RAI YA JENERALI Adui wa maendeleo: Ndwele na gharika, nakisi ya uongozi pia
WIKI jana nilijaribu kuonyesha jinsi ambavyo mwanzo wa maisha ya binadamu yanaweza kushabihiana na yale ya mbuzi na wanyama wengine, na hata na yale ya mche wa mchunga kwa maana ya kupandikizwa katika mazingira stawishi, mazingira yanayostawisha kutungwa kwa mimba na kumea kwa mche.
Nilijaribu kuonyesha pia jinsi ambavyo binadamu anavyojipambanua baada ya muda mfupi, kwanza kwa muendelezo wa malezi na makuzi yake, ambayo huchukua kipindi kirefu zaidi, na chenye kuhitaji uangalizi mkubwa na wa karibu zaidi kuliko ilivyo kwa mbuzi au mche wa mti.
Hii ina maana kwamba, ili binadamu aweze kutekeleza wajibu wake kama mtawala wa mazingira yake na vitu vyote vinavyomzunguka, anahitaji malezi na makuzi yaliyo makini kuliko yale ya viumbe vingine. Aidha, malezi hayo na makuzi hayo yanatakiwa yatokane na jamii ya binadamu wenyewe, tofauti na ambavyo malezi ya mbuzi na mche wa mchungwa kwa kiasi kikubwa hayaelekezwi na mbuzi wenyewe au michungwa yenyewe bali huelekezwa na binadamu.
Jamii ya binadamu hujilea yenyewe. Nasema hivyo nikijua kwamba wako ambao, kutokana na itikadi za kidini, watasema kwamba binadamu hulelewa na Mungu, au miungu, ikitegemea iwapo itikadi hiyo ni mojawapo ya zile za kwetu za asili au ni mojawapo ya hizi zilizokuja kutoka ughaibuni.
Lakini hata tungekubali kwamba kuna “uungu” katika malezi na makuzi ya binadamu, hatuna budi kwamba sehemu ya “uungu” huo imekasimiwa jamii ya binadamu kupitia wakuu wa asasi zinazosimamia mambo haya, ikiwa ni pamoja na familia, asasi za utawala na zile za imani.
Katika imani zetu za asili, na katika imani zilizoletwa kwetu na wageni, umuhimu wa jamii katika kuendesha maisha yetu umewekwa wazi, kiasi kwamba, hasa katika imani zetu za kale, hakuna mtu mmoja aliyeweza kuwa na nguvu, hekima, ukwasi au uwezo wowote ule ambao haukutokana na jinsi miungu walivyoona kwamba ni vyema awe navyo kwa manufaa ya jamii.
Ni kweli, nakiri, kwamba, imani za jamii zilitofautiana katika maudhui yake; na ni kweli pia kwamba jamii zetu, kabla hazijaparaganyika zilipokumbana na wavamizi, hazikuwa zimefikia viwango vilivyofanana vya weledi, umakini na upeo wa maono. Tunazo kumbukumbu zinazoonyesha kwamba baadhi ya jamii zilikuwa zina viwango vya juu mno vya sifa hizo, na zikiwa zimejijengea taratibu za dola zilizowashangaza wageni, wakati jamii nyingine zilikuwa bado ni za “kishenzi,” za wasasi wa ndezi na wachumaji wa matunda-pori.
Inatubidi kuchukua mifano kutokana na jamii zilizokuwa zimepiga hatua muhimu za maendeleo, nikijua kwamba, kama isingekuwa kuingiliwa na kuvurugwa na wageni, hata zile jamii zilizokuwa nyuma kimaendeleo zingepata fursa ya kujifunza kutokana na maingiliano na jamii jirani zilizokuwa zimetangulia. Hiyo ndiyo silika ya jinsi maendeleo yanavyoambukiza.
Si kila jamii hupiga hatua za maendeleo. Zipo jamii, na tunazijua, ambazo tangu zianze kuwa jamii, ni jamii zilizodumaa zikilinganishwa na jamii zilizo jirani tu. Na wala si kila jamii iliyowahi kuonja matunda ya maendeleo imeendelea kuchuma matunda makubwa zaidi au yaliyo bora zaidi.
Nyingine huonyesha dalili za uwezo wa kuendelea na kwenda mbali sana, lakini, hutokea, kwa sababu zinazoelezeka, zikapotea njia, zikajikuta zimekwama, na zikaanza kutembea kinyumenyume, zikapitwa na jamii jirani zilizokuwa zikidharauliwa zamani, zikabaki ni kichekesho.
Iwapo jamii iliyokuwa imeonyesha dalili za maendeleo hapo mwanzo ikikumbwa na zahma kubwa ya tabia-nchi, kama tetemeko la ardhi au gharika; au iwapo jamii kama hiyo ikikumbwa na vita ya muda mrefu inayosababisha maangamizi makubwa ya maisha ya watu na upotevu wa mali; au iwapo jamii hiyo itashambuliwa na ndwele ya maambukizo ya halaiki, kama tauni, jamii hiyo, hata kama itakuwa imekwisha kuonyesha dalili za maendeleo, itarudi nyuma.
Lakini, pia, iwapo jamii yoyote iliyo nyuma kimaendeleo lakini ikawa imetangaza kwamba imedhamiria kupiga hatua za haraka kujiletea maendeleo, halafu jamii hiyo ikadhani kwamba maendeleo yataletwa na watu wengine, wageni kutoka nje, jamii hiyo itaweza kwenda sehemu nyingi, lakini haitakwenda kokote kwa maana ya maendeleo.
Inaweza kwenda utumwani, hilo ni rahisi, kwa sababu hao inaowaona kama “wafadhili, “wawekezaji,” “marafiki,” “washirika wa maendeleo,” na maelezo mengine ya kipuuzi, ni watu kutoka jamii zinazotafuta maslahi yao, si yetu, na kutupeleka utumwani tena si jambo la ajabu iwapo tutajipeleka wenyewe kama mazuzu.
Njia moja kuu ya kutusaidia kutupeleka katika utumwa mamboleo na zahma kubwa kuliko hizo nilizozitaja hapo juu, ni balaa ya kuwa na nakisi (deficit) ya uongozi ndani ya jamii. Nakisi ya uongozi ni ugonjwa mbaya zaidi kuliko tauni, kuliko tatizo jingine lolote la kijamii.
Hapa ninazungumzia “uongozi” kwa maana ya ujumla wa watu, mifumo, miundombinu, maadili, maono, mitazamo, matarajio, makatazo, miiko, ya watu wanaojitambua kama wa jamii moja yenye utambulisho unaojitambua na malengo yanayoshabihiana.
Sizungumzii watu waliomo ofisini, wengine wakiwa “wamechaguliwa” kwa kura za ukweli na za uongo, wengine wakiwa wameteuliwa na kuchomekwa katika ofisi hizo. Nazungumzia uongozi kwa maana ya nishati mchanganyiko ya jumla ya kijamii ya kujisukuma kuelekea kwenye hali bora zaidi ya maisha (maendeleo) kwa misingi endelevu na ya masafa marefu.
Ni rai yangu kwamba hili si jukumu la wale wanaoshikilia ofisi mahsusi, kwa sababu ingawaje baadhi yao wanaweza kuwa viongozi pia, wengi wao ni wakuu wa ofisi hii au ile, lakini hawana sifa zozote za uongozi.
Nitajadili ni jinsi gani tumejenga nakisi kubwa ya uongozi, na ni kwa nini tunashindwa kujiletea maendeleo ya haraka, na badala yake tunajikuta tunasuasua katika maendeleo mengi, na hali hii inatujengea unyonge mkubwa kama taifa.