Bukobawadau

Jitu lenye miraba minne linapotolewa kamasi na vijitu vidogo tumshangilie nani?


Na Prudence Karugendo
 
KAWAIDA si jambo la kushangaza kwa jitu lenye miraba minne kuonesha ubabe kwa watu dhaifu. Jitu lenye miraba minne linaweza kumtishia kijana mdogo na hata kumuonea kiurahisi likiamua kufanya hivyo bila mtu yeyote kushangaa, maana maumbile yanakuwa yanashawishi uwezekano huo. Lakini inapofikia hatua ya kijana mdogo kuanza kulitunishia kifua jitu lenye miraba minne kiasi cha kudiriki kupambana nalo huku jitu lenyewe likionesha woga na wakati mwingine kupiga makele ya kwamba kijana kalishika pabaya, hata jitu hilo likija kushinda pambano baada ya kuwa limetolewa jasho na kijana mdogo, likiamua kutamba kwamba mnanionaje ni lazima lizomewe badala ya kupongezwa.
 
Anayepaswa kupongezwa ni kijana mdogo hata kama anakuwa ameshindwa, sababu kule kuthubutu kwake tu kulikabili jitu hilo ili kujaribu kukomesha ubabe wa jitu hilo ni ushindi tosha.
 
Katika hali kama hiyo kuna mambo mawili yanayojitokeza. Moja ni kwamba jitu lenye miraba minne litakuwa limeonesha  kwamba nguvu zake zimeanza kupungua na hiyo kuwa dalili ya kwamba ubabe wa jitu hilo unakaribia kutoweka. Na kwa upande mwingine ni kuonesha kuwa, pamoja na kushindwa, kijana aliyelikabili jitu hilo kaanza kukomaa na kutia matumaini ya kuukomesha ubabe na  uonevu wa jitu lenye miraba minne.
 
Kwahiyo kinachofuatia ni kuanza kudharauliwa kwa jitu lenye miraba minne wakati kijana mhusika akijijengea heshima miongoni mwa watu. Kwa hali yoyote ushindi linaokuwa limeupata jitu la miraba minne, hata kama unakuwa umepatikana kiuhalali kwa vigezo vyote, unakuwa haufai kushangiliwa na mtu yeyote. Sababu kwa mtu ambaye alikuwa hagusiki lakini baadaye akaanza kuupata ushindi kwa mbinde baada ya kuwa amekabwa na  kutolewa jasho sana, tena na mtu mdogo,  kiasi cha kuhitaji msaada wa mbinu chafu, huo ni ushindi unaodhihirisha kuporomoka kwa uwezo wa mhusika. Ni ushindi usiopaswa kushangiliwa, sanasana ni ushindi wa kuzomewa.
 
Hali kama hiyo ndiyo inayojionesha katika siasa za nchi yetu. Chama tawala,Chama cha Mapinduzi, tunaweza kukifananisha na jitu la miraba minne. Hiki ni chama cha siasa ambacho kimekaa peke yake bila mpinzani wala mshindani kwa muda mrefu. Hali hiyo ilikuwa inakipa fursa kubwa ya kujijenga kwa starehe bila misukosuko yoyote na kuwa lichama likubwa,  si katika Tanzania tu,  bali hata katika Afrika nzima. Maana ni chama kilichokuwa kikijiamria kinavyotaka bila yeyote kutia neno, wakati huo kikidai kimeshika hatamu. Kumbuka hatamu hushikiwa farasi.
 
Kutokana na kushika hatamu chama hicho kimehodhi vitega uchumi vingi mno vilivyopatikana kwa jasho la wananchi wote lakini vikang’ang’aniwa na CCM peke yake bila vyana vingine kuambulia chochote. Chama hicho pia kimehodhi mamlaka makubwa kutokana na kuwa ndicho kilichoishikilia serikali. Chama hicho ndicho kinachotoa maelekezo kwa vyombo vya dola na mwenyekiti wake ndiye Amiri Jeshi Mkuu. Hali hiyo inatosha kukiondoa chama hicho katika ushindani wa kisiasa ulio sawa na vyama vingine kutokana na kukosekana chama kingine chenye muundo kama wa kwake. CCM linabaki kuonekana kama jitu lenye miraba minne lisilokuwa na mshindani.
 
