Wanajeshi 6 wa Congo wafungwa jela
Wanajeshi sita wamefungwa jela nchini Congo Brazaville kwa milipuko iliyotokea katika bohari la silaha na kuwaua watu 300 mwezi Machi mwaka 2012.
Watuhumiwa wakuu akiwemo Kakom Kouack Blood mwenye cheo cha Koplo, amefungwa jela miaka 15 pamoja na kufanyishwa kazi ngumu kwa kuteketeza bohari hilo kwa maksudi katika mji mkuu Brazzaville.
Watuhumiwa wengine 26 waliachiliwa na kuondolewa lawama yoyote kuhusiana na milipuko hiyo, iliyosemekana kutokana na hitilafu ya umeme iliyosababisha moto
Milipuko hiyo iliwajeruhi zaidi ya watu 2,300 na kuwaacha wengine 17,000 bila makao.
Milipuko hiyo ilikuwa na nguvu sana kiasi cha kuvunja madirisha na paa za nyumba mjini Kinshasa DRC mbali sana na mji wa Brazaville.
Mahakama mjini Brazzaville pia ilimhukumu naibu katibu mkuu wa zamani wa baraza la usalama wa kitaifa Marcel Tsourou, jela pamoja na kufanya kazi ngumu kwa miaka mitano, kwa kuhusika na milipuko hiyo.Hii ni kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.
Congo ni nchi maskini , inayoongozwa na Rais Denis Sassou Nguesso aliyeingia mamlakani kwa mara ya kwanza miongo mitatu iliyopita akisaidiwa na jeshi.