguzi wa kina na kuchukua hatua stahili ili ukweli ubainike, lakini sasa hoja imekuwa kufanikisha nia ya kumng’oa Amani, hili halistahili kukubalika,” alisema akiwa na Diwani wa Kata ya Kahororo (CCM), Chifu Kalumuna.

Imeelezwa kuwa Amani, anatumia fursa ya kuwapo katika manispaa hiyo kwa muda mrefu kuliko Balozi Kagasheki, kujiimarisha kiutendaji na kimtandao, ili agombee ubunge wa Bukoba Mjini katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Amani alipohojiwa na gazeti hili wiki hii, alithibitisha kuwapo hofu hiyo, lakini hakueleza ikiwa ana nia ama hatarajii kuwania nafasi hiyo ambayo hivi sasa ‘inashikwa’ na Balozi Kagasheki.

KAMBI YA KAGASHEKI YAMGOMEA KIKWETE

Taarifa zinaeleza kuwa, kambi ya Balozi Kagasheki imeshindwa kukubaliana na agizo la Rais Kikwete, badala yake kuendeleza msimamo wa kumng’oa Amani.

Balozi Kagasheki alipotafutwa kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na katika ofisi ya Mbunge, jimbo la Bukoba Mjini, hakupatikana kwa madai kuwa yupo safarini Geneva nchini Uswis.

Lakini, taarifa zaidi zinadai kuwa kambi ya Balozi Kagasheki yenye madiwani nane ndani ya baraza la madiwani, ilimuandikia barua Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Shimwela Enosisye, kumtaka aitishe kikao chenye kusudio la kumng’oa Amani, ikakataliwa.

Shinikizo la madiwani hao, linadaiwa kuwa na `mkono’ wa Balozi Kagasheki, kwa kadri anavyotajwa, ingawa watu walio karibu naye wamekuwa wakiipinga hoja hiyo.

MEYA AMANI AFUNGUKA

Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, aliiambia NIPASHE Jumamosi kwamba kikwazo kikubwa katika kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huo ni Balozi Kagasheki.

Kwa mujibu wa Amani, Balozi Kagasheki, alitamka katika vikao kadhaa kikiwamo kilichoongozwa na Rais Kikwete, kwamba hayupo tayari kufanya kazi naye (Amani).

“Mimi sina tatizo katika hili lililopo na linanikera sana linapozidi kukuzwa, lakini Balozi Kagasheki hana nia hiyo na sijajua hofu yake ipo wapi, ingawa ninasikia inatokana na ubunge kwa mwaka 2015,” alisema.

Amani alisema miongoni mwa vikao ambavyo Balozi Kagasheki ‘aliapa’ kutoshirikiana naye ni mkutano alioutisha Novemba 24, mwaka jana ambapo alitumia dakika 55 kati ya 72 alizozitumia kuhutubia, akimtukana (Amani).

Pia Amani alidai kuwa, Desemba 18, mwaka jana katika kikao cha halmashauri ya CCM wilaya ya Bukoba Mjini na kikao kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, Januari 23, mwaka huu, Balozi Kagasheki ‘aliapa’ kutoshirikiana naye.

Kuhusu kutilimuwa madarakani, Amani alisema bado anautumikia umma kupitia nafasi yake na kwamba hadi alipokuwa akihojiwa na gazeti hili, alikuwa katika maonyesho ya Nanenane ambayo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa Viktoria, yalifanyika jijini Mwanza.

MKURUGENZI MTENDAJI ANENA

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba, Shimwela Enosisye, alipowasiliana na gazeti hili, alisema si muda muafaka kuzungumzia suala hilo kwa vile ni moja ya maagizo mengi yaliyotolewa na Rais Kikwete.

“Hilo ni agizo moja tu, ingawa yote yalielekezwa kwa Mkuu wa Mkoa, Kanali mstaafu Fabian Massawe, lakini jambo la msingi hapa ni kufuata sheria na taratibu, muda ukifika tutalitolea taarifa,” alisema.

Enosisye, aliyesema ana uzoefu wa nafasi hiyo kwa miaka mingi, alisema hatua ya kutoa taarifa ‘fupi fupi’ inayohusu utekelezaji wa maagizo ya Rais Kikwete, inaweza kuchochea upotoshaji kwa umma.
Hata hivyo, Enosisye alisema baadhi ya mambo anayoyasikia kupitia vyombo vya habari, hayana ukweli wowote
CHANZO: NIPASHE
Next Post Previous Post
Bukobawadau