Mpaka uwekwe wazi kati ya uanajeshi, siasa
Madai kwamba vyombo vya dola vinaingilia shughuli za kisiasa sasa yameanza kuzoeleka hapa nchini na hakuna juhudi zozote zaidi ya kukanusha. Zinazoonekana kufanyika ili kutenganisha mambo haya mawili – siasa na shughuli za ulinzi na usalama wa nchi yetu.
Kwa muda sasa, vyama vya upinzani vimekuwa vikiishutumu Serikali kwa kuwashirikisha watumishi hao wa dola kwa kutumia nafasi hizo za kisiasa kukisaidia chama tawala, CCM, kujiimarisha na kuhujumu au kukandamiza shughuli za upinzani.
Kwa mfano, wakati wa mjadala wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba bungeni, yalizuka malumbano kati ya wabunge wa CCM na wale wa upinzani juu ya kuruhusu wakuu wa wilaya kushirikishwa katika mchakato wa Katiba Mpya badala ya wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wilaya, miji hadi hoja hiyo ikaamuliwa kwa kura na wakuu hao wa wilaya kuruhusiwa kuingia.
Ukiacha madai hayo ambayo yamekuwa yakikanushwa na vyombo vya dola kwa upande mmoja na Serikali kwa upande mwingine, yapo matukio ambayo yanatia shaka, kwa kuwa yanaonyesha dhahiri kwamba si ya bahati mbaya kuwaingiza baadhi ya watendaji wa vyombo vya dola katika shughuli za kisiasa.
Tatizo hili pia linabainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyoishia Juni 30, 2012 kuwa, “Maofisa wa Jeshi waliokuwa wameteuliwa katika nyadhifa za uongozi wa kisiasa waliendelea kuwa na nyadhifa zao za kijeshi kinyume na maagizo yaliyotolewa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu yaliyowataka kujiuzulu vyeo vyao vya kijeshi mara tu baada ya uteuzi katika nyadhifa za kisiasa.”
Licha ya tatizo hilo kubainishwa na CAG na kuendelea kulalamikiwa, limendelea kufumbiwa macho na kutoa picha kuwa matukio hayo yanaachwa kwa makusudi au kwa malengo maalumu.
Hatuoni sababu ya suala hili kuendelea kuwapo kwa kuwa anayewateua anajua kwamba majukumu yao ni tofauti na shughuli za kisiasa na mambo haya hayastahili kuchanganywa ili kulinda utengamano katika nchi yetu, hivyo watumishi hao wanatakiwa kustaafu kwanza utumishi wao katika vyombo vya dola kabla ya kuingia katika nafasi za kisiasa.
Mathalan, ni hivi majuzi tu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, Brigedia Jenerali Cosmas Kayombo amerudishwa Makao Makuu JWTZ kuendelea na kazi yake.
Taarifa za Jenerali Kayombo kurudishwa jeshini baada ya kuitumikia wilaya hiyo kwa miaka miwili na nusu, zimeripitiwa na gazeti hili, Ijumaa juzi kuwa nafasi hiyo ya kisiasa iko wazi.
Tayari Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Elaston Mbwilo amemteua Martha Umbulla, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto kukaimu nafasi hiyo hadi Rais Jakaya Kikwete atakapomteua mwingine.
Huo ni mfano tu wa watumishi wa vyombo vya dola na hasa jeshi wanaoshirikishwa kwenye shughuli za kisiasa kwa nafasi za wakuu wa wilaya na wakuu mikoa, huku ikifahamika kuwa wakuu hao pia ni wajumbe wa kamati za siasa za chama kinachotawala katika maeneo wanayoongoza. Ukiacha tatizo hilo la mgawanyo wa madaraka, CAG pia anaibua jipya la ulipaji wa pensheni kinyume jambo linalopaswa kufanyiwa kazi ili kuokoa fedha za umma, kama anavyosema:
“Maofisa wa jeshi wanaopata ajira za kisiasa hawaachi utumishi wao jeshini hadi wanapofikia umri wa kustaafu katika jeshi na hivyo kusababisha ukokotoaji wa mafao yao ya kustaafu kujumuisha muda ambao wametumikia vyeo katika siasa.”