Bukobawadau

Kufutwa sheria na. 20 pekee hakutoshi kuurudishia ushirika heshima yake

Na Prudence Karugendo

KABLA ya uhuru wa Tanganyika, wananchi katika maeneo mbalimbali, kwa kukitumia kilimo, walibuni njia kadhaa za kujikomboa kiuchumi. Njia moja kuu waliyoibuni ni ya kuunda vyama vya ushirika kwa ajili ya kuyashughulikia mazao yao makuu ya kibishara yaliyokuwa yakilimwa kwa lengo la kujipatia pesa.

Vyama hivyo viliwaneemesha sana wakulima kiasi cha kuwainua juu kiuchumi na kuwatofautisha sana na watu wa maeneo mengine ambayo hayakuwa na mifumo ya aina hiyo, ushirika, au yakiwa hayana kilimo cha mazao yaliyotakiwa kuuzwa hata nje ya nchi na kuwaletea kipato cha kuinua maisha yao.

Mfano katika mikoa ya Ziwa Magharibi (Kagera kwa sasa) na Kilimanjaro, kulikuwa na zao maarufu la kahawa, hilo ni zao lililokuwa likitakiwa sana nchi za nje, na mpaka sasa bado linatakiwa, likawafanya wakulima wa maeneo hayo wabuni vyama vya ushirika vya Bukoba Co-operative Union (BCU) na Kilimanjalo Native Co-operative Union (KNCU), kwa ajili ya kulishughulikia zao hilo kimasoko pamoja na mambo mengine ya kulifanya lisiweze kutetereka.

Pamoja na kuwainua wakulima wa maeneo hayo kiuchumi na kuwafanya waonekane tofauti na watu wa maeneo mengine ya nchi, kiasi cha kudhani hawatoki nchi moja, vyama hivyo vya ushirika vilikwenda mbali zaidi hata kuwainua kielimu watu hao katika maeneo husika.

Vyama hivyo viliwafadhili watoto wa wakulima, ambao wazazi wao walikuwa wanaushirika, kupata elimu nzuri na bora hapa nchini na hata nje ya nchi.

Mafanikio ya kielimu yaliyotokana na vyama vya ushirika yalionekana wazi, na mpaka leo bado yanaonekana.

Mfano, wakati Mwalimu Nyerere anasoma kuanzia Tabora, Makerere hadi Edinburgh, alisoma na wanafunzi wengi toka Ziwa Magharibi na Kilimanjaro, waliowezeshwa zaidi kufikia kiwango hicho na zao la kahawa. Hata Nyerere kwa kiasi fulani alikuwa mnufaika wa zao hilo.

Sababu hata mafanikio yake hayo aliyoyapata ya kwenda masomoni Ughaibuni, katika Uskochi, kwa ajili ya shahada na shahada ya uzamili, yalitokana na kuja kwake kufundisha katika shule ya St. Marry’s, Tabora, iliyokuwa chini ya misioni.

Pale ni Mwalimu Andrea Tibandebage, mwenyeji wa Ziwa Magharibi, aliyewashauri mapadri wa kizungu wamfuate Nyerere Makerere na kumleta pale kwa ajili ya kufundisha somo la baiolojia.

Ni mapdri hao wa kizungu waliompeleka Nyerere Scotland kwa ajili ya masomo zaidi. Kwahiyo Nyerere naye, kwa namna moja au nyingine, tayari akawa amenufaika na ushirika kupitia kwa Tibandebage.

Mhandisi wa ndege, John Nyamwihura, anatoa ushuhuda kwamba suti yake ya kwanza kuivaa alinunuliwa na chama cha kwao cha ushirika, BCU, pale kilipompeleka Wingereza kwa masomo ya juu.

Paulo Bomani, marehemu, wakati huo akijishughulisha na chama cha kwao cha ushirika, Nyanza Co-operative Union, alitoa ushuhuda jinsi alivyomfuata Nyerere kijijini kwake, Musoma, ili akashirikiane nao kuanzisha chuo kikuu pale chama chake cha ushirika kilipokuwa na mpango huo.

Hayo ni baadhi ya mafanikio yaliyojionesha katika vyama hivyo vya ushirika. Wakati huo ushirika ulikuwa ukiendeshwa kwa njia zisizokuwa za kilafi kama ilivyo sasa.

