CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kimetengua uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho Mkoa wa Kagera wa kuwafukuza uanachama madiwani wake nane katika Manispaa ya Bukoba.
Uamuzi wa kufukuza madiwani hao ulifanywa na Halmashauri ya CCM Mkoa juzi jioni, lakini CCM Makao Makuu iliubatilisha jana asubuhi.
Wakati kikao kilichowafukuza uanachama kiliwatuhumu na kuwahukumu madiwani hao kwa kuungana na madiwani wa upinzani kusaini hati ya kumng’oa Meya Anatory Amani, ambayo uongozi wa mkoa uliona ni usaliti kwa chama, taarifa ya CCM kutengua uamuzi huo, iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, ilisema uamuzi huo si wa mwisho.
“Utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM walio kwenye vyombo vya dola, hasa wabunge na madiwani, uamuzi wa NEC Mkoa si wa mwisho, kwani unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu NEC Taifa ndipo utekelezwe,” alisema.
CCM Taifa imeagiza madiwani hao nane waendelee na kazi zao za udiwani kama kawaida, huku wakisubiri uamuzi wa Kamati Kuu ya NEC Taifa, ambayo imeamua kuweka ajenda yao kwenye kikao hicho kitakachofanyika Dodoma Agosti 23.
Katika hali ya kushangaza, Nape alidai kwamba jana saa nne asubuhi alikuwa tayari amepokea barua za madiwani hao, kwamba walikata rufaa kupinga uamuzi wa kufukuzwa nyadhifa zao.
Hata hivyo, mantiki inakataa kwani uamuzi wa kufukuza madiwani ulifanyika jana na kutangazwa kwenye mkutano na vyombo vya habari kabla hata madiwani wenyewe hawajapewa barua za kuwafukuza.
Kwa maana hiyo, hata wao wasingeweza kuandika rufaa kabla ya kupokea barua hizo. Na hata kama wangezipata na kuandika, zisingekuwa zimefika ofisini kwa Nape alfajiri, kwa kuzingatia changamoto ya miundombinu.
Mwandishi mkongwe na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Ndimara Tegambwage katika maoni yake kwenye mtandao wa kijamii wa Mabadiliko naye alitilia shaka taarifa hiyo ya Nape.
“Umemsikia Nape wako? Madiwani wamefukuzwa jana. Huenda hawajapata hata barua za kuwafukuza; kwani sharti kila mmoja apate barua inayomweleza uamuzi na kwanini amefukuzwa.
“Lakini tayari Nape anasema madiwani wamekata rufaa na kwamba rufaa hiyo tayari imewafikia makao makuu - Dar au Dodoma (!?).
“Katika mazingira haya, madiwani wanaweza kuwa wamefukuzwa kwa tangazo la redioni, kwa sms au nzamba mitaani; na wao waweza kuwa wamekata rufaa kwa sms.”
Taarifa zilizoifikia Tanzania Daima kutoka vyanzo vya ndani vya CCM zinasema kuwa sakata hili limeleta msukosuko katika chama hicho, kwa maelezo kuwa iwapo madiwani hao watafukuzwa, itakuwa sawa na kufuta CCM Bukoba Mjini.
Vile vile, kama CCM ingeacha wakaenda mahakamani kupinga kufukuzwa, wangeweza kurejeshwa na kuendelea na mkakati ule ule wa kumtimua meya.
Habari za ndani zinasema ili CCM ijiweke katika mustakabali mzuri kisiasa Bukoba, italazimika kupoteza diwani mmoja badala ya madiwani wanane.
“Hata hivyo, taarifa zilizo ofisini kwetu zinaonyesha kwamba huyu bwana ana matatizo. Tukiwatimua hawa yataibuka makubwa, na yatatuaibisha hata sisi. Hapa ni kuvuta muda tu, lakini nadhani meya ataondoka tu,” kilisema chanzo chetu.
Hatima ya Meya Amani sasa inategemea hatua watakayochukua madiwani hao wakati wowote kuanzia sasa, na uamuzi wa Kamati Kuu itakayokutana Dodoma wiki ijayo.
Taarifa nyingine zinasema kuwa juzi jioni mara baada ya Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kusikia habari za kutimuliwa kwa madiwani hao, aliwapigia simu viongozi wa serikali na CCM Mkoa wa Kagera kuhoji shabaha ya wao kufikia uamuzi ule katika mazingira ya sasa ya kisiasa.
Mkuu wa Mkoa alimjibu kuwa walikuwa wanatekeleza ushauri wa Rais Jakaya Kikwete, hasa baada ya kuona madiwani wamekamia kumwondoa meya, badala ya kutii agizo la rais.
Hata hivyo, kauli ya Rais Kikwete aliyotoa hivi karibuni akiwa Bukoba, hakuzuia madiwani kufukuza meya, bali iliwataka Amani na Mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki wamalize tofauti zao; ushauri uliopingwa na madiwani wakisema mgogoro huo haukuwa kati ya watu wawili, bali kati ya meya na madiwani 16 wanaotaka ang’oke kwa kuingiza ufisadi kwenye miradi kadhaa ya manispaa.
Katika hali ya kushangaza, Nape jana alipoulizwa sababu za Rais Kikwete kushindwa kuona ufisadi katika mgogoro, badala yake akasema ni wa meya na mbunge, hivyo wapatane, alisema rais hajatoa ushauri huo, bali alinukuliwa vibaya na vyombo vya habari.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake mjini Bokoba hivi karibuni kuhusu mgogoro huo, alisema kuwa ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano ‘yasiyokuwa na msingi’.
Madiwani hao nane na wenzao saba wa upinzani walipinga kauli ya rais wakisema malumbano hayo si kati ya Kagasheki na meya kama alivyopewa taarifa bali wanapinga ufisadi wa miradi inayokusudiwa kutekelezwa.
Walisisitiza kuwa hawapingi miradi hiyo bali utaratibu ambao meya ametumia kuianzisha bila kuzingatia maslahi ya wananchi kwa kuwashirikisha madiwani.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Baada ya kikao cha NEC juzi jioni, Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera, Avelin Mushi aliwaeleza waandishi kuwa madiwani hao wamevuliwa uanachama.
Hata hivyo, uamuzi huo unadaiwa kulinda ufisadi anaotuhumiwa kuufanya Amani katika utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba amekuwa akikingiwa kifua na viongiozi wa chama na serikali mkoa ili asing’olewe na madiwani.
Madiwani 15 walisaini hati ya tuhuma za ufisadi dhidi ya meya na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Wapinzani waliokuwa wameungana nao ni Dismas Rutagwelela (Rwamisenyi), Israel Mlaki (Kibeta), Winfrida Mukono (viti maalumu), Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu CHADEMA pamoja na Ibrahim Mabruk (Bilele), Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia Badru (viti maalumu - CUF).
VIA;Tanzania Daima.
|