Bukobawadau

MWALIMU FILBERT PAUL: Nilipigwa risasi bila kosa mkononi

KATIKA Kijiji cha Kyarutale kilichopo Kata ya Rutoro wilayani Muleba, Kagera kumekuwapo na mgogoro baina ya wawekezaji waliovamia kijiji hicho na wazawa.

Mgogoro huo uliodumu kwa muda wa miaka saba umewasababishia wananchi wa eneo hilo kupata ulemavu wa kudumu.

“Mkono wangu wa kushoko maeneo ya kiwiko umepigwa risasi, askari aliyenipiga simtambui kwa jina wala sura yake, kutokana na giza liliokuwepo eneo la tukio,” anasema Mwalimu Filbert Paul wa Shule ya Msingi Kagoma iliyoko Muleba.

Mwalimu Paul ni mmoja wa wananchi walioathirika kutokana na mgogoro huo.

Anasema kabla ya kuhamia Shule ya Kagoma alikuwa anafundisha Shule ya Msingi Kyarutale iliyoko Kitongoji cha Kyobuheke, Kata ya Rutoro, ambako kuna mgogoro wa ardhi baina ya wazawa na wawekezaji haramu (wafugaji).

Anasema wafugaji hao ambao ni wafugaji waliitaka shule hiyo ya msingi pamoja na wakazi wa eneo hilo kuondoka ili wao waendele kubaki eneo hilo kulisha mifugo yao.

Mwalimu Paul anasema wafugaji hao wamekuwa hawajali mashamba ya wananchi wa eneo hilo, wamekuwa na tabia ya kuvamia na kulisha mazao yaliyolimwa kwa makusudi bila kujali wala kuwa na woga.

Anasema Shule ya Kyarutale ilipanda miti kwa ajili ya kivuli, wafugaji hao wakaanza kuleta mifugo yao katika eneo la shule na kugeuza eneo hilo kuwa malisho ya mifugo yao.

Baada ya kuzuiwa na uongozi wa shule wao waliendelea kukaidi na badala yake walianza kuleta makundi makubwa ya ng’ombe na kufanikiwa kuharibu miti iliyopandwa kwa matumizi ya kivuli.

Aprili 2010 wanafunzi wa shule hiyo walichukizwa na kitendo hicho cha wafugaji hao kuharibu miti ya shule yao waliyokuwa wakiimwagia maji ili iweze kustawi vizuri, waliamua kuwafukuza ng’ombe waliokuwa wakishambulia miti kuondoka eneo la shule.

Anasema wakati wanafunzi wakifukuza ng’ombe kutoka eneo la shule haikuwa rahisi wafugaji hao kurudisha mifugo yao katika eneo la shule.

Walimu walipofika na kukuta malumbano baina ya wanafunzi na wafugaji waliwazuia wanafunzi wao kwa kuwataka waache kuwafukuza ng’ombe hao.

Anasema kuwa wafugaji hao walikuwapo wakati wanafunzi wanafukuza ng’ombe wakasema sasa watapambana na walimu.

Baada ya kuongea hivyo wafugaji wakavamia ofisini kisha wakaanza kuwachapa walimu kwa fimbo walizokuwa nazo, wanafunzi kuona hivyo wakaanza kuwashambulia huku wakipiga kelele zilizowavuta wanakijiji na kufika eneo la shule.

Wafugaji hao walipoona wananchi wanakuja kwa wingi waliamua kukimbia na kuondoka eneo la shule.

Anasema wananchi kwa kushirikiana na uongozi wa shule walitoa taarifa kwa uongozi wa kitongoji ambapo uongozi huo uliamua kupanga siku ya kusikiliza pande zote mbili ambayo ilikuwa Aprili 26, 2010.

Anasema kabla ya mkutano kumalizika wafugaji hao walifika katika mkutano huo na kumtaka mwenyekiti awaandikie barua ili waende polisi na mwenyekiti alikataa ombi lao na kuwataka watoe maelezo kwanini hawakufika mkutanoni ili mambo hayo yakapatiwe ufumbuzi.

“Siku iliyofuata ambayo ni Aprili 27 2010 majira ya tisa alasiri nikiwa nyumbani kwangu nilisikia muungurumo wa pikipiki nje ya nyumba yangu, kabla sijatoka nje nilivamiwa na askari wawili wakiwa na Mnyarwanda aliyefanya fujo shuleni, wakanifunga pingu na kuniambia toka ndani huku wakinieleza kupanda pikipiki tuondoke, kabla ya kupanda nilitaka kufahamu kosa langu, wakanieleza kuwa nitafahamu nikifika kituo cha polisi,” anasema Mwalimu Paul.

Anasema Mwenyekiti wa Kitongoji alipofika akawaomba askari hao kutoa utambulisho wa kuwathibitisha kama wao kweli ni askari ili waondoke na yeye lengo likiwa kudhibiti mauaji ya wananchi yanayofanywa na wanaojifanya ni askari.

Anasema askari walisogea pembeni na mfugaji waliyeenda naye wakaanza kuongea na simu huku wakipokezana wote watatu, waliporudi wakawaeleza kuwa wamewasiliana na mkuu wa upelelezi anakuja mwenyewe.

Anasema walipoelezwa hivyo aliomba wamfungulie pingu walizokuwa wamemfunga wakamueleza kuwa hawawezi kumfungua kwa vile hawana funguo.

Anasema ilipofika majira ya saa nne usiku kiongozi wa wafugaji hao alifika na kuwakuta wananchi wakimsubiri katika uwanja wa shule, mara polisi hao wakatoa amri wote walale chini akiwamo mwenyekiti kabla hawajalala risasi zikapigwa hewani.

Anasema baadaye alitakiwa kupanda gari, wakati anasimama kuelekea kwenye gari alisikia risasi ikitua kwenye mkono wake, akaanguka chini wakati huo alikuwa bado amefungwa pingu akiwa hapo chini alifika askari akaanza kumrika na tochi ya simu yake.

Anasema damu zilikuwa zikinitoka nyingi akaomba msaada wa kufungwa mkono ambapo walikubali msaada huo kisha kuchukua shuka mbili zilizokokuwa kwenye kamba nyumbani kwake wakamfunga kuzuia damu isiendelee kutoka kwa wingi.

Anasema aliandikiwa PF 3 na kupelekwa Hospitali ya Izimbya ili apate matibabu.

Kutokana na hali mbaya aliyokuwa nayo, wahudumu walikataa kumpokea wakawaeleza aende Ndolage au Bukoba. Lakini alipelekwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Muleba (Rubya) ambapo alifanyiwa upasuaji kwa muda wa saa tano.

“Binafsi nilishindwa kufungua kesi ya madai kwa kuhofia usalama wa maisha yangu,” anasema.

Anasema anakishukuru Chama cha Walimu Tanzania kwa msaada wao wa hali na mali wa kumpatia matibabu yaliyogharimu sh milioni tano wakati serikali ilitoa sh laki mbili.
Anasema katika hospitali hiyo aliyofanyiwa upasuaji alikaa siku 26 akahamishiwa Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.

Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Muleba (Rubya), Dk. Diocles Ngaiza, anakiri kufikishwa kwa mwalimu huyo hospitalini hapo akiwa amejeruhiwa mkono wake wa kushoto kwa risasi.

Gideon Mfata ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kyarutale, anasema mgogoro huo ulianza baada ya wafugaji hao kuanza kulisha mazao ya wananchi.

Anasema wafugaji hao walifika katika kata hiyo mwaka 2005 bila wananchi wa eneo hilo kuwashirikishwa na wala hakuna vitalu isipokuwa wamepewa namba.

Anasema hali ya usalama katika kata hiyo si nzuri, wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 20 kufuata kituo cha polisi kilichopo Kishuro.

Wafugaji hao wamekuwa wakiwasumbua wananchi kwa kuwanyang’anya mali zao, vyakula na wakati mwingine fedha hata kuiba mazao shambani.

na shura Jumapili
Next Post Previous Post
Bukobawadau