KAMATI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaanza vikao vyake mjini hapa huku macho na masikio ya Watanzania yakitaka kujua hatima ya Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, ambaye anakabiliwa na tuhuma za ufisadi zilizosababisha mgogoro baina yake na madiwani wanane.
Ajenda ya mgogoro wa umeya mjini Bukoba imelazimika kuingizwa katika vikao hivyo vya juu baada ya chama makao makuu kusitisha uamuzi wa Halmashauri Kuu mkoa wa Kagera wa kuwavua uanachama madiwani wanane wakidaiwa kukisaliti chama kwa kuungana na wenzao wa upinzani wakitaka kumng’oa meya Amani.
Meya Amani anatuhumiwa na madiwani hao kuwa ameiingiza halmashauri kwenye mikataba mitatu ya kifisadi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vilevile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh. milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa NEC, Itakadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema kwa sasa sekretarieti ya chama hicho tayari inaendelea na vikao ambapo leo mchana Kamati Kuu itakaa chini ya mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete.
Alizitaja ajenda nyingine za vikao hivyo mbali na mgogoro wa umeya Bukoba kuwa kujadili maoni yaliyokusanywa na chama kuhusu rasimu ya Katiba mpya na hali ya kisiasa nchini.
Nape alisema kuwa Agosti 24 na 25 mwaka huu, NEC Taifa itaendelea na vikao vyake ambapo itatoa uamuzi mbalimbali wa mambo ambayo hayakupatiwa ufumbuzi na Kamati Kuu.
Alisema kuwa Agosti 24, asubuhi, chama hicho kitazindua baraza la wazee kitaifa ambalo wajumbe wake ni viongozi wakuu wastaafu ambao ni marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Dk. Salmin Amour, Amani Abeid Karume na Samuel Malecela na Pius Msekwa ambao walipata kuwa wenyeviti na makamu wa chama hicho.
Faida na hasara
Vyanzo vyetu vya ndani ya CCM vimedokeza kuwa endapo chama hicho kitabariki uamuzi wa NEC Kagera na kuwatimua madiwani hao wanane huenda kikajichimbia kaburi la kisiasa mjini Bukoba kwani kutokana na nguvu ya CHADEMA itakuwa vigumu kurejesha kata zote.
Hata hivyo baadhi ya madiwani hao wameonyesha wazi kuhamia CHADEMA endapo watavuliwa uanachama wa CCM kwani hata Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amewakaribisha rasmi kuwa watapokelewa kutokana na ushujaa wao wa kupambana na ufisadi.
Pia uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao, unaweza kukifanya chama hicho kumpoteza mbunge wake wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki, ambaye anawaunga mkono. Duru za kisiasa zinadai kuwa madiwani hao wamemshinikiza ajiuzulu ubunge ikiwa wao wataondolewa.
Lakini uamuzi wa kumtosa meya Amani unaweza kukijengea heshima chama hicho mbele ya umma kikaonekana kupambana na ufisadi kwa vitendo ingawa utaleta mpasuko kwa viongozi wake wa wilaya na mkoa.
Hadi tunakwenda mitamboni jana, kiongozi mmoja mwandamizi wa CCM ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu alilihakikishia gazeti hili kuwa meya Amani lazima ang’olewe ili kukinusuru chama.
“Unajua hata tukifumba macho tukamlinda meya na kuwatosa madiwani ambao kimsingi mimi sioni kosa lao, bado wanaweza kwenda mahakamani kupinga uamuzi wetu na ndani ya muda huo wa kungoja uamuzi wa mahakama wakapiga kura na kumwondo meya,” alisema kiongozi huyo aliyeomba kuhifadhiwa jina lake kwa vile si msemaji wa chama.
CCM Taifa iliagiza madiwani hao wanane waendelee na kazi zao za udiwani kama kawaida, huku wakisubiri uamuzi wa Kamati Kuu.
Nape alifafanua kuwa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola hasa wabunge na madiwani, uamuzi wa halmashauri ya mkoa si wa mwisho, kwani unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu ndipo utekelezwe.
Hivi karibuni akiwa mjini Bukoba, Rais Jakaya Kikwete alijaribu kuingilia kati mgogoro huo kwa kuwataka meya Amani na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki, kumaliza tofauti zao ili miradi hiyo iendelee kutekelezwa.
Hata hivyo, ushauri wake ulipuuzwa na madiwani hao pamoja na wenzao wa CHADEMA na CUF wakisema tatizo si ugomvi kati ya wawili hao bali wanapinga ufisadi wa meya wao kuingia mikataba ya miradi bila kuwashirikisha.
Madiwani 15 walisaini hati ya tuhuma za ufisadi dhidi ya meya na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Kati yao wa CCM na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Wapinzani waliokuwa wameungana nao ni Dismas Rutagwelela (Rwamisenyi), Israel Mlaki (Kibeta), Winfrida Mukono (viti maalumu), Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu CHADEMA pamoja na Ibrahim Mabruk (Bilele), Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia Badru (viti maalumu - CUF).
|