Bukobawadau

Mnyauko wa migomba wainyausha Kagera

NaJanet Josiah
UGONJWA wa ‘mnyauko’ unaowakabili wakazi wa mkoa wa Kagera sasa umekuwa kilio kikubwa na kila anayefika mkoani humo hupokewa na kilio hicho.
Makaribisho ya wageni na wenyeji miaka ya nyuma ilikuwa ni chakula cha ndizi lakini sasa ni nadra kupata makaribisho ya aina hiyo.
Mnyauko umesababisha kilio kitokanacho na njaa, maisha ya wananchi sasa ni ya kutangatanga yasiyo na uhakika wa chakula wala fedha walizokuwa wakizipata kutokana na mauzo ya bidhaa hizo.
Ugonjwa huo ni msiba wa mkoa Kagera kwa kuwa umezikumba kaya nyingi zinazolazimika kufyeka migomba iliyoathiriwa na kupanda upya.
Sasa ni miaka saba tangu uingie nchini mwaka 2006; wakazi wa Kagera walianza kuuona ugonjwa huo unaoaminika ulitokea nchini Uganda.
Wakazi wa mkoa huo (Wahaya), sasa wamelazimika kubadili utamaduni wa chakula kikuu ambacho ni ndizi; sasa wanalazimika kula vyakula vingine vilivyokuwa havilimwi wala kupewa kipaumbele.
Mhaya asipokula ndizi hana furaha, hawezi kujinasibu kala chakula lakini sasa analazimika kukubaliana na mabadiliko ya mazingira.
Wakulima wengi katika mkoa huo wamefyeka na kupanda upya migomba kwenye mashamba yao yaliyoathiriwa na mnyauko.
Licha ya mnyauko kuwatesa wakulima wa Kagera, serikali haionekani kuuvalia njuga ugonjwa huu ili kuutokomeza kama inavyofanya kwa magonjwa ya binadamu.
Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa na wakulima ni kutokuwapo kwa watafiti na wataalamu wa kutosha kuwaelimisha wakulima njia bora za kinga, tiba na tahadhari.
Novath Paulo mkulima wa kata ya Kamuli, anasema tangu ugonjwa huo uingie mwaka 2007 mpaka sasa, walipatiwa mafunzo mara moja ambayo yalitolewa na wataalamu kutoka Maruku, Bukoba.
Paulo anasema walifika na kuweka kambi kwa Mzee Vudasto Mutachoka ambaye ndiye mkulima wa kwanza kuvamiwa na ugonjwa wa mnyauko wa migomba.
Anasema wataalamu hao waliwaeleza namna ugonjwa huo ulivyo na kwamba wajitahidi kukagua mashamba yao kila siku na pale watakapoona mgomba umeathirika wauondoe haraka kwa kuuchimba na kuukatakata.
Naye Geofrey Kato Mkazi wa Bugene anasema maelezo kuhusu ugonjwa huo na namna ya kupambana nao walipatiwa na ofisa mtendaji  wa kata yao na si mtaalamu.
Kato anasema tangu siku hiyo, hawajawahi kupatiwa mafunzo ama maelekezo yoyote toka kwa wataalamu wa kilimo.
Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa halmashauri hiyo haina wataalamu wa kutosha huku mahitaji yakiwa ni wafanyakazi 10 na zaidi kulingana na ukubwa wa wilaya hiyo.
Pamoja na ufinyu wa wataalamu katika halmashauri hiyo yenye kata 40 ina maofisa ugani kilimo 16, huku vijiji 116 vikiwa na wataalamu wasiozidi 50.
Ufinyu huo ndiyo umesababisha wakulima wengine wakose elimu ya kupambana na ugonjwa huo kwa kuwa hakuna wanalolijua.
Pia uwepo wa wataalamu wachache, unasababisha wananchi kutofikishiwa ujumbe/mafunzo ya kitaalamu kuhusu ugonjwa huo.
“Kwa mfano mimi ni ofisa ugavi ambaye serikali ilinipanga katika kata, lakini inanilazimu nihudumie kata nyingine mbili na hii yangu ya tatu .... je, nitaweza kufanya kazi zangu vizuri kama inavyotakiwa?” alihoji ofisa huyo.
Mmoja wa wataalamu kutoka katika halmashauri hiyo  Dominick Yustadi anasema tangu ugonjwa wa mnyauko uingie wilayani humo fedha kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakulima zimekuwa zikitolewa kidogokidogo tofauti na mahitaji yao kwa siku.
Yustadi anasema hawana vifaa vya kutosha kama vile magari, pikipiki hata dawa kwa wale wakulima ambao mashamba yao yameathiriwa sana na ugonjwa.
Kutokana na hali hiyo, katika kata za Kamuli, Nyakatuntu na Bugene wakulima wengi hawana uelewa wa kudhibiti ugonjwa huo hali inayosababisha migomba mingi kuambukizana na kumaliza shamba zima.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wananchi hao walieleza kuwa wanashindwa kudhibiti ugonjwa huo kwa kuwa wengi wao hawajui namna ya kuihudumia migomba yao.
Bila kujua namna maambukizi ya ugonjwa huo yanavyofanyika, Alvera Batalingaya anasema yeye alitumia vifaa hivyo hivyo kuhudumia migomba isiyo na iliyoathiriwa kwa wakati mmoja.
Kidumu Byonabusha anasema elimu ya kuhudumia migomba yenye maambukizi wanaipata kwa kupeana taarifa wao kwa wao, hali inayowafanya wasiaminiane na kuendelea na utaratibu wao wa kawaida wa kuhudumia mashamba.
Byonabusha anasema hawajawahi kumwona mtaalamu (ofisa kilimo) katika kata au kijiji chao akizungumza na wananchi kuhusu ugonjwa huo.
Kauli ya serikali
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Sophia Kaduma, alikiri kwamba ugonjwa wa mnyauko wa migomba upo na unaenea kwa kasi.
Kaduma anasema ugonjwa huo mpaka sasa hauna dawa dunia nzima na kwamba kwa wale waliofanikiwa kuuondoa ugonjwa huo watakuwa wametumia njia ya GMO ambayo Tanzania sheria na kanuni haijaruhusu kuitumia.
Anasema GMO ni mmea au mnyama ambaye hupatikana (huzaliwa) kwa njia ya teknolojia ya kuchanganya jenetiki yaani DNA (chembe hai) za mmea au mnyama mmoja na mwingine tofauti, ili kuupa mmea huo mpya au mnyama tabia zisizo za asili.
Pamoja na serikali kukataa, wasomi, wanasiasa nchini wameendelea kupinga matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni ambayo huzalisha Genetic Modified Organs (GMO), wakisema matumizi ya teknolojia hiyo ni mabaya kwa taifa.
Anasema mara baada ya ugonjwa huo kuingia mkoani Kagera, wizara yake kwa kushirikiana na halmashauri pamoja na kituo cha utafiti cha Maruku kilichoko Bukoba, walianza kutoa maelekezo kwa wakulima namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Anasema serikali ilichukua jukumu la kutoa vipando kwa kituo cha Maruku na kuwahimiza kuzalisha ili iweze kupatikana miche 40,000 kila mwaka kwa ajili ya kuwapatia wakulima.
Kaduma anakiri kuwapo kwa uchache wa wataalam/ wagani kuanzia ngazi ya wilaya, kata na vijiji na kueleza kuwa serikali ilianza kulichulia uzito miaka miwili iyopita.
Anasema kwa sasa hadi mwaka huu, mkoa wa Kagera una jumla ya wataalamu wa kilimo 11,000 na kwamba serikali imejipanga kuongeza hadi kufikia 15,000 ifikapo mwaka 2015.
Mnyauko wa migomba unavyoambukiza
Ugonjwa wa mnyauko wa migomba unaambukizwa kwa njia ya kugusana; yaani majimaji ya mgomba ulioathirika kugusana na mgomba ambao ni hai.
Uambukizaji huo unaweza kusababishwa na mkulima mwenyewe kutumia vifaa vya kutengenezea migomba katika migomba isiyo na yenye maambikizi ya ugonjwa.
Pia migomba isiyo na maambukizi inaweza kupata ugonjwa endapo mifugo (mbuzi, ng’ombe, kondoo, sungura na mingine) itakula migomba yenye ugonjwa).
Pamoja na mifugo, ndege na nyuki nao wanachangia kwa kiasi kikubwa kueneza ugonjwa kwa kufuata asali iliyoko katika ua dume. Hapo wanaweza kufyonza katika mgomba usiohathika na kuhamishia ulioathirika.
Kuondoa mnyauko wa migomba
Baadhi ya wakulima wilayani Karagwe waliopata bahati ya kuonana na maofisa ugani/wataalamu wa kilimo waliambiwa kuwa ugonjwa wa mnyauko hauna dawa, bali wanaweza kutumia njia ambazo nitazitaja hapo chini ili kuwezakukabiliana nao.
Maofisa hao wa wilaya ya Karagwe nao walitoa maelekezo hayo baada ya kupata mwongozo toka kwa watafiti kutoka kituo cha utafiti Maruku kilichoko Bukoba.
Pamoja na maelezo hayo, wadadisi na wataalamu kuhusu masuala ya kilimo waliotoka sehemu mbalimbali nao wamejitahidi kutoa maelekezo katika mtandao, namna ya kupambana nao.
Wanasema suala la kuondoa mnyauko wa migomba linapaswa kutekelezwa na ngazi zote kuanzia mkulima, mfanyabiashara na mtendaji wa serikali ngazi zote.
Mkulima anapaswa kujijengea tabia ya kufanya usafi wa shamba lake kila siku na kuhakikisha anaondoa ua dume kwa wakati.
Pia mkulima anapaswa kuondoa mgomba ulioathiriwa, kusafisha vifaa alivyotumia shambani kwa maji ya moto yanayochemka, moto au dawa ya jiki ili kuua vijidudu vya maambukizi.
Kama mkulima atashindwa kufuata utaratibu wa kukagua shamba lake mara kwa mara na kuvisafisha vifaa vyake, ugonjwa wa mnyauko hautatoweka kwani utaenea shamba zima.

0754 305805
Next Post Previous Post
Bukobawadau