Nitoe mfano wa BCU iliyobadilishwa majina mara kadhaa wakati ufanisi wake ukididimia, ikawa KCU na sasa KCU (1990) Ltd..

Wakati chama hicho kikiendeshwa kiuadilifu, bila ulafi toka kwa viongozi wake, kilikuwa na kitengo kilichoitwa Balimi Education Fund. Kitengo hicho kiliwasomesha watoto wote wa wakulima wa kahawa waliokuwa wanaushirika.

Kitengo hicho kilifikia kuanzisha hata shule za sekondari kilizozimiliki chenyewe. Hizo ni shule za Kishoju, Kashozi na Mugeza. Lakini baadaye kitengo hicho kikaliwa kwa ulafi wa viongozi wa ushirika huo waliojitokeza baadaye, mpaka kikaisha kiasi cha kuiomba serikali iziendeshe shule hizo kilizokuwa kikizimiliki. Kitengo hicho kikawa hakina tena uwezo wa kuwasomesha tena watoto wa wanaushirika.

Mbali na shule pamoja na maendeleo ya kielimu, chama hicho kikuu cha ushirika kilikuwa nayo miradi mingi mizuri. Miradi hiyo ni pamoja na mahoteli makubwa ya kitalii, Hoteli ya Lake pamoja na Coffee Tree Inn.

Mahoteli hayo yalianza kusuasua kutokana na ulafi ulioanza kujijenga ndani ya chama hicho. Badala ya kuzihudumia hoteli kwa kiasi cha miradi hiyo kuleta ufanisi uliokusudiwa, viongozi wa chama hicho wakaamua kuyahudumia matumbo yao. Mali ya ushirika ikageuka mali ya viongozi watawala, wakiila bila kuihudumia kwa njia yoyote!

Wakulima wa kahawa, wanaushirika, wa wilaya ya Karagwe, kuona hivyo wakaamua kujitenga na kuanzisha chama chao kikuu cha ushirika. Kwahiyo ikabidi mali zigawanywe na wao kupewa, pamoja na mambo mengine, hoteli moja ya Coffee Tree Inn.

Wakati wanapewa hoteli hiyo ilikuwa katika hali ya kusikitisha, hivyo wakaifanyia ukarabati na kuiboresha, na kwa sasa ni moja ya hoteli zinazotisha katika mji wa Bukoba.

Hoteli ya Lake iliyokwenda upande wa KCU (1990) Ltd. kwa sasa limegeuzwa gofu ambalo wapangaji wake wakuu ni popo na panya. Hatahivyo gofu hilo bado linatumia kiasi cha shilingi nilioni 150 kwa mwaka likiwa limeingiza shilingi milioni moja tu kwa kipindi hicho.

Hayo yamo katika mahesabu yaliyokaguliwa ya chama hicho cha KCU (1990) Ltd..

Lakini pamoja na uzembe wote huo wa makusudi, chama hicho cha ushirika bado kinao ujasiri wa kuanzisha miradi mingine bila kujali miradi hiyo inawaathiri wakulima kwa kiasi gani.

Mfano chama hicho kimenunua hoteli nyingine ya Yasillah bila kujali kwamba tayari kinayo hoteli ya Lake ambayo, kwa sababu kinazozijua chenyewe, kimeigeuza gofu!

Vilevile kinadai kujenga nyumba ya kitegauchumi katika mtaa wa One Way, Bukoba Mjini, wakati kinavyo vitegauchumi kibao kilivyoviterekeza!

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, alipobanwa na maswali kuhusu chama hicho cha ushirika, akakiri kuwa kinaendeshwa kiufisadi na mafisadi. Akasema kwamba kila anapopeleka wakaguzi wake kwa lengo la kukikagua, watu wake wanaishia kuhongwa na mafisadi hao.

Baadaye ndipo waziri huyo akasema kwamba amelazimika kutengeneza muswada na kuupeleka Bungeni ili kutengua sheria na. 20 ya 2003, ya vyama vya ushirika.

Lakini hatahivyo yote hiyo itakuwa ni kazi bure iwapo watu walioufikisha ushirika katika hali mbaya kiasi hicho wataachwa waendelee kupeta bila kufanywa lolote.

Mdau mmoja wa ushirika amekuwa akipiga kelele akisema kwamba chama chake cha ushirika inabidi kikaguliwe na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Wazo hilo limekuwa likibezwa sana na viongozi walafi wa ushirika wakidai kwamba hicho ni kitu kisichowezekana.

Lakinisasa kimewezekana, ushirika kwa sasa utakaguliwa na CAG. Ni jambo linalopongezwa sana na wanaushirika wakisema kwamba mafisadi sasa inabidi waelewe kwamba hakuna kisichowezekana mbele ya haki.

Hatahivyo wanaushirika hao wanasema kwamba CAG anapaswa aikague KCU (1990) Ltd. walau kuanzia miaka 5 iliyopita badala ya kuanzia wakati huu uliopo. Hiyo eti ni kwa sababu madudu mengi ya wizi na ufisadi yamefanyika wakati uliopita.

Vilevile inasemwa kwamba viongozi wa ushirika, na hata waliomo serikalini, waliohusika kuufikisha ushirika katika hatua hii mbovu, ambapo CAG analazimika kuingilia mambo ya ushirika, wasimamishwe kazi wakati uchunguzi ukiendelea. Na ikibainika kuwa ni wao wanaohusika na madudu yote yanayojionesha wafilisiwe na kuchukuliwa hatua nyingine za kisheria. Wakulima, wanaushirika, wanasema hawawezi kuhangaika kuzalisha lakini wanachokizalisha kikaishia kuliwa na mafisadi wachache.

Hatua hiyo ya serikali kuamua kulifikisha suala la uteterekaji wa ushirika Bungeni imekuja kufuatia jitihada za baadhi ya wanaushirika wakereketwa kulivalia njuga bila kulala.

Lakini inaonekana wapo baadhi ya watu, wanaopaka mafuta kwa mgongo wa chupa, wakidai kwamba ndio wamesababisha muswada huo kupelekwa Bungeni, huku wakiwa wanayalinda kwa njia ya kitaalamu madhambi ya viongozi wa ushirika. Hao ni wanafiki tu.

Haiwezekani suala hilo lipelekwe Bungeni baada ya baadhi ya watu kuyapinga yote yanayodaiwa na wanaushirika wakereketwa wanaoonesha hujuma zinazofanywa dhidi yao, ikidaiwa kuwa ni uongo usio na uthibitisho, na kwa upande mwingine kwamba ni husuda kwa kukosa nafasi za uongozi katika ushirika.

Kama kweli serikali ingeamini kwamba madai ya wanaushirika ni uongo na husuda, sidhani kama ingeona haja ya kulipeleka suala hilo Bungeni. Tangu lini uongo na husuda vikafanyiwa kazi na watu wenye akili timamu?

Katika hatua nyingine meneja wa KCU (1990) Ltd., Vedasto Ngaiza, katika kuonesha kwamba magendo ya kahawa nje ya nchi ndiyo inayoudhoofisha ushirika, katumia neno “balimanyaila” lenye maana ya watatambua muda ukiwa umepita sana. Nahisi maana yake ilikuwa kwamba mpaka wakulima wa kahawa, wanaushirika, walio wengi waje kupata elimu ya ushirika na kuyashtukia wanayofanyiwa na chama chao muda utakuwa umeisha, “Balimanyaila”!

Mwisho, wanaushirika wanasema kwamba kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa mkoani Mwanza, kwamba ushirika ni sekta binafsi inayopaswa kujilinda yenyewe, ilikuwa na lengo la serikali kujipunguzia majukumu.

Wao wanaona kwamba ni jukumu la serikali kuvilinda vyama vya ushirika kama inavyoulinda usalama wa kila raia wake na mali zake. Wanasema haiwezekani mtu avamiwe na kunyang’anywa mali zake serikali idai kwamba haihusiki kwa vile aliyevamiwa ni mtu binafsi. Eti ni jukumu la serikali kuyaangalia hayo yote kwa vile yenyewe ni mali ya watu, wananchi.

Wanaongeza kwamba rais anao uwezo wa kuwatia ndani wote wanaohujumu mali za wanaushirika. Eti anaposhindwa kufanya hivyo akabaki akilalamika tu, manyang’au ndani ya ushirika wanaendeleza uporaji wao wakijua kwamba hakuna kitakachofanyika. Matokeo yake wakulima wanateketea na hivyo ushirika kuangamia na nchi kudhoofika.

prudencekarugendo@yahoo.com

0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau