Bukobawadau

KAMATI KUU YAKUTANA NA KINA KAGASHEKI JANA AGOSTI 25,2013

Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete akiongoza kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM, Makao Makuu ya CCM, mjini Dodoma jana, Agosti 25, 2013. Kikao hicho kilifanyika kwa ajili ya kukutana Mbunge wa Bukoba mjini Khamis Kagasheki, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera, Constansia Buhiye,  Katibu wa CCM mkoa wa Kagera Abedi Mushi, Mwenyekiti na Katibu wa CCM wilaya ya Bukoba mjini na Meya wa Manispaa ya Bukoba Anatory Amani  kuhusu sakata la madiwani wa wanane wa CCM katika Manispaa ya Bukoba mjini. Kulia ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
 Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera Constansia Muhiye na Katibu wa CCM wa mkoa huo, Abedi Mushi wakisubiri kuingia ukumbini kukutana na Kamati kuu mjini Dodoma leo.
 Mbunge wa Bukoba mjini Khamis Kagasheki akiwasili Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma.
Balozi Kagasheki akiperuzi mtandao wakati akaisubiri kukutana na Kamati Kuu mjini Dodoma jana.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya vikao vya Kamati Kuu zimesema kwamba viongozi kadhaa wa chama hicho akiwamo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamisi Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani wameonywa kutokana na mgogoro wa muda mrefu katika wilaya hiyo.
Wengine waliotakiwa kupewa karipio ni pamoja na  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye na Katibu wake, Averin Mushi ambao walitarajiwa kuhojiwa jana usiku.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo vinavyofanyika Mjini Dodoma zilisema hata ule uamuzi wa kuwazuia Amani na Kagasheki kufanya siasa umeonekana unaweza kuleta athari kwao na kwa chama chenyewe, hivyo kuamua kutoa onyo na madiwani waliokuwa wamefukuzwa uanachama kuachwa kuendelea na nyadhifa zao. Vyanzo hivyo vya habari vilieleza kuwa suala hilo lilikuwa tayari limeamuliwa, isipokuwa ilikuwa ni lazima wahusika waitwe kufahamishwa uamuzi dhidi yao badala ya kusikia kwenye vyombo vya habari.
Hata hivyo, hadi jana wakati tunakwenda mitamboni ni viongozi wawili tu, waliokuwa wamehojiwa na Kamati Kuu ambao ni Buhiye na Mushi kwa kuwa tayari walikuwapo Dodoma wakiwa ni wajumbe wa Halmashauri Kuu.
Balozi Kagasheki na Amani licha ya kwamba walikuwa wamewasili hapa, suala lao liliahirishwa kutangazwa kuwasubiri Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Yussuf Ngaiza na Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Janeth Kayanda waliochelewa kufika mjini hapa baada ya gari lao kuharibika.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema uamuzi wa Kamati Kuu ungetolewa baada ya kumalizika kwa hatua ya kuwahoji viongozi hao jana.
Mgogoro wa Manispaa hiyo unatokana na miradi iliyopangwa na Meya Amani, ambayo inapingwa na baadhi ya madiwani wa CCM wa Manispaa akiwamo Balozi Kagasheki, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii.
Hali ya siasa mkoani humo ilichafuka zaidi baada ya  Halmashauri ya CCM ya Mkoa wa Kagera kuwafukuza madiwani wanane kwa kosa la kumpinga Meya huyo na kupanga kumng’oa madarakani.
Madiwani hao ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Ngaiza(Kashai).
Hata hivyo, uamuzi huo wa kuwafukuzwa ulisimamishwa na Sekretarieti ya CCM ambayo ilisema kuwa Kamati Kuu ndiyo iliyokuwa na madaraka ya kutoa uamuzi wa mwisho dhidi yao na kuwataka kuendelea na kazi wakisubiri hatima yao.
Katika hatua nyingine, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), ambacho kilikuwa kimalizike jana kimeongezewa siku moja zaidi na kitafungwa rasmi leo.
CHANZO; GAZETI LA MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau