Waziri Mkuu Pinda ashtakiwa mahakamani
Dar/Dodoma. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemfungulia mashtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi karibuni kwamba wanaokaidi maagizo ya dola wapigwe.
Hatua hiyo ya LHRC imepingwa vikali na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Dk Elieza Feleshi akisema hakuna uhalali wa mashtaka yoyote dhidi ya kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba alifungua mashtaka hayo katika Mahakama Kuu jana akisema kuwa wanamshtaki Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa amekiuka kifungu cha Katiba Ibara 13 (1). Pinda ametajwa kuwa ni mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo namba 24.
Mkurugenzi wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia alisema jana kwamba, mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ya kikatiba iliyofunguliwa na LHRC na Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema.
Alisema katika kesi hiyo, kuna jopo la mawakili wasiopungua 20 na kwamba wamepata saini za wananchi 2,029 wanaopinga kauli hiyo ya Pinda na kuunga mkono kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Mjumbe wa Bodi ya LHRC, Wakili Dk Ringo Tenga alisema katika kesi hiyo wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi za binadamu na kwamba kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki hizo.
Kauli yenyewe
Wakati wa Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni, Juni 19, mwaka huu, Waziri Mkuu akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo vya dola?”
Waziri Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna namna nyingine... maana tumechoka.” Kesi hiyo itakayosikilizwa na majaji watatu, haina uhusiano na kesi nyingine ambazo wajibu maombi hupewa siku 90 kujibu hoja zilizowasilishwa. Kesi hiyo imefunguliwa kwa mujibu wa Katiba Sura ya Tatu.