Lakini sasa hali sivyo ilivyo. CCM inao washindani tena wanaoitia wasiwasi na kiwewe kiasi cha kuifanya kupagawa. Vitu viwili vinajionesha hapa. Inawezekana ni uzembe ilioufanya wa kukosa kujipanga, tuseme jitu la miraba minne lilisahau kufanya  mazoezi kwa kuamini kwamba mwili wake mkubwa ungeendelea kulilinda kama “tisha toto” muda wote na kusahau kuwa umri ungeweza kulitupa mkono na hivyo kujikuta vijana wakiitumia nafasi hiyo kulichachafya.
 
Tumeshuhudia katika chaguzi ndogo mbalimbali ambazo chama tawala kimetolewa kamasi na vyama vya upinzani ambavyo ni vidogo kwa maana halisi ya udogo, kiumri, kiuchumi pamoja na mazingira magumu vinayowekewa na chama hicho tawala. Chama tawala kimepata ushindi wa mbinde na wenye utata huku kikibwagwa katika maeneo mengine.
 
Sasa tumekishuhudia chama hicho tawala, kikivunja kwa makusudi au kwa kutokuelewa (?) kanuni za Umoja wa Mataifa za kumtumia balozi wa nchi ya nje kukifanyia kampeni. Balozi wa China kafanya kazi za CCM hapa nchini badala ya kufanya shughuli za mahusiano kati ya Tanzania na nchi yake!
 
Kwa maana hiyo balozi huyo hawachukulii wanachama wa vyama vya upinzani kama Watanzania, yeye anaowatambua ni wana CCM tu!
 
Ni kitu gani cha kushangilia katika hali kama hiyo? Kwa upande wangu naona hiyo kama aibu ya mtu mzima kupigana na mtoto akikimbilia kushika mapanga na kuanza kutamba kuwa yeye ni kidume.
 
Mara nyingi nasikia CCM kikitamba kwamba sera zake zinakubalika, nashindwa kuelewa sera hizo zinakubalika kivipi ambapo katika kila uchaguzi mdogo tulioushuhudia zaidi ya nusu ya wapiga kula hawajitokezi kupiga kura, na wanaojitokeza, tuseme robo ya wapiga kura, wanakuwa ni wa kugombaniwa kati ya CCM na upinzani. Na CCM ikifaniwa kushinda kwa kura mbili tatu inatamba kwamba yenyewe  ni mwamba! CCM inasahau kwamba wale wote wanaokuwa hawakujitokeza kupiga kura, ambao mara zote ni zaidi ya nusu ya wapiga kura, wanakuwa wameikataa CCM ila wanakosa uamuzi kura zao wakipe chama gani.
 
Pamoja na hilo, huu mtindo wa CCM kuanza kuwatumia mabalozi wa nchi za nje katika kujinadi kwa wananchi bila uelewa wa kwamba kinakiuka kanuni za Umoja wa Mataifa, una maanisha nini kama sio kutangatanga na kuweweseka? Kwa umri kilio nao wa karibu miaka 60, kinaweza kutukumbusha ni lini kiliwahi kufanya kitu cha aina hiyo?
 
 
Jambo la kujiuliza ni moja, kama CCM inaamini kwamba inapendwa kwa nini inategemea zaidi vyombo vya dola katika kila shughuli zake? Kwa nini polisi waonekane wengi zaidi kuliko hata wapiga kura wakati wa uchaguzi. Hofu hiyo ya kuimarisha ulinzi kiasi hicho imeletwa na nini kwa chama kinachojiamini ni kipenzi cha wananchi?
 
