CCM kama kobe, gamba lake ndio uhai wake
Na Prudence Karugendi
MOJA ya makosa ya kibinadamu aliyoyafanya Rais Kikwete, kiuongozi na kimwongozo, ni kauli yake ya kwamba chama chake ambacho yeye ndiye mwenyekiti kwa sasa, Chama Cha Mapinduzi, ni lazima kijivue gamba ili kiwe na mwonekano mpya ambao ungeweza kukirudishia mvuto kwa wananchi ambao kimeupoteza. Nasema hilo ni kosa la kibinadamu sababu Mwenyekiti Kikwete alipaswa kuelewa kwamba gamba linalokifanya chama chake kikose mvuto kwa wananchi ndilo limeushikilia uhai wa chama hicho kwa sasa. Kama ambavyo huwezi kumvua kobe gamba lake akabaki mzima ndivyo ilivyo hata kwa Chama Cha Mapinduzi.
Matokeo ya kauli hiyo ya mwenyekiti wa CCM aliyoitoa kimakosa ni hizi kebehi zilizoiandama kauli hiyo toka kwa baadhi ya makada wa chama hicho zinazotishia hata nafasi ya mwenyekiti na kumfanya Mwenyekiti Kikwete akose kujiamini na hivyo kulazimika kuitetea kauli yake hiyo kwamba ilitafsiriwa vibaya.
Kikwete angewahi kulikumbuka hilo angekuwa makini na kujaribu kutafuta vizuri maneno ya kuyatumia katika kufikisha ujumbe wake kwa wanachama wake na wananchi kwa ujumla akiwa ameepuka fadhaa inayomwandama kwa sasa. Hiyo ni kwa sababu kauli kama ile ya Andrea Chenge ya kwamba gamba limekwamia kiunoni na mwenye uhakika wa kulitoa kabisa ni lazima aje na shoka, ambayo bilashaka ililenga kumfadhaisha mwenyekiti wake na kumfanya ajione dhalili mbele ya wananchama wake, ingeweza kuepukwa.
Kupitia kwa kauli ya Chenge tunaweza kuona kwamba mwenyekiti wa CCM alitamka kitu ambacho hawezi kabisa kukitekeleza. Hiyo ni dosari kubwa kwa chama ambacho ndicho chenye dhamana ya kuiongoza nchi. Sababu iwapo chama kinashindwa kutekeleza maazimio yake chenyewe kama hilo la kujivua gamba, huku baadhi ya makada wake wakitoa kebehi kwa kujiamini kabisa kuwa hilo haliwezekani, wananchi wengine wasiokuwa wananchama wa chama hicho wanawezaje kuwa na imani kwa chama hicho tawala kuwa kinaweza kuyatekeleza maazimio ya ki nchi iwapo yale ya kichama yanakishinda?
Wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi, kwenye uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza, Februari 5 mwaka huu, mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, alijaribu kuonyesha kwamba kauli yake ya kujivua gamba aliyoitoa mwaka mmoja uliokuwa umetangulia kule Dodoma, kwenye maadhimisho kama hayo ya mwaka jana, ilitafsiriwa vibaya. Lakini hiyo ni baada ya kubanwa na kuonekana kwamba alichokitamka kule Dodoma hakitekelezeki. La sivyo kwa nini asubiri mwaka mmoja upite ndipo agundue kwamba kauli yake ilitafsiriwa vibaya? Na kwa mwenendo huo tutarajie nini katika maadhimisho ya mwaka kesho? Hayo ndiyo maswali yanayowasumbua wananchi kila wanapoifikiria tarehe 5 Februari.
Tukirudi nyuma tutaona kwamba wakati chama tawala kilipokuwa hakijaota gamba, kuanzia enzi za TANU na baadaye CCM ya mwanzoni, maazimio ya chama au hata fikra za mwenyekiti vilikuwa vikitekelezwa bila kuyumbayumba wala kuoneana haya.
Mfano mmojawapo ni wa Azimio la Arusha. Hilo lilikuwa ni azimio la chama, TANU, kwa wakati huo. Ni azimio ambalo katika hali ya sasa lisingeweza kutekelezwa kutokana na maudhui ya azimio hilo kuonekana yanalenga moja kwa moja kuwaathiri waliojigeuza gamba linaloulinda uhai wa chama.
Ikumbukwe kwamba gamba katika CCM lilipata Baraka za chama pale viongozi wa chama hicho walipokaa Zanzibar na kuamua kuliengua Azimio la Arusha katika azimio la kimya kimya lililokuja kujulikana baadaye kama Azimio la Zanzibar mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Kama yupo anayepingana na maoni yangu haya atueleze kilichomfanya Rostam Aziz, aliyekuwa mbunge wa Igunga, ajiuzulu ubunge na nyadhifa zote ndani ya CCM kutokana na kile alichokiita kuchoshwa na siasa uchwara ndani ya chama chake.
Hiyo ilikuwa baada ya Rostam Aziz kusakamwa sana kuwa yeye ni gamba ndani ya CCM linalokichafua chama. Lakini ajabu baadaya Rostam kujiuzulu CCM haikushangilia kwamba gamba limeondoka wala kuilaani kauli ya Rostam ya kwamba CCM inaendesha siasa uchwara! Ila badala yake CCM ikamwendea Rostam, gamba chafu, kumlamba miguu ili akubali kuifanyia kampeni Igunga huku chama hicho kikimpiga marufuku Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kukanyaga Igunga ili asije akaharibu mpango ambao chama kiliutegemea kwa wakati huo uliokuwa ukiwezeshwa na Rostam Gamba ili kiweze kupata ushindi. Mpaka hapo nani hawezi kuona kipi ni kipi?
Kwa mtazamo wa haraka na mwepesi tunaweza kuona kwamba gamba la CCM ni sawa na jinni walilolinunua wenyewe kwa tamaa zao. Na wataalamu wa masuala ya majini wanaeleza kwamba kulileta jini, tuseme kulifuga, ni rahisi lakini kuliondoa ni kazi ngumu sana. Hata pale jini linapokuwa limeanza kuleta madhara inabidi kulinyenyekea tu.
Hayo ndiyo yanayojitokeza kwa Chama Cha Mapinduzi kwa sasa. Gamba lililooteshwa kwa mbwembwe huku maadili ya chama yakiwa yamepigwa kisogo, limegeuka balaa na kushindikana kuvuliwa likitishia kuvuka na uhai wa chama baada ya kukifanya chama hicho kukosa mvuto kwa wananchi.
Kadiri nilivyomuelewa mwenyekiti Kikwete, Februari 5, mwaka jana, ni kwamba chama hicho kilitakiwa kujivua gamba ambalo kwa sasa linaonekana ni uchafu unaokinyima chama hicho mvuto. Lakini ilisahaulika kwamba pamoja na uchafu wake gamba hilo ndilo lililokabidhiwa jukumu la kuulinda uhai wa CCM pale chama hicho kilipojiengua kwa wananchi walio wengi, wakulima na wafanyakazi, na kujibakisha kwa watu wachache wenye kuonekana wana nguvu za kiuchumi hata bila kujali kama nguvu hizo ni za halali au haramu.
Leo hii chama hicho kinataka kujirudishia mvuto wake wa tangu zamani, baada ya kujigundua kwamba kimechafuliwa na gamba lakini gamba linashindikana kuvuliwa na kukwamia kiunoni! Jini kulileta ni kazi rahisi lakini kuliondoa ni kasheshe.
Madhara ya gamba ndani ya mfumo wa chama tawala ni pamoja na kuvuruga mfumo mzima wa uwajibikaji ndani ya chama. Pale ambapo wanachama walikuwa wanajitolea kiuzalendo kwa moyo uliokolezwa na itikadi ya chama kukitumikia chama pamoja na nchi kwa ujumla sasa hivi pamechukuliwa na tunaoweza kuwaita wawekezaji ndani ya CCM. Hawa wanaonekana kama wawekezaji kutokana na kuyaangalia maslahi tu bila kuonyesha dalili zozote za uzalendo kwa chama na kwa nchi. Kinachoangaliwa ni wamewekeza nini katika chama na watapata nini kama faida. Katika hali kama hiyo itikadi ya chama ni lazima itabaki kuimbwa tu kama wimbo wa promosheni ili kuwavutia wateja.
Hilo tunaweza tukalihakikisha kupitia katika marekebisho yaliyopendekezwa kufanyika katika katiba ya CCM. Katika marekebisho hayo wanachama walio na utumishi wa kudumu kwa tiketi ya chama hicho wanatakiwa wasiwe na nafasi nyingine ya utumishi ndani ya chama hicho.
Kwa mtazamo wangu mabadiliko hayo yanalenga kutoa nafasi pana kwa wanachama wengi kuweza kukitumikia chama chao na kuondoa ukiritimba wa kulimbikiza majukumu mengi ya kichama kwa mtu mmoja ilhali chama kinao mamilioni ya wanachama.
Mabadiliko hayo ya katiba ya CCM yanawataka wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kupatikana wilayani badala ya mkoani. Wabunge kupitia chama hicho wanazuiwa kugombea nafasi hizo za ujumbe wa NEC kwa vile tayari wanazo nafasi za utumishi ndani ya chama hicho, ubunge, ambao ni kazi ya muda wote.
