WAKULIMA wa kahawa Kagera wanaounda Chama Kikuu cha Ushirika cha KCU (1990) Ltd., wanasema kidogo ujio wa Rais Kikwete mkoani kwao umekuwa na neema.
Eti kabla ya Kikwete kukanyaga ardhi ya Bukoba uongozi wa KCU (1990) Ltd. ulihakikisha unawalipa wakulima wa kahawa malimbikizo yote ya madai yao waliyokuwa wanakidai chama hicho.
Shukurani za pekee za wakulima hao wanazitoa kwa waandishi ambao muda wote wameuvalia njuga ufisadi unaofanyika ndani ya KCU (1990) Ltd., ufisadi unaokifanya chama hicho cha ushirika kiwageuze wakulima na kuwafanya waonekane kama manamba wanaokizalishia kwa neema ya uongozi wake.
Sababu muda wote imeonekana wanaoneemeka na ushirika huo, au tuseme wanaoneemeka na kinachozalishwa na wakulima hao ni viongozi na watumishi wa KCU (1990) Ltd. badala ya wakulima, wanaushirika ambao ndio wenye mali.
Washirika hao wanasema kwamba bila waandishi kulivalia njuga suala hilo la ufisadi ndani ya chama hicho uongozi usingeshtuka na kuwalipa malimbikizo yao ya madeni kabla ya ujio wa rais, ambaye uongozi wa KCU (1990) Ltd., ulitaka akisafishe chama hicho dhidi ya tuhuma za ufisadi zinazokikabili.
Muda wote wakulima hao wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli zao muhimu kutokana na ukata unaosababishwa na KCU (1990) Ltd. kutowapatia malipo yao kwa muda unaotakiwa kwa madai kuwa chama hicho hakina pesa, lakini wakati huohuo viongozi na watumishi wake wakiwa wamebobea kwenye ‘matanuzi’ ya kila aina.
Nyaraka za kiofisi za chama hicho ambazo inaaminika kwamba wakulima walio wengi hawazioni, zinadhihirisha madai hayo ya wakulima.
Zimekuwapo hoja za utetezi zinazotolewa na uongozi wa KCU (1990) Ltd. kwamba malalamiko yanayotolewa na wakulima dhidi ya uongozi huo yanasukumwa na baadhi ya watu walioukosa uongozi katika chama hicho.
Hata hivyo hoja hizo hazitengui maswali mbalimbali ya msingi. Mfano, inawezekanaje mmoja wa viongozi wa KCU (1990) Ltd. amiliki kampuni inayofanya kazi na chama kinachomuajiri, yeye akiwa muhidhinisha malipo na mpokea malipo?
Wanauliza inawezekanaje chama hicho kikasalimika kiuchumi katika mgongano wa masilahi wa aina hiyo?
Hoja nyingine zinazotolewa na wanaushirika hao ni kwamba kiongozi huyo analipwa sh 250,000 kwa mwezi, eti kwa kufanya kazi katika mazingira magumu kana kwamba ofisi yake iko porini, wanauliza ni mazingira gani anayofanyia kazi yaliyo magumu kuyazidi ya wakulima wanaomuajiri?
Wanasema pamoja na hiyo ana walinzi wawili kwa mshahara wa sh 125,000 kwa mwezi kila mmoja.
Anaingia kwenye vikao vya bodi mara 12 kwa mwaka akilipwa sh 40,000 kwa kila kikao.
Anapatiwa matibabu na bima, anapewa malipo ya mawasiliano, malipo ya makaribisho, zawadi za sikukuu, posho mbalimbali za safari ndani na nje ya nchi.
Sasa wakulima wanauliza kwamba hayo ndiyo mazingira magumu yanayomfanya mkuu huyo alipwe kiasi hicho kwa mwezi?
Eti malipo hayo yanayofanyika bila kuzingatia kuyumba kwa bei ya kahawa yanafikiriwaje kama ugumu wa maisha na mazingira ya mkulima havitiliwi maanani?
Sababu chama cha ushirika kipo kumnufaisha mkulima, kumtafutia soko la mazao yake kwa bei nzuri na kumtia moyo wa kuendeleza kilimo husika.
Lakini eti kwa KCU (1990) Ltd. mambo yamekuwa kinyume kabisa. Chama kinaonyesha majengo kama vitega uchumi wakati wanaushirika wakikaribia kuing’oa mibuni kutokana na zao hilo kuonekana halina masilahi kwao, bei ndogo na pesa haitolewi kwa wakati.
Swali lao ni je, waachane na kulima kahawa ili wakawekeze kwenye majengo ambayo chama chao kinaona ndivyo vitega uchumi vinavyofaa?
