Bukobawadau

HONGERA HAPPINESS WATIMANYWA REDD'S MISS TANZANIA 2013

MWANADADA Happiness Watimanywa kutoka mkoani Dodoma, juzi usiku alitwaa taji la Redd’s Miss Tanzania, akiwashinda wengine 29 waliokuwa wakiliwania kutoka kwa mtangulizi wao, Bridgette Alfred.
Ushindi wa Happiness haukuwashangaza wengi katika ukumbi wa Mlimani City kwa vile alishaonyesha uwezo mkubwa tangu hatua za awali akitwaa taji la Miss Tanzania Photogenic 2013, hivyo akawa kati warembo watano walioingia hatua ya 15 bora.
Mbali ya kuvikwa taji, Happiness amebeba zawadi ya gari na fedha taslimu shilini mil. 8. Nafasi ya pili katika shindano hilo lililogubikwa na kila aina ya shangwe za wapenzi na mashabiki wa urembo na burudani, ilikwenda kwa Latifa Mohamed kutoka Kitongoji cha Kigamboni, Kanda ya Temeke.
Nafasi ya tatu ilitwaliwa na Clara Bayo ambaye awali alijitwalia taji la Miss Tanzania Sports Woman huku nafasi ya nne na tano ikienda kwa Lucy Tomeka na Elizabeth Prety.



Sisi Tanzania Daima tukiwa sehemu ya wadau wa michezo, burudani na maendeleo kwa ujumla, tunampongeza Happiness kwa mafanikio tukiamini taji halijafika kwenye mikono yake kwa bahati mbaya, bali ni kwa vile amestahili kwa mujibu wa vigezo vya shindano hilo la 21 tangu 1994.
Kwa misingi hiyo, tunampongeza kwa ushindi ambao unampa tiketi ya kuiwakilisha nchi katika shindano la dunia ambalo tangu kurejeshwa shindano hilo mwaka 1994, Tanzania haijafanya vizuri.
Japo inasikitisha na kuibua maswali mengi juu ya kushindwa huko kwa warembo wetu, lakini ndio ukweli kwani mafanikio pekee ya Tanzania katika shindano la dunia (Miss World), ni mwaka 2005, pale Nancy Sumary alipofanikiwa kuingia hatua ya sita bora.
Hiyo ikamfanya kuvikwa taji la Miss World Africa, yakiwa ni mafanikio makubwa pekee kwa vile hayajafikiwa na wengine wa kabla na baada yake ambao wamekuwa wasindikizaji na mabingwa wa kuzua sababu mbalimbali katika mazingira ya kujenga uhalali wa kushindwa.
Kushindwa huko kunatufanya turejee kwa waratibu wa shindano hilo, Kampuni ya Rhino Agency Ltd ya jijini Dar es Salaam chini Mkurugenzi Hashim Lundenga kubaini dosari zinazowafanya warembo wetu washindwe kufurukuta kila wanaposhiriki shindano hilo lenye umaarufu mkubwa.
Tunachomaanisha hapa ni Lundenga na wenzake kuonyesha kwa vitendo kiu na shauku ya kutaka warembo wetu wafanye vizuri kuanzia kwenye mfumo wa kumpata mwakilishi wa nchi na aina ya maandalizi anayopewa mwakilishi huyo kabla ya kuondoka nchini kwenda kushiriki Miss World.
Kutokana na mazingira hayo, tunampongeza Happinness kwa ushindi na tunamtakia kila la kheri katika safari yake ya kuiwakilisha nchi na kuitumikia jamii, tukiamini atakuwa balozi mzuri na si kituko kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi yao.





Jambo muhimu kwa Happiness ni kutambua kuwa kulitwaa taji hilo ni kazi ya kwanza, lakini kazi kubwa ya pili na nzito ni namna gani atalitumia ili kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii anamoishi, jambo ambalo ni mtihani mgumu uliowashinda wengi.
Happiness anapaswa kutambua kuwa Tanzania kama sehemu ya ulimwengu wa sasa, inakabiliwa na changamoto nyingi cha kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo ni muhimu kwake kutambua ni namna gani atalitumia taji hilo katika mazingira ya aina hiyo bila kupendelea kundi fulani.
Mbali ya Happiness, tunawapongeza washiriki wote tukiamini katika ushindani, suala la kushindwa ni sehemu ya shindano hilo, hivyo bila kujali mrembo ameshika nafasi gani katika kinyang’anyiro hicho, tunaamini uwepo wa kila mmoja ndio ulilifanikisha.
Tunampongeza Happiness kwa ushindi na kumtakia kila la heri katika jukumu jipya la kuitumikia jamii na  tunawakumbusha tena na tena Lundenga na wenzake kufanya kila wawezalo kumwandaa vya kutosha ili wakati ukifika awe mshindani si msindikizaji katika shindano la Miss World.



Next Post Previous Post
Bukobawadau