Bukobawadau

Sina hatia, sina hatia, sina hatia- Ruto

Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amekana mashtaka yote yanayomkabili kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama hiyo, Fatou Bensouda anayesimamia kesi hiyo, alisema watuhumiwa wawili waliofikishwa mahakamani hapo jana, Ruto na mtangazaji wa Redio, Joshua arap Sang wanakabiliwa na mashtaka matatu kila mmoja, ambayo ni kuwalazimisha watu kukimbia makazi yao, mauaji na kuchochea ghasia.
Kesi hiyo imeanza kusikilizwa siku chache baada ya Bunge la Kenya kupiga kura kutaka nchi hiyo ijitoe uanachama wa ICC, wakieleza kwamba imekuwa haina tija na inatumiwa kuwakandamiza Waafrika.
Ruto ambaye alionekana kujiamini alifika kwenye jengo la Mahakama akiwa ameambatana na baadhi ya wabunge waliosafiri kutoka Kenya hadi The Hague kwa ajili ya kumuunga mkono.
Mwendesha Mashtaka wa ICC, Fatou Bensouda alianza kwa kusoma mashtaka matatu yanayomkabili kiongozi huyo wa Kenya na akaiomba Mahakama hiyo kumtia hatiani kutokana na vurugu zilizojitokeza baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Akiwasilisha hoja ya mashtaka, Bensouda alisema kuwa Ruto ni mwanasiasa aliyejawa na kiu ya madaraka na wakati fulani aliitii kiu yake kwa gharama ya maisha ya wengine. Alieleza kuwa Ruto alianzisha machafuko alipoona shabaha yake kutwaa madaraka kwa njia ya kura kushindwa.
“Ruto alikuwa mwanasiasa mwenye nguvu sana ambaye alikuwa tayari kuratibu uhalifu dhidi ya binadamu ili kukidhi matakwa yake ya kutwaa madaraka.
Ni vigumu sana kutathmini maumivu na mateso waliyoyapata wanaume, wanawake na watoto ambao baadhi yao walichomwa moto huku macho yao yakishuhudia kile kilichotendeka. Wengi waliteswa hadi kufa huku wengine wakitimuliwa kutoka kwenye nyumba zao na kwenda kuishi uhamishoni,” alisema Bensouda katika sehemu ya hoja zilizowasilishwa na upande wa walalamikaji.
Akieleza zaidi mahakamani hapo, Bensouda alisema kuwa Ruto na wenzake waliapa kutwaa madaraka kwa njia yoyote na walipoona jaribio lao kwa kuingia Ikulu kwa njia ya kura limeshindikana walianzisha hila kwa kuchochea machafuko ya kikabila.
Alisema upande wa walalamikaji uko tayari kuthibitisha madai kwamba Ruto alihusika kuandaa mashambulizi dhidi ya wananchi wa kabila la Kikuyu.
“Tupo tayari kudhibitisha madai yetu pasipo na shaka yoyote kwamba mashambulizi ya Wakikuyu yaliratibiwa na kutekelezwa na wahusika hawa,” alisema Bensouda.
Wakati Bensouda akiendelea kuwasilisha ushahidi upande wa pili, Ruto alionekana kuwa mtulivu na wakati fulani alitikisa kichwa na kisha akanyanyua glasi ya maji na kunywa. Kuna wakati pia alitabasamu na kuendelea kufuatilia kwa makini ushahidi wa upande wa walalamika.

Ruto akana mashtaka
“ Sasa Ruto ni fursa yako kusimama na kujitetea kuhusiana na mashtaka yaliyopo mbele yako,” alisema mmoja wa majaji kwenye kesi hiyo. Wakati aliposimama Ruto hakuwa na maneno mengi mbali ya kurudia maneno yake mara tatu “Sina hatia, sina hatia, sina hatia”.
Ilipowadia zamu ya utetezi wa upande wa washtakiwa, Mwanasheria wa Ruto, Karim Khan alikosoa vikali maelezo ya walalamikaji aliyoyaita kuwa ni “uzushi” na baadhi ya washahidi walirubuniwa kwa fedha ili kutoa ushahidi wa uwongo.
“ Waheshimiwa majaji, najua haki ni muhimu itendeke, lakini katika hili hakuna ukweli wowote. Sehemu kubwa ya ushahidi uliotolewa na walalamikaji na hapa singependa nimlalamikie Bensouda kwani ushahidi huu ulikusanywa na mtangulizi wake Ocampo…hakuna ukweli wowote.
“ Ushahidi huu umekusanywa bila ya kuwepo mwongozo wa Mahakama hii waheshimiwa majaji… tena napenda nithibitishe hapa, Ruto ni mwanasiasa mwadilifu tena mtu safi aliyeletwa kwenye Mahakama hii kwa makosa,” alisisitiza Khan katika sehemu ya ushahidi wake.
Ili kuonyesha msisitizo wa hoja zake, Mwanasheria Khan alilazimika kutumia sehemu ya mahojiano yaliyofanywa baina ya Ruto na Mtangazaji wa K24 Jeff Koinange.
Inakariwa kuwa zaidi ya watu 1,200 walipoteza maisha wakati wa machafuko hayo ya baada ya uchaguzi na wengine 600,000 walifurumishwa toka sehemu zao na kwenda kuishi maeneo ya mbali kwa kuhofia usalama wa maisha.
Taarifa za hivi karibuni zinasema kuwa zaidi ya watu 40,000 bado wanaendelea kuishi kwenye makambi kutokana na makazi yao kuharibiwa.
Hata hivyo serikali ya Rais Uhuru Kenyatta wiki iliyopita ilisema kuwa hadi ifikapo Septemba 20 mwaka huu kambi hizo zitakuwa zimefungwa na wahusika wake watapatiwa msaada wa fedha ili kujenga nyuma mpya.
Baadhi ya mlolongo wa matukio muhimu kabla ya machafuko na baada ya machafuko hayo
• Rais Mwai Kibaki alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa mwezi Desemba 2007 huku mpinzani wake Raila Odinga aliyalalamikia matokeo hayo
Next Post Previous Post
Bukobawadau