Bukobawadau

WIAZARA YA MAGUFURI YAMJIBU ZITTO ZUBERI KABWE

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UJENZI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Yah: USAHIHI WA MATUMIZI YA KASMA MAALUM YAUJENZI WA MIRADI YA BARABARA NCHINI SHS. 252,975,000,000.00

Tarehe 22/08/2013, Wizara ya Ujenzi ilikutana na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kwa ajili ya kujadili Hesabu zilizokaguliwa za Fungu 98 kwa mwaka wa fedha wa 2011/2012. Kikao hicho kilifanyikia katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Mhe. Gaudence Cassian Kayombo Mbunge wa Mbinga Mashariki, ambaye alitoa maamuzi na maelekezo rasmi ya Kamati.

Katika kikao hicho hoja kadhaa zilijadiliwa ikiwamo hoja kuhusu Matumizi ya Kasma Maalun ya Ujenzi wa Miradi ya Barabara nchini ambayo ilitengewa kiasi cha Shs. 252,975,000,000.00.

Katibu Mkuu (Afisa Masuhuli) wa Wizara ya Ujenzi alikiarifu kikao hicho kuwa fedha za Mradi huo Maalum zilitumika kwa ajili ya kulipia madai ya Makandarasi na Wahandisi Washauri kwa miradi ya ujenzi wa barabara inayoendelea katika mipango na bajeti ya Serikali. Katika ujenzi wa barabara; jukumu la msingi kwa Wizara ni kulipa madai ya Makandarasi na Wahandisi Washauri.

Aidha, alifafanua kwamba Mradi huu umekuwa na matokeo mazuri kwani ulifanikisha shughuli za ujenzi wa barabara nchini. Afisa masuhuli aliendelea kufafanua kwamba mradi huu wa barabara haukuwa mradi kivuli bali ulikuwa ni mradi maalum kwa lengo la kufanikisha programu ya barabara na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

Tarehe 22/08/2013 na tarehe 23/08/2013 zimetolewa taarifa za upotoshaji na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu ukweli wa suala hili ambapo baadhi ya vyombo hivyo vilinukuliwa kusema kuwa kumekuwepo na ufisadi, matumizi tata na ubadhirifu katika mradi huu.

Wizara inapenda kuudhibitishia umma kwamba katika utekelezaji wa mradi huu hapakuwepo na ufisadi, ubadhilifu, au matumizi tata.

Ukweli huu umethibitishwa kwa maandishi na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwamba hoja ya ukaguzi huu haikuhusu ubadhirifu au matumizi mabaya yoyote ya fedha bali ni suala la uandishi wa vitabu vya fedha uliohitaji kuboreshwa.

Wizara ya Ujenzi inapenda kutoa ufafanuzi huu na kuudhibitishia tena umma kwamba hakuna upotevu wowote wa fedha kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vimetaka ieleweke.

Taarifa hii imetolewa na;

Balozi Herbert E. Mrango
KATIBU MKUU (AFISA MASUHULI)
WIZARA YA UJENZI
Next Post Previous Post
Bukobawadau