Nilipozungumza na mdau mmoja wa ushirika akanieleza kwamba alipata nafasi ya kuhudhuria sherehe za vyama vya ushirika duniani zilizofanyika jijini Manchester, Uingereza.
Anasema kwamba katika nchi za wenzetu vyama vya ushirika vimeendelea kiasi cha kumiliki viwanda vya kutengeneza ndege.
Swali tunaloweza kujiuliza ni je, sisi tutaweza kufika huko katika hali hii ya viongozi tunaowaweka kuongoza na kusimamia ushirika kugeuka mchwa unaoutafuna ushirika?
Katika kuhakikisha mchwa unaoutafuna ushirika unadhibitiwa ni lazima uongozi wa nchi uingilie kati pasipo kujali kauli tata kama ile iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC), Willigs Mbogoro, kwa waandishi wa habari kwamba wanasiasa hawapaswi kuingilia shughuli za ushirika.
Maana siasa inasimamia kila jambo ndani ya nchi. Hata mzazi hakikataa kumpeleka shule mtoto wake ni lazima siasa itaingilia kati bila kujali kwamba mtoto husika haikumzaa yenyewe.
Rais Kikwete kaonesha mfano kwa kuunda tume ya kuchunguza kwa nini bei ya kahawa inakuwa chini upande wa Tanzania ilhali ikiwa juu upande wa Uganda, kiasi cha kuwashawishi wakulima wa kahawa mkoani Kagera kuamua kuuza kahawa yao kwa magendo nchini Uganda?
Mbona rais hakusema asiyaingilie hayo kwa vile ni masuala ya ushirika na yeye ni mwanasiasa?
Ila jambo analopaswa kulielewa rais ni kwamba juhudi zake za kuwaona wananchi wakineemeka kwa jasho lao zinakwamishwa na wasaidizi wake.
Mfano, suala la kushuka kwa bei ya kahawa lililomshtua rais kiasi cha kuliundia tume ya uchunguzi alipaswa apate jibu lake kutoka kwa Waziri wake wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, kabla ya uamuzi aliouchukua.
Maana waziri huyo anayo malalamiko mengi aliyoyakalia, hasa yaliyopelekwa kwake na wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. kuhusu ufisadi ndani ya chama hicho.
Wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. walitegemea Injinia Chiza aseme lolote kuhusu sakata la washirika wa KCU (1990) Ltd. na uongozi wake, wakati wa ziara ya rais mkoani Kagera.
Lakini wakashangaa kumuona waziri amenyamaza huku rais akihangaika kujua kinachoendelea pamoja na kuonyeshwa jengo jipya kuwa ni kitega uchumi cha ushirika huo.
Ni kwamba, uendeshaji wa kifisadi ndani ya chama hicho ni lazima utakuwa unachangia kwa kiasi kikubwa malipo kiduchu wanayoyapata wanaushirika hao.
Haiwezekani makao makuu ya KCU (1990) Ltd. yakapandisha bajeti yake na kufikia karibu sh bilioni 2 kwa mwaka ikakosa kuathiri bei ya kahawa kwa mkulima.
Hayo ni mambo ambayo Chiza amekwisha kuelezwa, lakini kwa sababu ambazo haziwekwi wazi, anaonekana kuyapiga chenga.
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe, naye alipaswa kuwa na jibu kwa nini bei ya kahawa iwe chini mkoani Kagera wakati iko juu nchini Uganda. Au kwa nini wafanyabiashara binafsi wanunue kwa bei ya juu lakini KCU (1990) Ltd. inunue kwa bei ya chini?
Vilevile Massawe alitakiwa kumweleza rais ukweli juu ya malalamiko ya wakulima wa kahawa mkoani kwake kwa Chama chao Kikuu cha Ushirika cha KCU (1990) Ltd. kama kweli amedhamiria kumsaidia bosi wake katika dhamira yake ya kuwaona wananchi wananufaika na jasho lao.
Lakini badala yake Massawe alimuacha rais akalifungua jengo linalodaiwa ni la kitega uchumi cha ushirika huo ambao hapana shaka yoyote kuwa unayumbishwa na uongozi wake.
Tukio la rais kuzindua jengo la kitega uchumi cha KCU (1990) Ltd. huku akikimwagia sifa chama hicho kuwa walau kinacho cha kuonyesha, limetafsiriwa na wengi kama rais kuubariki ufisadi.
Hata hivyo rais hakuwa na hatia, maana alionyeshwa kitega uchumi cha ushirika badala ya kuonyeshwa hali halisi ya kiuchumi ya wanaushirika ilivyo.
Hivyo ndivyo Rais Kikwete anavyokwamishwa na wasaidizi wake katika mambo mbalimbali.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
|