CCM inavyotishia majaaliwa ya Watanzania
NA PRUDENCE KARUGENDO
TANZANIA ni moja ya nchi zenye makabila mengi duniani, sina takwimu sahihi kwa hapa, lakini nadhani katika Afrika Tanzania itakuwa ya pili kwa wingi wa makabila nyuma ya DRC yenye makabila zaidi ya 400. Kwa mtaji huo ni lazima Tanzania itakuwa na lugha nyingi tofauti tofauti, tamaduni nyingi tofauti tofauti mbali na tamaduni za kigeni tulizozipokea na kuzifanya sehemu ya tamaduni zetu, hapa namaanisha dini za kigeni.
Lakini hatahivyo, pamoja na ukweli huo, Watanzania tumekuwa muda wote tukionekana ni kitu kimoja kuliko nchi nyingine yoyote duniani. Utitiri wa makabila, lugha na tamaduni tulio nao haujaweza kutugawa kiasi cha kutukosesha amani. Pamoja na vilugha chungu nzima tulivyo navyo tumeamua kuchukua lugha moja tu na kuienzi kama lugha yetu, Kiswhili, tukiwa tumeviweka pembeni vilugha vyetu vyote hivyo.
Kiswahili kimeweza kuziunganisha tamaduni zetu zote na kuzifanya zionekane ni utamaduni mmoja. Ni kwa maana hiyo hata tamaduni za kigeni, hasa Uislamu na Ukristo, ambazo kimahesabu ni kama zimeigawa idadi ya Watanzania nusu kwa nusu, hazijaweza kutufarakanisha. Watanzania mpaka sasa tunaonekana ni kitu kimoja, kabila moja, lugha moja na utamaduni mmoja. Ni kitu ambacho nchi nyingi zinakionea husuda.
Nitoe mfano wa majirani zetu wa DRC, wingi wa makabila na lugha zao umewafanya wawe na lugha tano rasmi za taifa, Kiswahili, Lingala, Kikongo, Tshiluba na Kifaransa. Lakini hatahivyo utaratibu huo haujaweza kuyafanya makabila ya DRC kuaminiana na kujiona ni kitu kimoja. Kila kabila nchini mle linalishuku lingine na kuliangalia kwa jicho la tahadhari. Machafuko yaliyodumu nchini mle tangu enzi za wakoloni mpaka miaka 50 baada ya uhuru ni ushahidi tosha wa hili ninalolitazama hapa.
Kwa maana hiyo Watanzania hatunabudi kumshukuru Mungu kwa yote aliyotujaalia ikiwa ni pamoja na kutuweka katika makabila mengi mbalimbali pia akatuwezesha kuelewana kwa upendo ndani ya utitiri huo wa makabila kiasi cha kuonekana kama kabila moja. Tunao utitiri wa lugha lakini tumeamua kutumia moja tu isiyo na upande wowote, Kiswahili.
Tukifika hapo kuna wanaopenda kumvisha kilemba cha ukoka Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, kuwa ndiye aliyekileta Kiswahili, sijui alikileta kutoka wapi! Wakati Nyerere mwenyewe alikuwa akikiri mara kwa mara kuwa alikuja Dar es salaam akiwa hajui kuongea Kiswahili fasaha. Pia tukumbuke kwamba Mfalme Rumanyika wa Karagwe aliongea Kiswahili kwenye karne ya 19, miaka ya 1800, alipokutana na mzungu kwa mara ya kwanza, wakati huo Nyerere hakuwepo.
Hayo niliyoyatanguliza yanahusu tunu ambayo Watanzania tulijaaliwa na Mwenyezi Mungu, tunu ambayo chama tawala, CCM, kimekuwa muda wote kikiwalaghai Watanzania kuwa ndicho kilichoiwezesha ikawepo na kwamba ndicho kinachoendelea kuisimamia tunu hiyo isiyumbishwe.
Chama hiki kinasahau historia, pamoja na kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, mwasisi wa chama hicho, alikuwa akiihubiri mara kwa mara mpaka alipoingia kaburini, kwamba kilichomsaidia kukabidhiwa nchi na wakoloni bila kushika silaha kuidai ni umoja wa watu wa nchi yake na lugha ya Kiswahili. Ukweli huo unaonyesha kwamba hali hii tuliyo nayo ilikuwepo hata kabla ya kujitawala kwetu.
Kwahiyo kwa vile umoja huu tulio nao haukuletwa na mtu yeyote sidhani kama yupo wa kuuyumbisha, maana hata CCM yenyewe bado imeshindwa kuuyumbisha pamoja na ukweli kwamba imekuwa ikijitahidi sana kufanya hivyo kwa nyakati mbalimbali.
Kwa nini CCM itake kuuyumbisha umoja na mshikamano wa watu wa nchi yake? Hilo ni swali muhimu kwa watu wasioyafuatilia kwa karibu masuala ya chama hicho tawala. Ni kwamba chama hiki kimekuwa kikiutumia kila udhaifu unaojitokeza kwenye jamii ya Watanznia kujinufaisha chenyewe. Kwahiyo pale ambapo hakuna udhaifu kimejaribu kuulazimisha udhaifu uwepo kwa manufaa ya chama hicho.
Mfano chama hicho kinapoona kimekaribia kuondolewa kwenye ulaji ndipo kinapoanza kutishia kwamba kikiondolewa umoja wa nchi utasambaratika, amani itatoweka na Kiswahili kitayoyoma. Ni kama futuhi lakini CCM inayafanya ya kweli. Hizo zote ni kama jitihada za mfa maji.
Hebu tuangalie jinsi CCM inavyoichezea tunu ya nchi yetu ili, pamoja na mambo mengine, ijihakikishie kubaki madarakani. Kwa upande wa tunu ya lugha, Kiswahili, tunaona kwamba chama hicho kina vitu kama CC na NEC kwenye muundo wake, tumtake kada yeyote wa chama hicho aje kutufafanulia maneno hayo ni Kiswahili cha wapi kama siyo kuinajisi lugha yetu adhimu. Tunawezaje kudai kwamba chama hicho kinaienzi lugha ya taifa kwa kuifanya chotara tukiwa tumeviacha vyama vingine vyenye kutumia maneno kama BARAZA kuonyesha muundo wake ulivyo?
Tunashuhudia jinsi juhudi za CCM kukifanya Kiswahili kuwa lugha chotara zilivyopanuka na kuingia hadi Bungeni. Kwa sasa wananchi walio wengi wanashindwa kufuatilia kwa umakini mijadala ya Bunge kutokana na kutoielewa lugha chotara inayotumika bungeni kuendeshea mijadala hiyo kwa sasa. Mbunge anaongea neno moja la Kiswahili anaweka mawili ya Kingereza, huko ndiko kukienzi Kiswahili? Hata kama kwa sasa bunge lina wabunge wa kutoka vyama mbalimbali lakini utaratibu huo tayari ulikuwepo wakati wabunge wa vyama vingine wanaingia bungeni, wameukuta ukiwa umeasisiwa na chama tawala.
Utamaduni wetu; CCM imeingilia tamaduni zetu na kuanza kuzitumia kuwagonganisha vichwa wananchi, kitu ambacho hata wakoloni hawakutufanyia! Mfano tuliona namna CCM ilivyotumia imani ya Kikristo kumpenyeza mgombea wake wa urais kwenye roho za wananchi, hasa Wakristo, kwa vile mgombea huyo alikuwa Mwislamu ambaye hakuwa na tatizo lolote na watu wa madhehebu yake. Hiyo ni mwaka 2005 ambapo maaskofu walipanda kwenye jukwaa la kisiasa na kuanza kumfagilia mgombea wa CCM kuwa ni chaguo la Mungu.
Lakini baada ya chama hicho tawala kufanya mambo yaliyo kinyume cha matarajio ya wananchi wote wanaofuata imani kuu mbili, Uislamu na Ukristo, katika kipindi cha kwanza cha utawala wa mwenyekiti wake, chama hicho machale yakakicheza, kikawa hakina urafiki wala imani na yeyote. Maana kiligundua kwamba waliomuona mgombea wake kama chaguo la Mungu tayari nao walishagundua kuwa walirubuniwa na ibilisi kutoa kauli hiyo. Chama hicho kikaanza kuhisi kuwa watu wa imani hizo kuu mbili, Waislamu na Wakristo, wakiamua kuwa wamoja, ambapo tayari Waislamu nao walikuwa na mashitaka yao dhidi ya chama hicho, basi chama hicho kimekula mweleka wa mende. Ndipo CCM ikaja na ujasiri wa kimafia. Ikaamua kuirudisha mbinu ya kikoloni ya “gawanya utawale”. Kwahiyo mbinu zikaanza kufanyika za kuwachonganisha Wakristo na Waislamu.
Kama kuna kitu kiliwahi kuishtua CCM tangu iasisiwe basi kitu hicho ni ujio wa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Dk. Wilbrod Slaa. Ujio huo wa Dk. Slaa, Mkristo, ikawa turufu kwa CCM kuingiza udini kwa mara ya kwanza kwenye siasa za nchi yetu bila kujali athari ambazo zingeweza kujitokeza. CCM ikaendesha propaganda kwamba Chadema ni chama cha Kikristo kwa vile mgombea wake aliwahi kuwa padre. Kwahiyo Wakristo wakaonekana ni watu wabaya wasiopaswa kupewa urais, wakati huohuo CCM wakisahau kwamba ndani yao pia kuna Wakristo ambao chama hicho hakijali wanajisikiaje kwa msimamo wa chama chao hicho wa kwamba watu wa imani yao hawapaswi kutoa rais.
