WATU watatu wanaosadikiwa kuwa majambazi wamemteka Diwani wa Kata ya Chonyonyo wilayani Karagwe mkoani Kagera kisha wakamchomea gari lake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi, tukio hilo lilitokea juzi saa 2:00 usiku katika eneo la Nyakasimbi wilayani humo.
Alimtaja diwani huyo kuwa ni Anord Rwesheleka (CCM) akisema kuwa alitekwa na watu watatu wasiojulikana wakiwa na bastola japo alifanikiwa kuwatoroka kabla ya hawajamdhuru.
Kamanda Kalangi alisema Rwesheleka alipita katika kizuizi cha polisi cha Chanyamisa saa 11:00 jioni akisema kuwa anaelekea katika kijiji cha Nyakasimbi kumuona bibi yake ambaye alidai ni mgonjwa.
Kwamba saa 2:00 usiku wakati diwani huyo akirudi Chonyonyo alikutana na mtu mmoja ambaye alimsimamisha na kisha kumtisha kwa kumuonyesha bastola na kumwamuru ageuze gari na kurudi barabara ya Benako.
Alisema kuwa wakati akiendelea na safari kuelekea alikoelekezwa, mbele kidogo walikutana na watu wengine wawili na kisha akaamriwa asimamishe gari na watu hao walianza kupakiza mizigo ndani.
Kamanda aliongeza kuwa wakati watu hao wakiendelea kupakiza mizigo ndani ya gari, diwani huyo alifanikiwa kuwatoroka na kutokomea porini na baadaye katika barabara iendayo Karagwe ndipo ghafla likatokea gari aina ya Toyota Hiace likitoka Benako na kumpa msaada.
Alisema kuwa wakati akiwa kwenye Hiace aliambiwa na wasafiri kuwa wameona gari lake likiwaka moto maeneo ya Nyakasimbi.
Kalangi alisema kuwa diwani Rwesheleka alifika katika kituo kidogo cha polisi Chanyamisa saa 3.30 usiku kutoa taarifa kuwa alitekwa na majambazi.
“Baada ya kutoa taarifa, polisi waliondoka naye mpaka eneo la tukio na kukuta gari hilo likiendelea kuteketea. Bado uchunguzi unaendelea kwani mazingira yake yanatatanisha.
Rwesheleka alipohojiwa na gazeti hili jana, alisema alinusurika kifo wakati akitoka kumuona bibi yake eneo la Nyakasimbi.
|