BUNDUKI ,RISASI VYAKAMATWA - KAGER
|
JESHI la Polisi mkoani Kagera limekamata bunduki mbili zinazotuhumiwa kutumika katika matukio ya ujambazi, likiwemo la utekaji na ujangili pamoja na risasi 78 zinazotumika katika bunduki aina ya SMG/SAR.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Philip Kalangi, alisema kuwa silaha hizo zimepatikana kutokana na msako unaoendeshwa na jeshi hilo katika wilaya zote za mkoa huu.
Alisema mnamo Agosti 11 mwaka huu saa 4:25 usiku katika kijiji cha Sasa Maharage, Kata ya Lusahunga, wilayani Biharamulo polisi waliweka mtego na kufanikiwa kumkamata Kazuba Misigwa (41) ambaye alikuwa akimiliki SMG yenye namba KO 17753 aliyokuwa ameificha katika shimo pamoja na risasi 78 na magazine tatu tupu nje ya nyumba yake.
Alisema mtuhumiwa huyo alimtaja mwenzake aitwaye, Alex Emmanuel (35) mkazi wa Kitongoji chaNyangamagulu eneo la Nyakahula Mizani, wilayani Biharamulo ambaye pia alikamatwa na kukiri na kuonesha silaha aina ya gobole iliyotengenezwa kienyeji.
Watuhumiwa hao wanadaiwa kukiri kuzitumia katika matukio mbalimbali ya uhalifu na ujangili yaliyokuwa yakitokea katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu na mikoa mingine.