Vilevile CCM wanasahau kwamba yule wanayejidai kumuenzi huku wakiwa wamemsaliti, Baba wa Taifa, naye alikuwa Mkristo. Je, kama Wakristo hawafai Nyerere aliwezaje kuonekana anafaa kiasi hata cha kukiasisi chama hicho? Je, kwa maneno kama hayo ya hatari yanayochongwa na chama hicho tunawezaje kusema kwamba chama hicho kinauenzi utamaduni wa kutokuwa na migongano ya kiimani tuliokuwa nao hata kabla ya wakoloni kuivamia nchi yetu? Je, Wakristo waliomo kwenye chama hicho kweli wanaweza wakajihakikishia usalama wao?
Vilevile tusisahau miaka michache iliyopita Chama Cha Mapinduzi kiliwahi kuulaani Uislamu pale kiliposema kwamba chama cha CUF kilikuwa chama hatari kwa vile kilikuwa na dalili za Uislamu, kwa maana kwamba Waislamu hawana haki ya kisiasa katika nchi hii. Je, kwa mtazamo huo Waislamu walio katika CCM wanawezaje kujihakikishia usalama wao ndani ya chama hicho?
Hatari iliyopo kwa sasa ni CCM kuonekana imegota mwisho wa safari wakati safari bado ni ndefu. CCM hawana mbinu mpya za kuifanya safari iendelee kwa kasi kulingana na mazingira yaliyopo. Ndiyo maana chama hicho kinalazimika kutumia mbinu za zamani kama hizo za kuwagonganisha vichwa wananchi ili chenyewe kipate unafuu wa kupumua.
Hebu tujiulize kwa pamoja, Watanzania kweli kinatufaa chama hiki? Chama kinachofanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuzichokonoa tunu za nchi yetu tulizojaaliwa na Mwenyezi Mungu ili kuona kama kinaweza kusogeza kidogo uhai wake?
Mwisho nimalizie na uchokonozi unaofanywa na CCM katika tunu za nchi yetu kwa upande wa makabila. Imetangazwa sana kwamba kijana mmoja, mtaalamu wa kuchonga domo, sitaki kumtaja jina lake kumuongezea umaarufu wake hasi ambao Waingereza huuita “notorious”, aliyepewa nafasi ya kuwa msemaji wa chama hicho, kanukuliwa akisema kwamba yeye hawezi kuingia kwenye Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa vile si Mchagga! Kauli hiyo maana yake nini? Anataka kutuambia kwamba Wachagga ni watu wasiofaa? Hawana haki ya kuongoza nchi hii? Hawana haki ya kuwa katika vyama vya siasa?
Na kwa vile tumeelezwa kwamba kauli za kijana yule zina baraka zote za mwenyekiti wake ni lazima tuamini kwamba kauli hiyo inauweka bayana msimamo wa Chama Cha Mapinduzi kuhusu ndugu zetu Wachagga. Ni kwamba CCM haiwahitaji Wachagga. Swali ni je, Wachagga walio ndani ya CCM wako salama? Na wanasubiri nini?
Mfamaji haishi kutapatapa, kwa vile CCM imeanzisha dhambi ya kulichukia kabila moja kutokana na imani kwamba linatishia uhai wake, dhambi hiyo haiwezi kuishia kwa kabila hilo moja tu, CCM ni lazima itawachukia Wahaya, itawachukia Wasukuma, Wanyakyusa, Wahehe, Wangoni na kila kabila, maadamu tu katika kabila hilo kuna watu wanaoziona dosari kedekede ndani ya chama hicho tawala.
Nchini Rwanda, kabla ya mauaji ya kimbari ya 1994, kauli za aina hiyo za kwamba mimi siwezi kuwa wa chama fulani kwa vile sio Mtutsi zilitamalaki sana toka kwa viongozi wa chama kilichokuwa kinatawala kwa wakati ule MRD. Kilichofuatia kauli zile ni mauaji ya kimbari.
Kwa mwenendo huo wa Chama Cha Mapinduzi hakuna Mtanzania atakayebaki anaonekana wa maana kwa chama hicho, hiyo ndiyo inayonileta kwenye usemi wa Wahaya wa kwamba “ekikukwanga okyanga”, wenye maana ya kwamba likukataalo nawewe likatae. Sasa Watanzania tunasubiri nini ndani ya chama hiki kinachotuonyesha kila dalili za hatari? Mpaka kituletee kama yale ya Rwanda ndipo tuamini kwamba CCM muda wote ilikuwa imetukataa? Kila mwananchi atafakari kivyake.
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512