Lakini kama nilivyoonyesha kwamba gamba limepunguza uzalendo, kama sio kuupoteza kabisa, ndani ya chama hicho tawala, wabunge kupitia chama hicho walikuwa wanayapinga mabadiliko hayo kwa nguvu zao zote kiasi cha kumtaka hata mwenyekiti wao naye achague moja kati ya mawili, kubaki na urais na kuuachia uenyekiti kama angeyaridhia mabadiliko hayo yanayowazuia wao kugombea u-NEC, ujumbe wa Halmashauri Kuu ya chama chao.
Mzozo huo unatuonyesha nini? Angalia, mtu tayari kakiomba chama chake kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya ubunge, chama chake kikamkubalia. Amekuwa mbunge, anawatumikia wananchi kwa kuwawakilisha bungeni. Lakini mtu huyohuyo bado anatamani awe mjumbe wa NEC ya chama na pengine CC ya chama kilekile. Na wakati mwingine awe katibu wa chama wa mkoa au wilaya! Mtu huyohuyo mmoja! Je, huo ni ukada kweli? Hatuwezi kuona kuwa mtu wa aina hiyo anajali zaidi uwekezaji ndani ya chama kuliko ukada wa chama?
Ingawa sipingi wazo la kutenganisha kofia ya uenyekiti wa chama tawala na urais, njia iliyotaka kutumiwa na wabunge wa CCM kumtaka mwenyekiti wao naye aachie nafasi moja sikubaliani nayo, sababu ilionekana kama ya kutaka kulipiza kisasi kutokana na wao kupunguziwa kinachoonekana kama ulaji kwa njia ya uwekezaji ndani ya chama. Hiyo ni njia inayodhihirisha utovu wa uzalendo ndani ya chama unaoenea na kugeuka utovu wa uzalendo kwa nchi. Ni kama madai yaliyopo kwa sasa kuwa tunaye waziri ambaye pia ni raia wa Marekani!
Athari za tabia hiyo ya kukosa uzalendo kwa chama na baadaye kwa nchi ni kama tulivyoona wakati wa sakata la ongezeko la posho za vikao vya bunge lililokuwa sambamba na mgomo wa madaktari nchini. Badala ya wabunge wa CCM kuwasemea madaktari ili waongezewe posho ili nao waweze kufanya kazi zao kwa umakini na kuyanusuru maisha ya watanzania wao wanalilia kulipwa posho za vikao vya bunge kwa shilingi laki mbili kila wanapoingia bungeni hata kama wanachokifanya humo ni kuzomeazomea na kupitisha mambo kiubabe kwa kutegemea wingi wao wakidhani wanawakomoa wabunge wenzao wa upinzani walio wachache.
Hata kama baadaye walikuja kuuona unyeti wa suala la mgomo wa madaktari na kuamua kuingilia kati lakini tayari roho nyingi za Watanzania zilishapotea na haziwezi kupatikana tena. Hiyo yote ni kwa sababu waliopaswa kuyaona hayo yote, wawakilishi wa wananchi, waliamua kuziwakilisha nafsi zao badala ya kuwawakilisha wapiga kura wao. Ndipo wakaona kuwa maisha yamepanda kwao, wabunge, na hivyo kutaka walipwe shilingi laki mbili kila wakitia mguu mjengoni bila kujali kama gharama za maisha zilikuwa zimepanda vilevile kwa madaktari waliokuwa wanataka walipwe walau shilingi elfu kumi kila wakiingia wodini katika muda wa ziada.
Tabia hiyo ya wabunge wa CCM ya kujiangalia wao peke yao bila ya kuwajali wanaowawakilisha hatuwezi kusema inatokana na kujisahau, sababu hiyo ni tabia inayoonekana kujengeka kuanzia kwenye chama chao, chama kilichoota gamba baada ya kuyapoteza maadili yote kiliyoanza nayo. Chama ambacho uanachama wake ulikuwa unasomewa kabla ya mtu kupewa kadi na kufikia kuwa chama ambacho uanachama wake unapatikana mahali popote na kutolewa na mtu yeyote pasipo kuangaliwa ana wadhifa gani ndani ya chama!
Kutokana na hali hiyo ni wazi kwamba Chama Cha Mapinduzi kiko njia panda, hakijui kiifuate njia ipi. Wananchi ni lazima kinawahitaji ili kionekane ni chama kinachoongoza nchi kwa ridhaa yao, lakini vilevile gamba lake kinalihitaji zaidi kwa vile ndilo linalokilindia uhai wake. Kwahiyo tusimshangae mwenyekiti wake pale anapotoa kauli mbili zinazokinzana katika shughuli ya aina moja, “tutajivua gamba” mara “nilitafsiriwa vibaya sikumaanisha kujivua gamba”. Ni kwamba Mwenyekiti wa CCM yuko njia panda, haelewi aifuate njia ipi kwa vile zote mbili ni njia mhimu kwake na kwa chama chake.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512