Ni jambo la kusikitisha kwamba kwa sasa demokrasia katika Afrika imevishwa sura ya kijeshi, inakuwa vigumu kuitofautisha nchi inayotawaliwa kwa njia ya demokrasia na ile inayotawaliwa kwa njia ya udikteta wa kijeshi. Hiyo ni kutokana na watawala wengi katika Afrika kutegemea zaidi vyombo vya dola, jeshi na polisi, kuingia na kubaki madarakani kuliko wanavyowategemea wananchi kupitia katika mfumo wa demokrasia ya kuchaguliwa kwa kura.
 
Ndiyo maana katika maandalizi ya uchaguzi serikali zinaoonekana kuimarisha zaidi vyombo vya dola kuliko kuimarisha vifaa vya kufanyia uchaguzi. 
 
Tuliona Zimbabwe kwa mfano, wakati wananchi wanakufa njaa kutokana na baa la njaa lililoikumba nchi ile Rais Mugabe anayedai muda wote kuwa anawapigania watu wake,  alikuwa anahangaika kuingiza zana za kivita nchini mwake kutoka Ughaibuni ili kujihakikishia usalama katika kiti chake cha urais. Huyo ni mtu anayedai kwamba chama chake, chama tawala, kinapendwa kuliko vingine vyote nchini mwake.
 
Woga wa vyama tawala unatokana na makosa ya kubweteka vikiwa vimejisahau na kushindwa kutimiza matakwa ya wananchi,  jambo ambalo limekuwa tatizo linalogeuka ukoloni mambo leo,  ambapo wananchi wanajikuta wakitawaliwa bila ridhaa yao kupitia mfumo wa demokrasia bandia unaosimamiwa na kuendeshwa kijeshi,  mshindi akiwa ameishajulikana hata kabla wananchi hawajapiga kura.
 
Kwahiyo kinachofanywa katika kiini macho hicho kiitwacho uchaguzi ni kuwatumia wananchi kuufunika mfumo huo wa kidikteta ili  waonekane wamefanya uchaguzi wakati ikieleweka kuwa maamuzi yao hayawezi kuheshimiwa na mamlaka yoyote iwapo wanaamua kinyume na matakwa ya mamlaka husika.
 
Mfano, jambo la kujiuliza ni kwa nini serikali haioni umuhimu wa kuongeza idadi ya askari ili kukabiliana na wimbi la uhalifu linaloitetemesha nchi kwa wakati huu? Wananchi wanapoteza maisha yao wakiwa majumbani mwao, wanapoteza maisha wakiwa katika sehemu zao za biashara, wakiwa safarini, tuseme kila mahala. Serikali inaona sawa tu, ila katika Uchaguzi Mkuu ndipo inaona kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya askari. Je, umuhimu huu ni wa heri? Tuseme mwananchi anakuwa na thamani kubwa wakati wa Uchaguzi Mkuu kuliko wakati mwingine?
 
Suala la vurugu wakati wa uchaguzi linaeleweka chanzo chake ni  nini. Vurugu katika uchaguzi husababishwa na kasoro zinazojitokeza katika mwenendo wa uchaguzi, ama za makusudi au zinazoletwa na uduni wa vifaa vya kufanyia  uchaguzi. Katika kukabiliana na tatizo hilo tungetegemea kusikia vinaletwa vifaa vya kisasa zaidi kwa ajili ya uchaguzi  ili kujaribu kuondoa kasoro hizo, lakini badala yake tunaambiwa vinaletwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kukabili vurugu kana kwamba vurugu hizo zimeishapangwa na kupata baraka!
 
Tukichukulia kwamba wananchi wanapiga kura na matakwa ya walio wengi yanaheshimiwa,  kwa nini tuwe na hofu ya kuzuka vurugu? Kwa nini tuwahofie walio wachache,  ambao watakuwa wameshindwa, kwamba wanaweza kuzua vurugu kiasi cha askari wetu kuonekana hawatoshi? Kwa nini tusiamini kwamba haya pengine ni maandalizi ya kutengua maamuzi ya walio wengi? Inabidi tuutafakari kwa pamoja ukubwa wa miraba minne wa chama tawala. 
 
 
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau